Rafiki yangu mpendwa,
Ule ushauri maarufu kabisa wa nenda shule, soma kwa bidii, faulu vizuri na utapata kazi ya uhahika, inayolipa vizuri na kukuwezesha kuwa na maisha mazuri, haufanyi tena kazi.

Wengi wamefuata ushauri huo, wakasoma kwa bidii katika ngazi zote za elimu, wakapata ufaulu mkubwa na kuweza kudahiliwa kwenye vyuo vikuu.

Huko pia wakaweka juhudi kwenye masomo na kupata ufaulu mzuri.
Wanahitimu wakiwa na matumaini makubwa kwamba wanakwenda kupata kazi nzuri.

Maana ndiyo wimbo waliokuwa wanaimbiwa kila siku na hata kuonyeshwa mifano ya wahitimu wengine waliosomea kile wanachosomea, ambao wamepata kazi nzuri.

Ni pale wahitimu wanapoingia mtaani ndiyo wanakutana na uhalisia ambao hawakuutegemea, mambo yanakuwa ni tofauti kabisa na mategemeo waliyokuwa nayo.

Pamoja na kuwa na ufaulu mzuri, nafasi za kazi hakuna.
Na hapo wanakuwa njia panda kwani hawajui wakamlaumu nani kwa ushauri waliopewa kwa uhakika na sasa haufanyi tena kazi.

Wanajitokeza watu na kuanza kuwalaumu wahitimu wao kwa kuwaita ni wazembe, kwamba kwa nini wanashindwa kujiajiri wao wenyewe licha ya kupata elimu kubwa?

Watu hao wanajiona wanawashauri vizuri ili kuwasaidia, lakini ushauri wao huo unakuwa hauna msaada wowote.

Mtu aliyekaa darasani kwa zaidi ya miaka 16 (7 + 6 + 3+) akiandaliwa kwenda kuwa mwajiriwa, kumwambia ghafla aende akajiajiri, tena kwa maneno tu bila mafunzo haina msaada wowote, ni kuwadhihaki tu.

Wengine wamekuwa wanatumia mifano ya wachache ambao pia ni wahitimu waliokosa ajira na kuchukua hatua ya kwenda kujiajiri.
Kwa nje utawaona ni wahitimu, lakini kwa ndani kuna kitu wanacho ambacho wengine hawana na hicho ndiyo kinawasukuma.

Hatuwezi kusubiri wachache wenye msukumo wa tofauti ndiyo wachukue hatua. Na pia hatuwezi kuwatupia tu maneno wahitimu kwamba wanapaswa kwenda kujiajiri na kuona tumewasaidia sana.

Kama tunataka kweli kuwasaidia wahitimu kuingia kwenye uhasiriamali na kujiajiri, lazima tuwe na mkakati wa  makusudi wa kuwajengea uwezo na uzoefu ambao utawawezesha kufanikiwa kwenye hilo.

Kabla ya kuangalia ni namna gani ya kuwasaidia wahitimu kwenye hili, tuangalie kanza ukweli kuhusu ujasiriamali ambao huwa hauwekwi wazi.

1. Ujasiriamali ni mgumu.
Unamhitaji mtu kujitoa kweli kweli kwa sababu anahitajika kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.
Unapokuwa mjasiriamali wewe ndiye mtengenezaji wa bidhaa/huduma, wewe ndiye mtu wa masoko, mauzo, huduma kwa wateja na mengine mengi.
Wahitimu wanakuwa wamefundishwa kubobea kwenye eneo fulani tu, wakati ujasiriamali unamtaka mtu afanye mambo mengi.

2. Ujasiriamali ni hatari.
Katika biashara 100 zinazoanzishwa, 80 zinakuwa zimekufa kabisa ndani ya miaka 5 tangu kuanzishwa, 15 zinakuwa za kawaida ambazo bado ni mzigo kwa waanzilishi na 5 pekee ndiyo zinakuwa na mafanikio makubwa.
Unaweza kujionea hapo jinsi hatari ilivyo kubwa, yaani nafasi ya kushindwa ni kubwa kuliko ya kushinda.
Wahitimu wapya hawana uwezo wa kukabiliana na hatari kubwa kama hiyo.

3. Ujasiriamali ni kutengeneza timu sahihi.
Wengi hudhani ujasiriamali ni kuwa na wazo bora na la kipekee tu. Huo siyo ukweli, mafanikio ya biashara yoyote ile hayategemei sana wazo, bali watu wanaolifanyia kazi wazo hilo.
Kupata watu sahihi wa kushirikiana nao kama waanzilishi ni changamoto kubwa. Wengi huwa wanapenda mafanikio ya haraka.
Lakini pia kupata wafanyakazi sahihi wa kuanza nao ni kitu kigumu mno, mwanzoni mwa biashara kazi zinakuwa nyingi huku malipo yakiwa kidogo.
Lazima mjasiriamali apambane sana kupata watu watakaoelewa maono yake na kuungana naye kuyapambania mpaka yafanikiwe.

4. Ujasiriamali utakutenga na jamii.
Hatua za awali za biashara zinakutaka ujitoe kweli kweli ili kuweza kufanikiwa. Inakutaka uachane kabisa na mambo yote ya kijamii.
Biashara ndiyo kipaumbele cha kwanza kwako, masaa 24 ya siku na siku 7 za wiki.
Muda wa mapumziko kwako unakuwa mdogo sana na ni ule muda tu unaolala.
Starehe na anasa mbalimbali unapaswa kuachana nazo kabisa.
Njia mbalimbali za kuburudika, iwe ni kukutana na marafiki baa, kuangalia michezo mbalimbali au kuzurura mitandaoni unakuwa huna.
Huwezi kupata muda wa kuhudhuria kila aina ya shughuli za kijamii, iwe ni sherehe, misiba, vikao mbalimbali n.k.
Ujasiriamali unakutenga kabisa na jamii kwa kipindi kifupi kama unataka ufanikiwe.

5. Ujasiriamali siyo kwa ajili yako.
Unapofanikiwa kama mjasiriamali, utapata mengi mazuri, lakini siyo wewe pekee unayekuwa umenufaika. Bali jamii nzima inakuwa imenufaika pia.
✔Utakuwa umetatua changamoto ambayo watu wanayo kwenye jamii na hivyo kuongeza thamani kwenye maisha yao.
✔Unakuwa umezalisha nafasi mpya za ajira ambapo utaweza kuwaajiri wengine na hivyo kupunguza tatizo la ajira.
✔Unakuwa mfano mzuri kwa wengine na kuwapa hamasa ya kuingia kwenye ujasiriamali pia.
Hivyo unapoingia kwenye ujasiriamali, usijiangalie wewe mwenyewe, bali angalia wengi watakaonufaika na kile unachokwenda kufanya.

Jinsi ya kuwasaidia wahitimu kuingia kwenye ujasiriamali.

Baada ya kuliona tatizo na ukweli kuhusu ujasiriamali, sasa tuone jinsi tunavyoweza kuwasaidia wahitimu kuingia kwenye ujasiriamali.

1. Kuunda vikundi vinavyokuwa mtandao wao wa mafanikio.
Tumeona jinsi ujasiriamali ulivyo na hatari kubwa.
Na mtu anapoingia kwenye ujasiriamali peke yake, hatari hiyo anaibeba yeye peke yake.
Njia ya kupunguza hatari hiyo ni kuunda vikundi ambapo wahitimu wenye mitazamo inayoendana na ndoto kubwa wanakuwa karibu na kutengeneza mtandao wao wa mafanikio.
Vikundi hivi vinakuwa na malengo matatu;

Moja ni kuwa sehemu ya kuwajibishana wao kwa wao. Mtu anapoingia kwenye ujasiriamali peke yake ni rahisi kukata tamaa na kuishia njiani. Lakini anapokuwa na wengine wanaojua anachofanya na wapi anataka kufika, hawatamuacha kirahisi.

Mbili ni kujenga fursa ya kupata mitaji ya kuendesha biashara zao. Mtaji ni changamoto na kwa mtu mmoja mmoja ni changamoto kubwa zaidi. Lakini watu wanapokuwa kwenye kikundi ambacho wanajuana kweli ni rahisi wao kwa wao kuchangishana mitaji ya kuendesha biashara zao. Lakini zaidi inakuwa rahisi kupata ufadhili wa kifedha, iwe ni zuruku au mikopo kutoka taasisi mbalimbali. Hatari ya fedha kupotea ni ndogo kwa kikundi kuliko kwa mtu mmoja mmoja.

Tatu ni kuwa sehemu ya kupata timu sahihi. Tumeona umuhimu wa timu kwenye ujasiriamali na hatari ya kushindwa. Wale wanaokuwa kwenye kikundi kimoja wanakubaliana kwamba wale ambao biashara zao zitafanikiwa, watawaajiri wale ambao biashara zao zitashindwa.
Kwa kuwa tumeona kwenye kundi lolote biashara chache zinafanikiwa na nyingine kushindwa, hilo linapunguza hatari kwa wanaoshindwa, kwani wanakuwa hawajaanguka kabisa, bali wana mahali pazuri pa kuanzia tena.

Vikundi vina changamoto zake lakini watu wakichujwa vizuri na kuwekwa kwenye vikundi sahihi, matokeo yatakuwa mazuri.

2. Kuwaunganisha wahitimu na waanzilishi wa biashara mpya.
Wahitimu wengi hukimbilia kuomba kazi kwenye mashirika makubwa. Kitu ambacho ni kigumu kwao kwa sababu mashirika hayo hayana nafasi nyingi za ajira.
Lakini wakati huo huo kuna watu wanaanzisha biashara zao mpya na wana uhitaji mkubwa wa watu wa kuwasaidia, ila hawapati wenye sifa.
Kama wahitimu wakiunganishwa na wale wanaoanzisha biashara mpya, itakuwa na manufaa mazuri kwao.
Wanapata nafasi ya kujijengea uzoefu wa moja kwa moja kwa kuwa wanafanya mengi wakiwa kwenye biashara changa kuliko wakiwa kwenye biashara kubwa.
Hilo linawapa ujasiri wa kwenda kujiajiri wenyewe wakiwa wanajua namna ya kuepuka hatari mbalimbali.

Wengi wanaoanzia kazi kwenye mashirika makubwa kwa lengo la kuja kuacha kazi na kujiajiri baadaye hawafanikiwi kufanya hivyo. Kwani wanapokuwa kwenye mashirika hayo makubwa wanajikuta wakiwa tegemezi kwenye uhakika na kuogopa sana hatari.
Kwenye biashara changa mtu anaziona hatari waziwazi na kuweza kukabiliana nazo, kitu kinachompa ujasiri wa kwenda kufanya mwenyewe.

3. Kuwa na mamenta kwa ajili ya wajasiriamali wapya.
Kuna wajasiriamali wengi ambao wameweza kufanikiwa licha ya kuanzia chini na kukabiliana na magumu mengi.
Hao ni walimu wazuri kwa wajasiriamali wapya.
Kukitengenezwa mfuno wa kila mjasiriamali mpya kuwa chini ya uangalizi wa mjasiriamali ambaye ameshapiga hatua, itakuwa na msaada mkubwa kwa kuwajenga wajasiriamali wapya wengi na kuwawezesha kufanikiwa.

4. Kuwepo kwa sera zinazochochea wahitimu kuingia kwenye ujasiriamali.
Kuna baadhi ya vijana huwa na mawazo mazuri ya biashara, lakini urasimu ukiopo kwenye kurasimisha biashara unakuwa kikwazo kwao.
Mtu anapaswa kupata leseni ambayo atailipia na kuanza kukipa kodi hata kabla ya biashara kuanza au hata kutengeneza faida.
Bado kuna vibali vingine vinavyokuwa vinahitajika, ambavyo ni gharama na mlolongo wa kuvipata ni mrefu.
Kunapaswa kuwepo kwa sera nzuri inayovutia vijana kuingia kwenye ujasiriamali.
Mfano miaka miwili ya mwanzo ya biashara yoyote mpya inayoanzishwa na mhitimu au kijana yeyote asilipe gharama mbalimbali kama leseni, kodi na nyinginezo.
Mwanzo wajasiriamali wapya wasajiliwe na kuweza kufanya biashara zao bila ya usumbufu na baada ya miaka miwili ndiyo waanze kulipa gharama mbalimbali.
Biashara yoyote inayovuka miaka miwili inakuwa na ukomavu wa kuweza kuendelea.
Kwenye hili haimaanishi biashara ziendeshwe kiholela, bali usajili na vibali vyote vitolewe kulingana na vigezo, ila gharama na urasimu visiwe kikwazo.

5. Mfumo wa elimu ufanyiwe marekebisho makubwa.
Kama tulivyoona hapo juu, ni kichekesho kumwandaa mwanafunzi kuwa mwajiriwa kwa miaka zaidi ya 15 halafu kuja kutegemea abadilike na kufikiria kujiajiri ndani ya muda mfupi.
Mfumo wa elimu unahitaji matekebisho makubwa na kikubwa cha kuanza nacho ni kufundishwa kwa somo la ujasiriamali kwa vitendo na siyo nadharia.
Hapo inamaanisha wanafunzi kuanzisha biashara za kweli wakiwa mashuleni au vyuoni na ambazo zitaendelea kuwepo hata baada ya wao kuhitimu.
Biashara ambazo watu wanalipa fedha kabisa na kupata huduma au bidhaa ambazo wana matumizi nazo.
Kwa kujifunza elimu ya ujasiriamali kwa vitendo kutampa mwanafunzi manufaa matatu;

Moja ni kufungua fikra zake na kumwezesha kuyaona matatizo na changamoto kama fursa na kuzitumia kuanzisha biashara.

Mbili ni kujenga mtandao sahihi ambao ataweza kuutumia kwenye safari yake ya baadaye. Wale anaoshirikiana nao shuleni ataweza kushirikiana nao vizuri kwenye maisha ya baadaye.

Tatu ni uzoefu wa kuanzisha biashara na ikafanya kazi, hilo litampa ujasiri wa kufanya hivyo tena.

Bila ya kubadili mfumo wa elimu, tutaishia kuwalaumu wahitimu bure kwa kitu ambacho wao wenyewe hawajui namna gani ya kukivuka.

Tuanzie wapi?

Baadhi ya hatua nilizoshirikisha hapa zinahitaji serikali kuchukua hatua. Kitu ambacho huwa kinachukua muda mrefu.
Tatizo tunalo sasa na linazidi kukua, hapa kuna hatua za mimi na wewe kuchukua katika kusaidia hili.

1. Kama ni mhitimu, tafuta wenzako ambao mnaendana kumtazama na mna ndoto kubwa, tengenezeni kikundi na anzeni ujasiriamali kwa hatua ndogo kabisa. Angalieni changamoto zinazowazunguka pale mlipo na anzeni kuzitatua.

2. Tuwaunge mkono wajasiriamali wachanga kwa kununua kile wanachouza. Hilo linawapa nguvu ya kuendelea.

3. Tuwachangie wajasiriamali wachanga mitaji kama tunavyochangia kwenye sherehe na misiba. Hata kama mchango ni kidogo, unatosha kuleta mabadiliko.

4. Tusiwe wakatishaji tamaa kwa wahitimu na vijana wanaokuja na mawazo mapya ya kibiashara, tuwatie moyo na kuwasaidia wafanikiwe.

5. Kama ni mjasiriamali uliyeweza kupiga hatua, chagua wajasiriamali wadogo utakaowaongoza ili nao wafanikiwe.

Kila mmoja wetu ana kitu cha kufanya na tukasaidia kutatua tatizo hili linalozidi kukua kwa kasi huku juhudi za kulitatua zikiwa haziendi kwa kasi kubwa.

Leo saa mbili usiku kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA tutakuwa na mjadala wa kitabu kinachoitwa SMART PEOPLE SHOULD BUILD THINGS ambacho kimeandikwa na Andrew Yang.
Kwenye kitabu hicho, Yang ameonyesha kwa mfano jinsi anavyofanyia kazi changamoto hiyo ya ajira kwa wahitimu.

Karibu kwenye mjadala tujifunze kwa kina zaidi. Kama bado hujawa mwanachama wa SOMA VITABU TANZANIA tuma ujumbe kwa telegram kwenda namba 0717 396 253 ili uweze kuunganishwa, ushiriki mjadala wa leo na mingine ya kila wiki.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.
http://www.somavitabu.co.tz

Vitabu viwili muhimu kwako. Cha una nguvu ya kutenda miujiza kinakuonyesha uwezo mkubwa ulio ndani yako. Cha Elimu ya msingi ya biashara kinakupa mwongozo wa kuanzisha na kukuza biashara yako. Jipatie nakala kwa kuwasiliana na 0752 977 170