Sikilia hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Dunia haijawahi kuwa na shida na watu wanaoridhika na maisha ya kawaida. Itahakikisha wanapata chakula na mahitaji ya kuwawezesha kuendelea kuwa hai. Lakini kwa maisha ya aina hiyo, wengi wanapita hapa duniani kama minyoo, kwani wanapoondoka, hakuna alama yoyote wanayoacha.
Ni mpaka pale mtu unapotaka kufanya makubwa, ambayo ni tofauti kabisa na mazoea yaliyopo, ndipo dunia inakuonyesha makucha yake. Dunia haitakuachia kirahisi upate mambo makubwa unayoyataka.
Na siyo kwamba dunia haitaki upate makubwa, bali inataka kuhakikisha inatoa makubwa kwa wale kweli wanaoweza kuyatumia vizuri. Asili inajua watu wengi hawana uwezo wa kutumia makubwa wanayopata kwa manufaa ya wengine.
Na ndiyo maana huwa inamjaribu kwanza mtu kabla ya kumpa kile anachotaka. Na kadiri mtu anavyotaka makubwa, ndivyo majaribu yake yanavyokuwa makubwa pia.
Kwa wachache ambao wanapata njia ya kukwepa majaribu hayo ya dunia na kupata mambo makubwa bila kuyashinda majaribu, unajua kinachowatokea. Waangalie watu wengi walioshinda bahati nasibu au kupata mirathi na fursa nyingine kubwa. Huwa wanaishia kupoteza kila kitu ndani ya muda mfupi.
Kwenye haya majaribu ambayo asili huwa inampa kila mtu, wengi hushindwa kwa sababu ya kutokujua ni karibu kiasi gani wanakuwa na kupata matokeo wanayotaka. Wapo watu waliokata tamaa wakiwa wamekaribia kabisa kupata matokeo waliyokuwa wanayapambania.
Hivyo, kama kweli unayataka mafanikio makubwa, unapaswa kuchagua njia ya kuyafikia mafanikio hayo na kuhakikisha unabaki kwenye njia hiyo bila kuondoka. Hata pale mambo yanapokuwa magumu kabisa, hupaswi kuacha kupambania kile unachotaka.
Ili uweze kuendelea licha ya kukabiliana na mambo yanayokatisha tamaa, unapaswa kujipa miiko binafsi. Miiko hiyo ni misingi yako binafsi ambayo kamwe hupaswi kuivunja. Ni mambo ambayo utayasimamia kwenye siku zote za uhai wako. Kwa kuwa na miiko hiyo na kuiishi, hakuna kitakachoweza kukuzuia kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kupata miiko mitano ya kujipa ili uendelee kubaki kwenye safari yako ya mafanikio licha ya magumu utakayoyapitia.

1. Kamwe Usiwe Na Haraka
Hesabu zozote za mradi wowote unaotaka kufanya, huwa zinaonyesha matokeo makubwa na ya haraka. Iwe ni mpango wa mradi wa kuku, unaweza kuhesabu tu kirahisi, ukianza na mitetea 10, kila mmoja akataga mayai 10, wakatamia na kuangua, ndani ya mwezi 1 unakuwa na mitetea 10 na vifaranga 100. Ukirudia kila baada ya miezi mitatu, ndani ya mwaka utakuwa na kuku zaidi ya 500. Na wale vifaranga nao wakikua na kuanza kutaga na kutamia …. Nadhani unaipata namba.
Ni mpaka pale utakapoenda kuanza na hao mitetea 100, wanataga 8 badala ya wote 10, na watano tu ndiyo wanataga mayai 10, wengine ni chini ya hapo. Na wanapotamia, nusu ya mayai yanaharibika, hivyo unapata vifaranga 20. Na mpaka vifaranga hao wanamaliza mwezi, wamebaki 10 peke yake.
Ukiwa na haraka, utaona mradi huo wa kuku haufai na ukisikia mradi mwingine rahisi na wa haraka zaidi, unaukimbilia. Unaenda kwenye matikiti, au vitunguu, au nyanya, au chochote ambacho hesabu zake zinaonyesha matokeo ya haraka.
Ukweli ni kwamba, kila kitu ambacho unaona kinaleta matokeo makubwa kwa wengine, wamekuwa wanakifanya kwa muda mrefu. Walipokuwa wanaanza hawakuwa wanapata matokeo makubwa kama yanayoonekana sasa. Ni baada ya kufanya na kujifunza kwa muda mrefu ndiyo wameweza kupata matokeo makubwa.
Kamwe usiwe na haraka. Haraka iwe mwiko kabisa kwako. Umeshajua unachotaka na umeshajua unachopaswa kufanya. Wajibu wako ni kufanya na kuendelea kuboresha na baada ya muda utapata kile unachotaka. Weka kazi na jipe muda, utafika kule unakotaka kufika.
2. Kamwe Usiwe Na Hofu
Nikikuambia upite kwenye makaburi usiku, utajiamini kiasi gani kufanya hivyo? Na hata kama utajiamini na kupita, halafu ukakutana na kitu kimevalia mavazi meupe, utachukuliaje?
Kwa walio wengi, kupita sehemu ya makaburi usiku ni kitu ambacho hawana uthubutu wa kufanya. Japokuwa wanaweza kupita kwenye makaburi hayo mchana, ila kunapokuwa na giza, wanashindwa kufanya hivyo.
Ukiangalia tofauti ya hayo makaburi wakati wa mchana na usiku haipo kabisa. Lakini inapokuja kwenye fikra, tofauti ni kubwa. Kwani wakati wa giza, akili za watu zinafikiria makaburi yakiwa na vitu visivyokuwa vya kawaida.
Vitu ambavyo havipo kabisa, vitu vya kufikirika tu. Na hivyo ndivyo hofu inavyofanya kazi. Chochote kile ambacho watu wanahofia, huwa hakipo kabisa. Ni kitu tu cha kufikirika. Na sehemu kubwa ya vitu ambavyo watu wanahofia, huwa havitokei kabisa.
Kama unataka mafanikio makubwa, lazima ujipe mwiko kwenye hofu. Kamwe usiwe na hofu. Ndiyo, usihofie kitu chochote. Unapotaka kufanya kitu, wewe fanya. Matokeo yoyote yatakayokuja utakabiliana nayo.
Ukiwa mtu wa hofu, kamwe hutakuja kufanya chochote kikubwa. Kwa sababu kila unapoangalia kikubwa unachotakiwa kufanya, unaona uwezekano mkubwa wa mambo kwenda tofauti na unavyotarajia.
Hata kama mambo yataenda tofauti na matarajio, bado ni bora kufanya kuliko kutokufanya kabisa. Ishinde kila aina ya hofu inayokuzuia kuchukua hatua unazojua unapaswa kuchukua ili kupata matokeo unayoyataka.
Na njia nzuri ya kutumia hofu ni kuifanya kuwa mwongozo wako. Kile unachohofia kufanya, ndiyo unachopaswa kukifanya zaidi. Wakati wengine wanaacha kufanya pale wanapokutana na hofu, wewe unaitumia hofu kama msukumo wa kufanya zaidi.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK121; Jipe Hii Miiko Binafsi Itakayokuwezesha Kupata Mafanikio Makubwa