2958; Abiria ambao hawaendi Arusha washuke.

Rafiki yangu mpendwa,
Pata picha wewe ni dereva wa basi ambalo linafanya safari zake kutoka Dar kwenda Arusha.

Basi imepaki kwenye stendi kuu ya mabasi ya Dar na kupakia abiria.
Basi inajaa kisha unaanza safari.

Ile unatoka tu kwenye stendi na kuelekea kibaha, kundi la abiria wanaanza kupiga kelele basi linaenda wapi.
Wanaeleza kwamba wao wanaenda Mtwara, kwa huo uelekeo wako siyo sahihi.

Unashangazwa ni kwa namna gani abiria hao wa Mtwara wamekuwa ndani ya basi la Arusha.
Kunakuwa na mvutano, hawataki kushuka kwa sababu hawataki kusumbuka tena kupata basi nyingine.
Wanachotaka ni basi igeuke na kuelekea upande wa Mtwara.

Unafanya kila namna kuwashawishi washuke, unawapa mpaka fidia. Baada ya mzozano mrefu, wanakubali kuchukua fidia na kushuka.

Unaona ahueni na safari inaendelea, japo sasa kwa kuchelewa.
Unaendesha mpaka Chalinze.
Ile unakatisha kona kwenda uelekeo wa Tanga, kundi jingine la abiria wanaanza kupiga kelele gari inaelekea wapi?
Abiria hao wanasema wanaelekea Mbeya hivyo basi inapaswa kuwa na uelekeo wa Morogoro.

Mnaanza upya majadiliano na abiria hao, ambao hawataki kusikia habari nyingine zaidi ya basi kwenda uelekeo sahihi.
Unawashawishi washuke, kitu ambacho hawapo tayari maana wanasema itawawia vigumu kupata basi.
Inakubidi uingie wajibu wa kuwatafutia basi ndiyo wakakubali kushuka.

Mpaka hatua hiyo, kama ni dereva makini itakubidi utoe tangazo kwa abiria wote.
Kwamba kama kuna abiria ambao hawaendi Arusha wanapaswa kushuka kwenye basi hilo.

Abiria hao wameingiaje kwenye basi hilo siyo kitu cha kusumbuka nacho sana katika hatua hiyo.
Maumivu makubwa ni safari inachelewa kutokana na kuwa na abiria wasio sahihi ndani ya basi.

Japokuwa wewe siyo dereva wa basi, ni dereva wa maisha yako, kazi na hata biashara yako.
Una abiria wengi kwenye kila basi lako na wengi ambao hawaendi unakoenda.

Tukiangalia basi la biashara yako ambalo wewe ndiye dereva, kuna abiria wa aina mbalimbali.
Kuna abiria ambao ni wafanyakazi, wengine wateja, wapo wasambazaji na washirika mbalimbali.

Katika watu hao, kuna ambao wana maono kama uliyonayo na mna uelekeo unaofanana. Hawa mnaendana vizuri.
Lakini kuna ambao mnatofautiana maono na hata mwelekeo.
Hawa mnakuwa na misuguano mingi inayochelewesha safari.

Unapaswa kufanya maamuzi sahihi kwa kuwaondoa abiria wote wasio sahihi kwenye basi lako.
Kwa wateja ni kuachana na wateja wote wasio sahihi kwa biashara yako.
Kwa wafanyakazi ni wale ambao hawakidhi vigezo vilivyopo.
Kadhalika kwenye maeneo mengine, wale ambao uelekeo wao ni tofauti na wa biashara, wanapaswa kuondolewa.

Ni zoezi gumu kufanya na wakati mwingine linapunguza kipato chako.
Lakini kwa muda na nguvu unazopoteza kuhangaika na abiria hao wasio sahihi, maamuzi ya kuwashusha yanakuwa bora zaidi.

Anza kwa kuwashusha abiria wasio sahihi, ambao uelekeo wao ni tofauti na wako.
Halafu kazana kupakia abiria walio sahihi, kwa kueleza wazi basi yako inaelekea wapi na watu wa aina gani unahitaji.

Bila ya kuwa na msimamo huu, hakuna hatua kubwa utakayoweza kupiga.
Uelekeo wa safari mmoja, abiria unaohitaji ni wale wenye uelekeo huo.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe