2959; Kisima kitupu.

Rafiki yangu mpendwa,
Kama una bomba la maji ambalo linatokea kwenye kisima, lakini halitoi maji, siyo kwamba maji hakuna kabisa, bali ni kisima ndiyo kitupu.
Kama kisima kingekuwa na maji, ni dhahiri bomba lingetoa maji.

Unaweza kulalamika hakuna wateja kwenye biashara yako, lakini huo siyo ukweli. Wateja wapo na wananunua, tatizo lako ni una wateja tarajiwa wachache unaowafuatilia.
Kama una wateja tarajiwa wawili tu unaowafuatilia na wote wakawa hawapo tayari kununua, utaona hakuna wateja.
Vipi kama utakuwa na wateja tarajiwa 100 ambao unawafuatilia? Kwa hakika kuna ambao watakuwa tayari kununua.
Kwa hiyo unajionea hapo, tatizo siyo maji (wateja), tatizo ni kisima (orodha ya wateja tarajiwa unaowafuatilia).
Kwa kuongeza idadi ya wateja tarajiwa unaowafuatilia, unaongeza nafasi ya kupata wateja zaidi.

Kadhalika kwa wafanyakazi unaowatafuta uwaajiri. Unapokosa wafanyakazi bora siyo kwa sababu hawapo, ila kwa sababu kuna wachache sana unaowafuatilia. Kama hao wachache wasipokuwa sahihi, unaishia kukosa wafanyakazi. Lakini kama ungekuwa na wengi ambao unawafuatilia, kati ya hao unakuwa na nafasi kubwa ya kupata walio bora.

Mara nyingi tunajikwamisha kwenye maisha kwa sababu ya namba ndogo tunayokuwa tunafanyia kazi. Namba hiyo ndogo inaposhindikana, tunakwama na kuona mambo hayawezekani.
Lakini kama tutakuwa na namba kubwa tunayofanyia kazi, uwezekano wa kupata tunachotaka unakuwa mkubwa zaidi.

Kwenye kila eneo la maisha yako, kuwa na namba kubwa unayoifanyia kazi. Hiyo ndiyo ndani yake utaweza kupata kile unachotaka.

Kama bomba halitoi maji, jaza kisima.
Kama utakuwa unajaza kisima kila wakati, bomba nalo litatoa maji kila wakati.
Unachohitaji ni mkakati sahihi wa kuhakikisha kila wakati maji yanaingia kwenye kisima, ili pia kila wakati maji yawe yanatoka bombani.

Kwa matokeo yoyote unayotaka kuyapata, weka juhudi za kutosha katika hatua zake za awali. Usitegemee matokeo ya mwisho kama juhudi za awali hujaweka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe