2714; Nguvu ni ile ile.
Watu huwa wanadhani kuna wakati wanaweza kuwa na nguvu nyingi zimazowawezesha kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.
Hilo ndilo huwa linawapa wengi tamaa ya kutaka kuanza au kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.
Matokeo yake ni vingi ambavyo mtu anajaribu vinaishia njiani au kushindwa.
Ukweli ni kwamba nguvu ambazo mtu unazo ni zile zile.
Unaposhawishika kufanyia kazi fursa mpya, jua hakuna nguvu mpya za ziada ambayo mwili wako utatengeneza.
Badala yake ni nguvu zile zile unazidi kuzitawanya zaidi.
Na changamoto kubwa kuhusu nguvu za miili yetu ni kwamba pale zinapotawanywa kwenye mambo mengi zaidi, ndivyo zinavyokuwa dhaifu zaidi.
Ni sawa na chai ambayo tayari ina kiwango fulani cha sukari, unapoongeza maji zaidi kwenye chai hiyo, unapunguza makali ya sukari hiyo.
Au chumvi kwenye mboga, ukiongeza maji zaidi unapoteza ladha yake.
Hatua ya kuchukua;
Chagua jambo moja au machache ambayo ndipo utaweka nguvu zako zote ili uweze kufanya makubwa kuliko ulivyozoea.
Na kila unapopata wazo jingine bora zaidi ya yale unayofanyia kazi, kabla hujapeleka nguvu zako huko tumia mfano wa sukari kwenye chai.
Ona ukiongeza maji zaidi kwenye chai huku sukari ikiwa imebaki kiasi kile kile.
Ukweli ni chai haitakuwa na utamu tena.
Tafakari;
Hatushindwi kufanya makubwa siyo kwa kuwa hatuna nguvu za kutosha, bali kwa sababu tunatawanya sana nguvu zetu kiasi kwamba zinaishia kutokuwa na madhara yoyote yale kwenye yale ambayo mtu unayafanya.
Epuka sana kutawanya nguvu zako, hicho ni kitu kinachoathiri sana ufanisi na uzalishaji.
#Let’sBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining