Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Sisi binadamu ni viumbe wa kihisia zaidi kuliko mantiki. Huwa tunasukumwa kuchukua hatua kwa hisia kwanza, kisha tunahalalisha hilo kwa mantiki. Bila ya hisia, ni vigumu sana kwetu kuchukua hatua ambazo tunapaswa kuchukua.

Hisia ambazo zinatusukuma binadamu zipo nyingi, ambazo zimegawanyika kwenye makundi mawili. Kundi la kwanza ni hisia chanya, ambazo zinatusukuma kupata kitu fulani ambacho ni kizuri. Hisia hizi ni kama tamaa na mapenzi tunayokuwa nayo juu ya kitu fulani.

Kundi la pili ni hisia hasi, ambazo zinatusukuma kuepuka kitu fulani ambacho ni kibaya. Hisia hizi ni kama hofu na hasira tunazokuwa nazo juu ya kitu fulani.

Kati ya hisia hizo chanya na hasi, hisia hasi huwa zina nguvu kubwa kwenye kutusukuma kuchukua hatua. Nguvu hiyo kubwa ya hisia hasi inatokana na mambo mabaya ambayo tunakuwa tunataka kuyaepuka au kuyazuia yasitokee.

Moja ya hisia ambazo zina mchango mkubwa kwenye mafanikio tunayoyataka ni hasira. Hasira ni dawa na sumu inayoathiri sana mafanikio tunayoyataka. Kama dawa inatupa msukumo wa kupambana kuyapata mafanikio. Lakini kwa upande mwingine, hasira hizo hizo zinaweza kuvunja mafanikio tuliyoyapata, na hapo zinageuka kuwa sumu.

Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza jinsi ya kuzitumia hasira kwa uangalifu ili kupata mafanikio makubwa na kujiepusha na madhara yanayotokana na kushindwa kudhibiti hasira unazokuwa nazo.

1. Hasira Kama Moto Wa Mafanikio.

Maisha ya binadamu hapa duniani yalibadilika sana baada ya kugundua moto. Ugunduzi wa moto ndiyo ulileta mapinduzi makubwa, kuanzia kwenye kupika chakula, kuleta ulinzi na kuzalisha zana ambazo zilitumika kuleta matokeo makubwa.

Utengenezaji wa zana mbalimbali kwa kutumia chuma na hata kupatikana kwa injini iliyorahisisha shughuli nyingi, vilitokana na moto. Moto umeendelea kuwa kitu chenye manufaa makubwa kwa maisha yetu hapa duniani.

Lakini moto huo pia umekuwa na hatari kubwa ya kuleta hasara na uharibifu. Moto unaposhindwa kudhibitiwa vizuri, unaharibu vitu. Moto pia umegeuka kuwa silaha ambayo imetumika kuumiza na kuangamiza watu na mali zao.

Pamoja na hatari na hasara hiyo kubwa ya moto, bado tunaendelea kuutumia moto, tukiwa na tahadhari ya kutuepusha na hatari hizo. Hata mtu ambaye vitu vyake vitaungua na kuteketea kwa moto, bado ataendelea kutumia moto. Hakuna anayeweza kukwepa kutumia moto kwenye maisha yake.

Hivyo pia ndivyo hasira ilivyo. Hasira inaweza kumsukuma mtu kufanya makubwa sana kwenye maisha yake. Inaweza kuwa hasira ya kukosa kitu fulani ambacho mtu amekuwa anakitaka sana. Hasira hiyo inamfanya ajisukume ili aweze kukipata. Kwa njia hiyo, hasara inakuwa ni dawa na kichocheo kwenye mafanikio.

Lakini kwa upande mwingine, hasara imekuwa sumu inayoweza kukwamisha na kuua kabisa mafanikio anayoweza kuwa nayo mtu. Kwa kusukumwa na hasira, mtu anaweza kufanya kitu au vitu ambavyo vinavunja mafanikio aliyojenga au kumzuia asipate mafanikio makubwa.

Upande mbaya wa hasira umekuwa ndiyo unatumika kuihukumu na kuifanya ionekane kama kitu ambacho ni kibaya. Upande mzuri wa hasira umekuwa hauonekani kabisa, kitu ambacho kinawafanya wengi kushindwa kuitumia hasira vizuri.

Kama ambavyo watu wamejifunza kuutumia moto vizuri, licha ya hatari na hasara zake, ndivyo pia wanavyopaswa kujifunza kutumia hasira vizuri ili kupata mafanikio makubwa. Na hilo ndiyo tunalokwenda kujifunza kupitia barua hii.

2. Hasira Inakusukuma Kufanya Makubwa Na Kuendelea Bila Kuacha.

Sisi binadamu tuna tabia moja ya kisaikolojia. Tukiwa tunataka kitu, tunaweza kukifanya au tusikifanye, msukumo wa kitu hicho hauwi mkubwa sana kwetu. Lakini tukiwa tunataka kitu, halafu wengine wakatuzuia au kutukwamisha kupata kitu hicho, huwa tunapatwa na hasira, ambayo inatusukuma kutaka kitu hicho zaidi. Kwa hasira hizo, tunakuwa na msukumo mkubwa wa kufanya mpaka tupate matokeo.

Kama ambavyo tumeona kwenye utangulizi, hisia hasi huwa zina nguvu ya kutusukuma zaidi kuliko hisia chanya. Tamaa ya kutaka kupata kitu fulani inaweza kutusukuma kuchukua hatua. Lakini hasira tunayokuwa nayo, inayotokana na kukosa kitu hicho, inatusukuma zaidi kwenye kuchukua hatua.

Pamoja na malengo na maono makubwa tuliyonayo, tunahitaji kuwa na hasira itakayotusukuma kuchukua hatua bila kuacha. Hasira ndiyo inatusukuma kuchukua hatua, kwa sababu ya kile ambacho hatutaki kitokee.

Na hasira tunayochagua inapaswa kuwa haina mwisho, ili tusifike hatua ya kuridhika na kile tunachokuwa tumepata. Tunahitaji kuwa na hasira ambayo haiwezi kutulizwa na kitu chochote isipokuwa ufanyaji endelevu wa kile tulichochagua.

Tumekuwa tunaona jinsi ambavyo watu wengi wanaoanzia chini wanajituma sana na kufanikiwa. Lakini wanapoanza kupata mafanikio madogo, wanaacha kuwa na msukumo waliokuwa nao na hilo linawakwamisha kuendelea kupata mafanikio makubwa zaidi.

Hapo kinachokuwa kimewakwamisha zaidi ni kukosa hasira ya kuwasukuma, kwa sababu hasira walizoanza nazo zimeisha. Kama mtu alipata hasira kwa kukosa kitu fulani, anapokipata hasira hiyo inaisha na msukumo unaishia hapo.

Ni muhimu sana kila tunapopiga hatua, tuhakikishe tunaendelea kuchochea hasira ambazo zimekuwa zinatusukuma. Na tuendelee kukumbuka hasira ni kama moto, tunapaswa kuzidhibiti vizuri ili zilete matokeo na kuepuka hasara zinazotokana na hasira hizo.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK120; Hasira; Dawa Na Sumu Inayoathiri Mafanikio Yako Kwa Kiasi Kikubwa