Rafiki yangu mpendwa,
Kama umewahi kudhani kwamba huwezi kuibadili dunia umekuwa unakosea sana.
Kila mmoja wetu kuna kitu anaweza kufanya kuibadili dunia na kuifanya kuwa sehemu bora kabisa ya kuishi.

Na leo hapa unakwenda kujifunza kitu kimoja unachoweza kufanya hapo ulipo na ukaibadili sana dunia.

Kabla hujasema wewe ni mtu mdogo tu ambaye huna madhara kwenye dunia, nikukumbushe kauli ya Dalai Lama ambaye amewahi kusema kama unadhani ni mdogo sana na kuwezi kuleta mabadiliko, jaribu kulala na mbu kwenye chumba.

Najua unajua namna mdudu mdogo kama mbu anavyoweza kubadili wakati wako, hivyo pia ndivyo ulivyo na nguvu ya kuibadili dunia.

Rafiki, dunia kwa sasa inapitia changamoto kubwa sana, changamoto ambayo imeleta mkwamo mkubwa wa kiuchumi.

Njia pekee ya kuondoka kwenye mkwamo huu ambao dunia ipo ni kwa sisi binadamu wote kushirikiana kwa pamoja.

Mkwamo tunaopitia sasa kama dunia ni janga la ugonjwa wa Korona (Covid 19).
Janga hili ambalo lilianzia nchini China mwishoni mwa mwaka 2019 na kusambaa kwa kasi dunia nzima mwanzoni mwa mwaka 2020 limekuwa tishio kubwa.

Ugonjwa huu ambao unasabaishwa na vijidudu aina ya virusi, umekuwa mgumu kutibu moja kwa moja kwa sababu ya tabia za virusi.

Na kama ilivyo kwa magonjwa mengine ya virusi, njia pekee ya kuondoka kwenye mkwamo huu ni kupitia chanjo.

Chanjo ni njia ya kuufanya mwili utengeneze kinga dhidi ya kirusi anayesababisha ugonjwa bila ya mtu kuumwa ugonjwa huo.

Tuishukuru sana sayansi na maendeleo yake makubwa, kwani kwa mara ya kwanza tumeweza kupata chanjo nyingi na zinazofanya kazi ndani ya muda mfupi.

Chanjo hizo ni za teknolojia mpya kabisa na hivyo kuwa na nguvu kubwa kwenye kuzalisha kinga dhidi ya ugonjwa.

Na hapa rafiki yangu ndipo dunia inapokuhitaji mno, kwa sababu una mchango mkubwa wa kuisaidia dunia kuondoka kwenye mkwamo kwa kutumia chanjo.

Pamoja na kupatikana kwa chanjo salama na za kuweza kututoa kwenye mkwamo huu, bado kumekuwa na wasiwasi mkubwa unaochochewa na wasambazaji wa taarifa zisizo za kweli kuhusu chanjo.

Nikuombe wewe rafiki yangu ufanye kitu hiki kimoja ili uchangie katiks kuibadili dunia. Nenda kapate chanjo ya Korona.
Na kama umeshapata, basi ongea na watu wako wa karibu ukiwasihi nao wakapate.

Dunia imefika hapa ilipofika sasa kwa sababu ya maendeleo ya sayansi. Kila tunachokifurahia leo, kuanzia vyakula, vinjwaji na vifaa mbalimbali ni matokeo ya maendeleo ya sayansi.

Sayansi ina mchakato wake wa kuhakikisha kile kinachopatikana kina manufaa makubwa kuliko madhara. Na ndiyo maana tumekuwa tunaiamini kwenye mambo mengi bila hata kutaka uthibitisho.

Na kwenye hili la chanjo ya Korona, tunapaswa kuendelea kuiamini sayansi ambayo imeleta mabadiliko makubwa hapa duniani ndani ya miaka 100 iliyopita na kuachana na ushirikina ambao uliididimiza sana dunia kwa miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita.

Upingaji wa chanjo unaoendelea sasa ni ushirikina pekee, kwa sababu hautoi hoja za msingi na majibu ya kitafiti yaliyofuata mchakato wa sayansi.

Hakuna kitu kisichokuwa na madhara kabisa, huwa tunapima madhara na faida na pale faida inapokuwa kubwa kuliko madhara, tunakuwa tayari kwa madhara hayo ili tuipate faida.

Rafiki yangu mpendwa, nenda kapate chanjo na washawishi wengine nao wapate chanjo.
Usiwe miongoni mwa wale wanaosambaza habari za uzushi kuhusu chanjo.

“Tunaamini kwenye sayansi ambayo imeiwezesha dunia kupiga hatua kubwa kwa miaka 100 iliyopita na siyo ushirikina ambao uliidumaza dunia kwa miaka zaidi ya elfu 2 iliyopita. Nenda kapate chanjo ya korona.” – Kocha Dr Makirita Amani

Hii ni nafasi yako ya kuchangia katika kuibadili dunia.
Mimi rafiki yako nimeshaipata chanjo, na nimechukua nafasi kukusihi nawe ukapate chanjo.
Chukua hatua hizo mbili pia, pata chanjo na wasihi wengine nao wapate chanjo.

Kwa pamoja tunaweza kuisaidia dunia kutoka hapa ilipokwama, kwani kadiri wengi wanavyokataa chanjo, ndivyo kirusi hiki kinapata nafasi ya kusambaa na kubadilika, kitu kinachokuwa kigumu kudhibiti.

Kama bado una maswali kuhusu uhakika na usalama wa chanjo, nimeandaa maelezo rahisi kabisa, unaweza kuyasoma kwa kupakua hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/wp-content/uploads/2021/08/Darasa-Chanjo-ya-Covid-19.pdf

Nenda kachukue hatua sasa rafiki yangu, dunia inahitaji sana msaada wako kwa sasa.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
http://www.somavitabu.co.tz