2993; Ukiondoka, siyo kwa sababu hizi mbili.
Rafiki yangu mpendwa,
Tangu nimeanza huduma hii ya ukocha, kuna watu wengi sana ambao wameshapita na kuondoka.
Wapo ambao niliwaondoa mimi mwenyewe na wapo ambao waliondoka wao wenyewe.
Niliowaondoa sababu kuu ni moja tu, kushindwa kukaa kwenye mchakato ambao tumekubaliana, licha ya kuelekezwa kwa kila namna. Pamoja na kupewa kila fursa ya kujirekebisha, bado walishindwa kufanya hivyo.
Kwa walioondoka wao wenyewe wana sababu zao binafsi, wapo walioahidi wanakaa pembeni kwa muda halafu watarudi na wengine walieleza wametosheka na yale waliyojifunza. Na pia wapo walioeleza hawataki tena kujitesa na mchakato tulionao.
Katika hii safari ya mafanikio makubwa tuliyonayo, mabadiliko ya watu yataendelea.
Wapo ambao nitaendelea kuwaondoa na sababu pekee ya kuwaondoa itaendelea kuwa kutokukaa kwenye mchakato kamili wa safari hii.
Halafu wapo wale watakaoamua kuondoka wenyewe, kwa sababu zao mbalimbali.
Kuna sababu nyingi za watu kuondoka ambazo siwezi kuzizuia, lakini kitu kimoja ambacho nimejiwekea ni hakuna atakayeondoka kwa sababu kubwa mbili.
Sababu ya kwanza ni kunishinda kwenye ufanyaji wa kazi. Moja ya sababu zinazoweza kuwafanya watu kuachana na kocha wao ni pale wanapomzidi kwenye ufanyaji wa kazi, yaani wanakuwa wanafanya kazi kuliko kocha wao.
Hilo sitaliruhusu kwangu, nitahakikisha kila wakati ninafanya kazi kuliko wote ambao wapo kwenye huduma yangu.
Yaani hata ujisukume kufanya kazi kwa juhudi kiasi gani, bado nitahakikisha ukiniangalia unaona bado hujanifikia kwenye ufanyaji wa kazi.
Ahadi niliyojiwekea ni mara zote nitaweka juhudi kubwa kwenye kazi kuliko wengine wote.
Na hili siyo tu kushindana nani anaweza kufanya kazi sana, bali kuhakikisha kila unaponiangalia unaona bado hujafanya vya kutosha.
Hilo litakusukuma ufanye zaidi na zaidi na hivyo uone bado hujafika mwisho wa kupiga hatua zaidi.
Ninachojua ni nikizembea kwenye kazi, utaona hakuna tena jipya na hivyo kuwa na sababu ya msingi ya kuondoka.
Hivyo kwenye huu ufanyaji wangu wa kazi bado sijafika mwisho na wala sitafika mwisho, kila mara nitahakikisha nafanya zaidi ya wengine wote.
Kwa kifupi kwa upande wa ufanyaji kazi, bado sijafanya, hivyo kama umekuwa unashangaa nafanyaje yote, bado utahitaji kukaa hapa ushangae zaidi, maana mchezo ndiyo kwanza unaanza.
Sababu ya pili ni kunishinda kwenye kujifunza. Sababu nyingine kubwa inayowafanya watu kuachana na makocha wao ni pale wanapoona hawana tena cha kujifunza kutoka kwa makocha wao.
Hicho ni kitu ambacho kamwe sitakuja kukiruhusu kwangu.
Ahadi nyingine niliyojiwekea ni kuwashinda wengine wote kwenye kujifunza.
Hivyo haijalishi unajifunza kiasi gani, bado nitaendelea kujifunza kuliko wewe.
Haijalishi unajua kiasi gani, bado ukija kwangu nitahakikisha una vitu vya kujifunza.
Pamoja na mengi ambayo nimeshajifunza, bado nitaendelea kujifunza zaidi na zaidi.
Kama umekuwa unashangaa najifunzaje yote hayo, bado hujaona kitu, nitahakikisha kila ukija kwangu kuna kitu unajifunza.
Nitaendelea kuhakikisha hata kama ni maongezi ya kawaida tu tunafanya, unaondoka na mambo ya maana ya kwenda kufanyia kazi na ukanufaika.
Kwa namna hiyo, utaendelea kuwa hapa kama bado unataka kujifunza na kuwa bora.
Sikuelezi haya kukushawishi ubaki au kukuzuia usiondoke.
Nayaeleza haya hapa kwa sababu kubwa mbili.
Moja ni kuweka kumbukumbu sawa, ili kila mmoja aelewe yupo hapa kwa sababu gani. Na kubwa ni hizo mbili, kujifunza na kuchukua hatua, yaani kuweka kazi hasa.
Mbili ni kuendelea kukupa msukumo wa kujifunza na kuweka kazi, kwa kukuhakikishia kwamba kama tayari unao msukumo wa ndani, basi umepata mahali sahihi wa kujipima.
Siku moja nilikuwa na maongezi na mkurugenzi mkuu wa kampuni moja kubwa yenye matawi kwenye nchi zaidi ya 8, Afrika na Uarabuni.
Katika mazungumzo yetu, sijui tulifikaje kwenye ufanyaji wa kazi, nikamwambia kwa kujivunia kwamba mimi siku yangu huwa inaanza saa tisa usiku kila siku. Nikamuuliza wewe umeanza siku yako saa ngapi? Akanijibu sijalala kabisa. Ah, kwa kweli nilipata msukumo mkubwa zaidi.
Japo sitakuwa na kesha kwa muda mrefu kama yeye, lakini nitahakikisha kwenye kila muda ninaoweka kwenye kazi, naweka kazi ya maana hasa.
Kwenye eneo la kujifunza, huwa naona najifunza kwa kasi kubwa. Kwa usomaji wa vitabu kwa muda mrefu nilikuwa nasoma vitabu 2 kwa wiki, baadaye nikaona wengi ninaojifunza kwao wanasoma kitabu kimoja kwa siku. Nimefika kwenye kusoma kitabu kimoja kwa siku, nimekutana na mtu mwingine ninayependa kujifunza zaidi kwake, ambaye anaitwa Tyler Cowen, ambaye anasoma zaidi ya vitabu vitano kwa siku.
Kadhalika kwenye usikilizaji wa vitabu, nimekuwa msikilizaji wa vitabu vilivyosomwa (Audio Books) kwa miaka mingi. Na kipindi chote nimekuwa nasikiliza kwa kasi ya kawaida. Nikaona kuna watu wanasikiliza kwa kasi mara mbili, nikaanza kufanya hivyo, japo mwanzo ilinitaka niongeze zaidi umakini.
Nilichokuja kushangaa ni kuna watu wanasikiliza vitabu kwa kasi mara 3 zaidi ya kawaida. Kwa kweli hilo lilinivutia sana, nikaona kumbe hata kama naona nafanya kwa juu kiasi gani, kuna ambao wanafanya kwa juu zaidi.
Ahadi yangu kwenye maisha imekuwa hii, nitawaruhusu watu wanizidi kwenye kila kitu isipokuwa vitu viwili; kazi na kujifunza.
Mara zote nitahakikisha nafanya kazi kuliko wengine wote na pia ninajifunza kuliko wengine.
Na ndiyo maana muda wangu wote ambao sijalala (ambao ni masaa 18 kwa siku), nakuwa nafanya kazi au najifunza, hakuna kingine nje ya hapo.
Na ushauri wangu mkubwa kwako ni waruhusu watu wakuzidi kwenye mambo mengine yote isipokuwa hayo mawili; kazi na kujifunza. Fanya kazi kwa juhudi kubwa kuliko wote na pia jifunze zaidi ya wengine wote.
Hilo lianzie kwenye timu yako na kwenda kwa washindani wako.
Litakupa fursa ya kufika kwenye mafanikio makubwa na kudumu hapo kwa muda mrefu.
Nimalizie kwa kukukumbusha kwamba haijalishi utafanya kazi kwa juhudi kiasi gani na kujifunza kwa wingi kiasi gani, kila mara utaniona niko mbele yako.
Na pale utakapokuwa mbele yangu kwenye hayo mawili, itabidi majukumu yabadilike na mimi ndiye nije kujifunza kutoka kwako.
Itabidi ujiue ili hilo litokee, nakuahidi hivyo.
Tuendelee na mapambano, mambo bado kabisa.
Na hii izidi kuchochea moto ndani yako, utakaokufanya ufanye zaidi.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe
Nitahakikisha tuko pamoja katika safari hii ngumu ya Mafanikio
LikeLike
Asante na karibu sana Hassan.
LikeLike
Nitaendelea kujifunza na kufanya kazi zaidi ya wengine.
LikeLike
Vizuri sana.
LikeLike
Ahsante sana kocha
LikeLike
Karibu
LikeLike
Aisee, hiyo ni challenge nzito kweli kweli.
Ngoja tupambane.
LikeLike
Tunahitaji kupambana sana, hii ngoma haijawahi kuwa rahisi. Lakini uzuri ni inawezekana.
LikeLike
Asante kocha ninakwenda Kuweka kazi zaidi na Kujifunza zaidi
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Kazi na Kujifunza. Kubali watu wakuzidi kila kitu lakini sio kazi na Kujifunza
LikeLike
Hakika.
LikeLike
Kaz, Kaz ,kaz na kijifunza
LikeLike
Safi.
LikeLike
KUJIFUNZA!!! KAZI!!!
LikeLike
Hayo tu.
LikeLike
hongera kwa kuweza kusoma kitabu kimoja kwa siku. ni kweli safari bado, tupokee changamoto zetu kama zawadi
AHSANTE
LikeLike
Asante na karibu sana Selemani
LikeLike
Sitarudi nyuma sitaacha na ntahakikisha kama nipo mzima basi nipo nawewe kocha Makrita katika safari yako. Hata hivyo wewe una Ndoto ya kuwa Rais wa Tanzania ila mimi nina ndoto ya kuwa bilionea na Mshauri wa Rais wa Kuanzia mwaka 2035. Hivyo mambo hayo mawili kwangu hayatapita kamwe.
LikeLike
Asante na karibu sana Patson
LikeLike
Kuweka kazi na kujifunza ndio mpango mzima kwenye maisha
Asante
LikeLike
Hayo ndiyo muhimu zaidi.
LikeLike
Hakika umeendelea kuwa kocha Bora kwangu!
LikeLike
Asante na karibu sana Fabian
LikeLike
Hakika wewe ni kocha Bora kwangu!
LikeLike
Kazi na kujifunza.Nitawaruhusu watu wanishinde kwenye kila kitu isipokuwa kwenye mambo haya mawili kazi na kujifunza.
LikeLike
Safi sana.
LikeLike
Nitaongeza bidii katika kujifunza na kazi.
LikeLike
Kila la kheri.
LikeLike
Natakiwa kufanya kazi kwa juhudi kubwa kuliko wote na pia nijifunze zaidi ya wengine wote.
Ahsante Kocha.
LikeLike
Hayo ndiyo ya msingi zaidi.
LikeLike
Kazi na Kujifunza. Kubali watu wakuzidi kila kitu lakini sio kazi na Kujifunza
LikeLike
Kabisa
LikeLike
Asante Sana kocha kwa makala Bora kabisa toka mwaka umeanza, nimejikuta ninasisimka mwili.
Makala imeamusha MSUKUMO mkubwa wa kuendelea kujifunza na kufanyia kazi kwa msimamo Yale tunayojifunza, Asante Sana.
LikeLike
Asante na karibu sana Miraji.
LikeLike
asante sana ,hii si mambo ya mchezo mchezo…vitabu 5 kwa siku .
LikeLike
Lazima damu zimwagike.
LikeLike
Hii hadithi ya mkurugenzi alie kwambia hajalala,mara ya kwanza nilipoisikiliza niliona alivyoamua kujitoa zaidi, na sasa hata wewe unaendelea kujitoa zaidi kwa ajili yetu,kwa nini na mimi nisijitoe kwa ajili yako ambayo Mimi ndiyo mnufaika zaidi
Ahadi yangu kwako nipo tayari kuendelea kuwmbatana na wewe ktk safari hii ngumu ya kusaka mafanikio.asante.
LikeLike
Asante na karibu sana Beatus.
LikeLike
Sitaruhusu mambo haya mawili katika biashara yangu na sehemu niliyoajiriwa.
Sitaruhusu wafanyakazi wangu wanizidi kwenye kazi kwani nitafanya mara 10 zaidi yao.
Sitaruhusu wafanyakazi wenzangu wanizidi katika kazi kwani nitafanya mara 10 zaidi yao.
Nakumbuka Kuna kipindi watu Wa usafi walidhani Huwa nalala ofisini maana mara nyingi waliniacha na hata wanapowahi kiasi Gani wananikuta nilishafika muda mrefu na kufanya kazi zangu nyingi…
Hakika tabia ya kuamka mapema ni msingi Bora Wa kufanya kazi.
LikeLike
Asante na karibu sana Rejoyce.
LikeLike
Maamuzi magumu, hatua Ngumu.
LikeLike
Ambavyo vinazalisha matokeo makubwa.
LikeLike
Naendelea kupambana
LikeLike
Mapambano hayana mwisho.
LikeLike
Umenitia hamasa nami kuendekea kupambana kuwa b
ora zaidi katika mambo hayo mawilili
LikeLike
Vizuri sana, kila la kheri.
LikeLike
Asante sana Kocha,naahidi kujifunza kila siku na kufanya kazi kwa ubora zaidi,sitaruhusu wengine wanishinde kwa hilo,kwa kweli unanipa hamasa sana maana siku hizi nikitaka kulala au kula nakumbuka nimesoma au nimeandika nini . Sipendi kuangusha Kocha wangu.
LikeLike
Safi sana, endelea na moto huo huo, usiruhusu upoe.
LikeLike