2444; Hakikisha Una Pa Kusimama.
Utegemezi uliopitiliza kwa wengine ndiyo kitu kinachowayumbisha wengi na kuwazuia kupata mafanikio makubwa.
Ni kweli unawahitaji sana wengine na ushirikiano wao ni muhimu kwa mafanikio yako.
Lakini kama unawategemea wengine kwa kila kitu na huna pa kusimama mwenyewe, unakuwa kwenye hatari kubwa.
Unapowategemea wengine kwa kila kitu unajikuta unategemea zaidi huruma yao kuliko msimamo wako ili kufanikiwa.
Unakuwa umewapa nguvu ya kukuamulia ufanye nini na kwa kiwango gani.
Unawapa mpanga nguvu ya kuamua ni kiasi gani upate.
Sasa kama unawapa watu uhuru mkubwa kiasi hicho kwako, ni vigumu sana kwako kupata mafanikio makubwa.
Mafanikio makubwa yanakutaka uwe na mahali unapoweza kusimama wewe mwenyewe bila ya kuyumbishwa na yeyote yule.
Unapokuwa na utegemezi uliopitiliza kwa wengine, huwezi kuwa na msimamo wa aina hiyo.
Kama unategemea kipato cha ajira pekee kuendesha maisha yako, kuna msimamo huwezi kuwa nao kwenye kazi yako.
Kama biashara yako inategemea mteja mmoja mkubwa ndiyo iweze kujiendesha, kuna namna atayumbisha msimamo wako.
Na kama unawategemea wengine wakusifie ndiyo ujione wa maana na unayekubalika, utahangaika na mengi yasiyokuwa na tija kwako.
Kwenye kila eneo la maisha yako, hakikisha una mahali unapoweza kusimama peke yako hata kama wengine wote wako tofauti na wewe.
Hakikisha hulazimiki kufanya kitu ili tu kuwaridhisha wengine, wakati ndani yako unajua hicho siyo kitu sahihi kufanya.
Utajaribiwa sana kabla hujapata mafanikio makubwa.
Na kama hutakuwa na mahali unapoweza kusimama peke yako, mafanikio makubwa yatakuwa ndoto kwako.
Hatua ya kuchukua;
Kwenye kila eneo la maisha yako, angalia wapi na kwa namna gani unaweza kusimama peke yako.
Haimaanishi usishirikiane na wengine au uwadharau, bali jihakikishie hata kama kila mtu atakuwa kinyume na wewe au kushindwa kukuelewa, una mahali pa kuendelea kusimama na kufanya kilicho sahihi kwako.
Hiyo ndiyo hatua ya msingi kabisa kwako kupata mafanikio makubwa.
Tafakari;
Kama umewapa wengine nguvu ya kukufanyia wewe maamuzi, umeshatengana na mafanikio makubwa.
Unapaswa kufanya maamuzi yako mwenyewe na kuweza kuyasimamia kwa gharama yoyote ile ili uweze kufanikiwa.
Kocha.
Asante Sana kocha, naendelea kupambana ili kusimama mwenyewe.
LikeLike
Vizuri.
Kila la kheri.
LikeLike
Ahsante kocha , hakika mafanikio ya kweli Ni kusimama kwa miguu yako mwenyewe bila kuyumbishwa na kitu chochote
LikeLike
Kabisa.
LikeLike