2468; Kutokujibu pia ni jibu.

Kwenye maisha huwa tunakutana na watu wa aina mbalimbali.
Wapo ambao huwa wanasema au kufanya mambo ambayo yanatukwaza na tunasukumwa kuwajibu ili wajifunze.

Tunaona tusipowajibu sawasawa na walichofanya au kusema, watazoea vibaya au watajiona washindi.

Lakini wakati mwingine kutokujibu ndiyo jibu lenye nguvu kubwa mno.

Wapo watu wanaofanya vitu fulani kwa makusudi kabisa, ili kuibua hisia zako, useme au kufanya kitu ambacho kitaleta taharuki zaidi.
Usipoelewa hilo utajikuta kila wakati unajiingiza kwenye matatizo.

Wapo watu ambao wao wenyewe hawajiamini na hivyo wanapoona mwingine anajiamini wanamshambulia kwa namna mbalimbali. Lengo lao kufanya hivyo ni ili mtu awajibu na wajione nao wana thamani.

Kwa watu wa aina hiyo, unapowajibu ndiyo unawapa nafasi ya kuendelea na kitu hicho. Lakini unapochagua kuwapuuza, kuchukulia kama vile ni watu ambao hawapo kabisa kwenye maisha yako, unazidi kuwakosesha nguvu na kuzidi kujiona hawana thamani.

Kuna nyakati ambazo kutokujibu ndiyo jibu lenye nguvu zaidi. Zijue nyakati hizo na uzifanyie kazi ili upunguze migogoro isiyokuwa na tija.

Hatua ya kuchukua;
Pale unapojua mtu anafanya kitu kwa makusudi kabisa kwako ili ujibu na muwe na mgogoro, wewe usijibu. Usilishe hiyo njaa yake ya kutafuta umuhimu kwako. Mpuuze, mchukulie kama ni mtu ambaye hayupo kabisa kwenye maisha yako na hilo litamwadhibu mno kuliko jibu lolote unaloweza kumpa.

Tafakari;
Hakuna kitu kinachoumiza kama kupuuzwa. Kama kuna mtu anajaribu kufanya vitu ili kukuumiza, jibu zuri kumpa ni kumpuuza. Ataumia sana kwa yote anayofanya halafu wewe ukampuuza.

Kocha.