2984; Yai na kuku.

Rafiki yangu mpendwa,
Unakumbuka ubishani ambao tulipenda kuwa nao tulipokuwa watoto?
Kwamba kati ya yai na kuku kipi kilianza?

Ukisema yao ndiyo lilianza, swali linakuwa yai hilo lilitoka wapi kama siyo kutagwa na kuku?
Na ukisema kuku ndiye alianza, swali linakuwa kuku huyo alitoka wapi bila ya yai?

Ni ubishi fulani unaoweza kuonekana wa kijinga na kitoto, lakini unaelezea vyema mkwamo ambao tunakuwa nao mara nyingi kwenye maisha yetu.
Mkwamo ambao tusipoamua kuchukua hatua fulani, tunabaki tukiwa tumekwama kwa muda mrefu.

Tuchukue mfano mzuri wa mkwamo ambao watu wengi wamekuwa nao kwenye biashara, hasa kwenye mauzo.

Ili uweze kukuza mauzo kwenye biashara, unahitaji kuwa na timu.
Lakini wengi wanashindwa kuwa na timu, kwa sababu hawawezi kuilipa.
Na ili uweze kuilipa timu, lazima uwe na mauzo makubwa.

Unauona mkwamo hapo, unajiambia sababu ya kutokuwa na timu ni kutokuweza kuilipa.
Lakini pia unahitaji kuwa na timu ili uweze kufanya mauzo makubwa na kuweza kuilipa timu.

Usipochukua hatua mahali, unaishia kubaki na biashara ambayo imekwama kwenye maeneo yote mawili.
Inakuwa haina timu kwa sababu huwezi kumudu kuilipa.
Na wakati huo huo inakuwa haina mauzo makubwa kwa sababu haina timu.

Kuvunja hilo unapaswa kuanza na timu kama uwekezaji kwenye biashara.
Kuwekeza malipo ya awali kwa timu hiyo wakati bado biashara haiwezi kumudu.
Kisha kuongoza, kusimamia na kufuatilia timu hiyo vizuri ili iweze kukuza mauzo na iweze kumudu kujilipa yenyewe.

Usijikwamishe kwa ubishani usiokuwa na mwisho, chagua sasa kuingilia mahali, ambapo rahisi ni kuwekeza kwenye timu.

Unaweza kuwa unajiuliza kwa nini kwanza usikuze mauzo kabla ya kuwa na timu ili timu ikifika iweze kujilipa na kuendelea kukuza mauzo.
Jibu ni kuna ukomo utakaofikia kwenye kukuza mauzo kama hutakuwa na timu.
Hivyo kwa vyovyote vile, ni muhimu ujenge timu, ambayo ukiiwekea kazi vizuri, lazima iweze kujilipa.

Chukua mfano tayari biashara yako ina wateja 100 ambao wamewahi kununua katika kipindi chochote kile.
Je ni wangapi ambao huwa wanatudi kununua mara kwa mara?
Na je wangapi ambao wamewahi kukuletea wateja wengine zaidi?

Kwa wateja hao 100 tu waliopo, bado unaweza kuuza zaidi na kupata wateja wengi zaidi.
Lakini hilo litahitaji uwafanyie hao kazi kubwa, uwape huduma nzuri, uwafuatilie kwa karibu na kuwajua kiundani.
Peke yako hutaliweza hilo na hivyo unajikuta ukipoteza fursa nyingi za kuuza zaidi kama huna timu ya uhakika.

Mkwamo wowote ule unaojikuta umeingia kibiashara jiulize ni uwekezaji gani unapaswa kufanya ili kuweza kuondoka kwenye mkwamo huo.
Kwa sababu bila uwekezaji, wa muda, fedha na ujuzi, mengi sana yanakwama kibiashara.

Usiseme kipi biashara inaweza na kipi haiwezi, biashara inaweza kila kitu iwapo uwekezaji sahihi utapatikana.
Piga hesabu zako vizuri kwa kila uwekezaji utakaofanya ni marejesho gani unayotegemea.
Kisha fanya uwekezaji huo na fuatilia kwa karibu uyapate marejesho unayoyataka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe