2672; Una matokeo yapi ya kuonyesha?
Kila mmoja wetu ana mambo mengi sana ambayo amewahi kuyafanya kwenye maisha yake.
Fursa mbalimbali ambazo amekimbizana nazo akiamini hizo ndiyo zitampa kila kitu.
Lakini kabla hata fursa moja haijalipa, au pale anapokutana na changamoto, haraka sana anakimbilia kwenye fursa nyingine.
Hiyo ndiyo imekuwa tabia ya wengi na kupelekea washindwe kupata matokeo makubwa wanayoyataka.
Huwezi kufanya makubwa kwenye maisha yako kwa kuhangaika na mambo mengi.
Ni lazima uweke juhudi zako kwenye mambo machache na kwa muda mrefu ndiyo uweze kupata matokeo mazuri.
Kama unabisha kwenye hili, jiangalie tu wewe mwenyewe. Ni mambo mengi kiasi gani umewahi kuhangaika nayo kwenye maisha yako na yamekufikisha wapi?
Ni wakati sasa wa kuacha kuhangaika na hayo mengi, kuweka juhudi zako kwenye machache na kupata matokeo bora.
Hatua ya kuchukua;
Leo kaa chini na ujitathmini fursa zote ambazo umewahi kukimbizana nazo kwenye maisha yako.
Fursa ambazo wakati huo uliona siyo za kukosa na ndiyo zitakazokutoa kabisa.
Je zimekufikisha wapi?
Majibu unayoyapata yanapaswa kukupa somo kubwa, kwamba kinachokunufaisha siyo kuhangaika na fursa nyingi, bali kutulia kwenye fursa moja kwa muda mrefu.
Tafakari;
Kadiri unavyohangaika na fursa nyingi ndivyo unavyojichelewesha kupata mafanikio makubwa.
Maana kila fursa mpya unayoiendea, inapunguza nguvu zako kwenye fursa uliyokuwa unafanyia kazi kabla.
Komaa na kitu kimoja mpaka kilete matokeo mazuri kabla ya kuhangaika na vitu vingine.
Usione unapitwa au kupoteza muda.
Muhimu ni upate kile unachotaka.
Kocha.
Asante Sana kocha utulivu na umakini ni kwa kile tunachoanzisha na kufanya.
LikeLike
Kabisa
LikeLike