2521; Tofauti inaanzia kwenye kujali.

Watu wawili, wanaweza kuwa wanafanya kazi au biashara ya aina moja, mmoja akafanikiwa sana na mwingine akashindwa kabisa.

Watu wamekuwa wakitafuta sababu za tofauti hiyo, wakiona labda ni bahati, fursa, upendeleo na uwezo tofauti.
Yote hayo yanaweza kuchangia, ila kuna kimoja kikubwa ambacho huwa hakipewi uzito; kujali.

Matokeo yoyote ya tofauti yanayopatikana huwa yanaanzia kwenye kujali.
Yule anayejali zaidi kile anachofanya, ndiye atakayekwenda hatua za ziada kwenye kufanya kitu hicho.
Hatua hizo za ziada ndizo zinazotengeneza fursa, bahati, upendeleo na mengine.

Japokuwa mwanzo tofauti ya anayejali na asiyejali haionekani.
Na pia mwisho matokeo hayaonyeshi mchango wa kujali.
Hilo ndiyo limesababisha wengi wasione mchango wa kujali katika kufanikiwa.

Ni kujali ndiyo kunamfanya mtu awe tayari kufanya kitu kwa muda mrefu bila kuchoka. Hilo linamjengea ujuzi na uzoefu ambao unamwezesha kufanyia kazi fursa mbalimbali zinazojitokeza.

Ni kujali ndiyo kunamfanya mtu awe king’ang’anizi kwenye kile anachofanya hata kama anapingwa, kukosolewa na kukata tamaa. Wakati wengine wanaacha, yeye anaendelea na hivyo kujikuta akibaki bila ushindani na bahati nzuri kuangukia kwake.

Ni rahisi kuona matokeo ya nje na kuyapa sababu mbalimbali za kutokea, lakini kujali ndiyo msingi mkuu wa yote.

Hatua ya kuchukua;
Ni kitu gani unajali sana kwenye kazi au biashara unayofanya? Weka nguvu zako kubwa hapo na utatengeneza fursa na kupata bahati zitakazokuwezesha kupiga hatua kubwa.

Tafakari;
Kama hujali kuhusu kitu ni vigumu sana kupata mafanikio makubwa kwenye kitu hicho. Kujali ndiyo tofauti kuu ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa.

Kocha.