2745; Atatenganishwa na fedha zake.

Mteja yeyote yule, huwa anakutana na watu wa mauzo ambao hufanikiwa kumtenganisha na fedha zake.

Mteja akiwa na fedha, kuna namna ambavyo atashawishika na watu wa mauzo na kununua vitu ambavyo hata hakuwa na uhitaji navyo.

Ndiyo maana wengi wakiwa hawana fedha wanakuwa na mawazo mazuri, lakini wakishakuwa nazo mawazo hayo mazuri yanayeyuka na kujikuta wanafanya vitu ambavyo hawakupanga.

Hili ni jambo muhimu sana la kujua na kuzingatia kwani litakuwezesha kuwasaidia wateja wako.

Kuna wakati unaweza kuona kama kutokumshawishi mteja anunue kwako ni kumsaidia, kwa sababu ataokoa na kutunza fedha zake.
Lakini hilo siyo kweli, unapomwacha mteja na fedha, unamweka kwenye hatari ya kulaghaiwa na wale wanaotaka tu kupata fedha hizo bila kujali maslahi ya mteja.

Sasa kipi bora?
Wewe ambaye unajali maslahi ya mteja ndiyo umtenganishe na fedha zake, huku ukimwacha na manufaa.
Au wasiojali maslahi ya mteja ndiyo wamtenganishe na fedha zake huku wakimwacha na maumivu?

Kama una kitu sahihi, chenye manufaa kwa wateja wako basi ni wajibu wako kuhakikisha wateja hao wanakipata.
Wanaweza kuwa wabishi sana, lakini unapaswa kuhakikisha wameelewa manufaa wanayokwenda kupata ili wachukue hatua.

Jua kabisa kwamba kama utashindwa kumshawishi mteja anunue kwako hujamsaidia, bali umemwacha kwenye hali ya hatari ya kushambuliwa na wenye tamaa ya kupata fedha zake bila ya kujali maslahi yake.

Hatua ya kuchukua;
Pale unapokutana na mteja mwenye uhitaji wa kile unachouza na kina maslahi makubwa kwake, hakikisha kwa namna yoyote ile mteja huyo anakielewa na kukubali kukinunua. Hiyo ndiyo njia pekee ya wewe kumsaidia mteja huyo asiangukie kwenye mikono ya wasio na nia njema.

Tafakari;
Fedha yoyote aliyonayo mteja itaishia kwenye mikono ya watu wengine. Kama hutaipata fedha hiyo wewe, kuna wengine ambao wataipata.
Changamoto ni siyo wote wapo tayari kuyaweka maslahi ya mteja mbele. Wengi wanaangalia zaidi nini wao wanapata.
Kuwauzia wateja wako ni wajibu wako kabisa, kwani unawaokoa wasianguke kwenye mikono ya wasiojali.

#LetsBuildBusinesses
#NothingElseMatters
#BillionairesInTraining
#WeAllGonnaMakeIt
#WorkHardAndYouWillSucceed