Rafiki yangu mpendwa,
Napenda kuchukua nafasi hii kukupa shukrani za dhati kutoka ndani ya moyo wangu.

Kwa siku 31 zilizopita nilikuwa nakupa taarifa za SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2021, yale muhimu utakayoyapata na kwa nini hupaswi kuyakosa.

Nilikusisitiza sana kwa sababu naamini nguvu ya tukio hilo katika kukusukuma kwenda mbele zaidi. Nilichojifunza miaka ya nyuma, kila anayekuwa na wasiwasi wa kushiriki, anaposhiriki huwa anashukuru kwa kufanya maamuzi hayo.

Hivyo huwa sipendi sababu yoyote imzuie mtu yeyote kushiriki semina hizi. Lakini kwa sababu haya ni maisha na huwa yana changamoto mbalimbali, kuna wanaokuwa wanatamani sana kushiriki semina na wapo tayari wanakwamishwa kwa sababu mbalimbali.

Nichukue nafasi hii kuwashukuru wale wote waliochukua nafasi ya kushiriki SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2021, mmenipa kazi kubwa ya kuhakikisha mwaka unaokuja wa mafanikio unakuwa na tofauti kubwa kwenye maisha yetu. Hilo nitalifanyia kazi bila sababu yoyote.

Niwashukuru pia wale ambao mlitamani sana kushiriki semina hii lakini kwa sababu mbalimbali mkashindwa. Kuna ambao mko nje ya nchi, wengine mtakuwa safarini kwenye tarehe hizo na wengine majukumu mbalimbali yamewatinga.

Niwakaribishe sana kwenye semina nyingine zijazo, muanze maandalizi mapema ili tuweze kuwa pamoja kwenye semina hizo.

Lakini pia sitawaacha hivi hivi, hivyo kama ulitamani sana kushiriki semina ili unufaike na yale niliyokuwa naahidi, usiumie na kuona umeyakosa. Bado zipo njia nyingine za kunufaika na hayo.

Kusudi la maisha yangu ni kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi kupitia kazi ninazozifanya. Na falsafa ninayoisimamia ni naweza kupata chochote ninachotaka kama nitawawezesha wengi zaidi kupata wanachotaka.

Hivyo bado ni wajibu wangu kuhakikisha maisha yako yanakuwa bora zaidi, iwe umeshiriki semina au la. Lakini pia nataka upate unachotaka ili na mimi nipate ninachotaka.

Lengo kubwa ambalo nimejiwekea kwenye mwaka wa mafanikio 2021/2022 ambao unaanza wiki ya kwanza ya mwezi novemba 2021 na kumalizika wiki ya mwisho ya mwezi oktoba 2022 ni kufanya kazi kwa karibu kabisa na watu 100.

Watu 100 ambao nitajua kwa kina mpango wao na kile wanachofanya, maono yao makubwa, malengo ya muongo na malengo ya mwaka wanayofanyia kazi. Kisha kwa mwaka mzima nawafuatilia kwa karibu na kuwapa nafasi ya ushirikiano mkubwa kwenye kile ambacho wanafanyia kazi.

Kuna nafasi chache katika hizo 100 zitakazobaki kwenye washiriki wa semina. Hivyo nitachagua wachache wa kujaza nafasi hizo ili idadi hiyo itimie na niweze kufanyia kazi lengo hilo.

Hivyo kuna nafasi yako hapa kama kweli umejitoa na uko tayari kujituma ili kufanya makubwa.
Kesho nitashirikisha fomu maalumu ya kujaza taarifa zako, kisha nitazipitia na kama utakidhi vigezo na nafasi kuwepo basi utaipata na nitakupa maelezo zaidi.

Nimalize kwa kuendelea kukushukuru kwa muda wote ambao tumeendelea kuwa pamoja. Naamini kuna manufaa makubwa unayoyapata ndiyo maana bado uko hapa. Na hilo ndiyo lengo na wajibu wangu.

Karibu sana tuendelee kuwa pamoja, tuweze kufanya makubwa na kupata mafanikio tunayoyataka.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani.