2998; Amini.

Rafiki yangu mpendwa,
Kujenga timu bora ya kuendesha biashara kunahitaji watu.
Na watu huwa wanapenda kumfuata mtu anayejua wapi anakwenda na ana amini atafika kule anakokwenda.

Ili uweze kuwavuta watu sahihi kuja kwako, lazima uwe kiongozi mzuri, ambaye unajua unakokwenda na unaamini utafika unakokwenda.
Watu wanataka uwe na imani isiyoyumba kuhusu kufika kule unakokwenda.

Imani huwa inaambukizwa, unapoamini kile unachoamini, bila ya kuyumbishwa, watu nao wanakuamini.
Wanachotaka watu siyo wao waamini kile unachoamini, bali waamini unaamini unachoamini.

Bila ya kuwa na imani ya kule unakokwenda, hakuna mtu anaweza kuwa na imani na wewe na kukufuata.
Hivyo hata kama huna uhakika, unapaswa kuwa na imani isiyoyumba, siyo kwa ajili yako, bali kwa ajili ya watu wako.

Na imani hiyo haipaswi kuwa ya kuigiza, bali imani thabiti, ambapo unakuwa tayari kujitoa kafara kwa kile unachoamini.
Ni kujitoa kwako kafara ndiko kunakowapa watu uhakika wa kukufuata wewe.

Kwenye safari yetu ya kuelekea kwenye ubilionea, imani yako inapaswa kuwa ya sehemu nne;
Moja ni kuamini kwenye kitu kikubwa nje yako, hapa ni kuamini kwenye mchakato wa kuelekea kwenye ubilionea. Amini sana kwenye mchakato huo na kuufuata bila kuyumba.
Mbili ni kuamini kwenye ndoto kubwa ulizonazo, amini utazifikia bila ya shaka yoyote.
Tatu ni kujiamini wewe mwenyewe kwamba utaweza kupata kile unachotaka, bila ya kuwa na wasiwasi wowote.
Na nne ni kuwaamini wale unaoambatana nao kwamba ni watu sahihi katika safari uliyopo.

Imani ina nguvu kubwa sana kwenye safari yoyote uliyopo.
Hiyo ni kwa sababu matatizo, vikwazo na changamoto huwa haviishi.
Pale mambo yanapokuwa magumu, watu humwangalia kiongozi.
Na hapo ndipo kiongozi anapopaswa kuwa na imani kali juu ya kile anachoendea.
Kiongozi hapaswi kuwa na wasiwasi au kuonekana kukata tamaa.

Kiongozi akionyesha wasiwasi au kukata tamaa anakuwa amefanya usaliti mkubwa kwa wafuasi wake.
Wafuasi wanakosa uhakika na kutafuta mahali pengine pa kwenda, ambapo panawapa uhakika zaidi.

Wajibu wako mkubwa kama kiongozi ni kuamini.
Na haijalishi kama una uhakika au la, unapaswa kuamini kwanza ili kuipa timu yako uhakika.
Mara kwa mara ieleze timu yako wapi mnakwenda na mtaweza kufikaje kule mnakokwenda.
Watie watu moyo kwamba pamoja na magumu na changamoto mnzopitia, ushindi ni uhakika.

Kazi yako kubwa ni kukaa kwenye mchakato na kuhakikisha watu wako wanakaa kwenye mchakato.
Na kwa sababu mchakato ni sahihi, ni swala la muda tu kabla matokeo mazuri hayajaonekana.

Amua kile unachotaka, ambacho hapa ni kuwa bilionea.
Amini kwenye mchakato wa kufika kwenye ubilionea na ufanyie kazi bila kuyumba.
Amini kwamba utafika kwenye ubilionea huo na wewe ni mtu sahihi kabisa.
Amini watu unaoambatana nao kwamba wanaweza na wasaidie kukaa kwenye mchakato.

Usiwe na shaka yoyote kwenye hayo unayoamini.
Hata kama ndani yako una wasiwasi wowote, usiuonyeshe nje.
Wewe simama kwenye imani yako na onyesha kuwa na uhakika mkubwa.
Hilo siyo kwa ajili yako, bali kwa ajili ya wale wanaokufuata.

Uzuri ni kwamba asili huwa inafanya mambo yake kwa namna ya ajabu kabisa.
Asili huwa inalipa mchakato, hivyo kwa kuamini na kukaa kwenye mchakato bila kuyumba, matokeo yanakuja, hata kama huna uhakika.
Kukaa kwenye mchakato kunaleta matokeo, utake usitake.
Ndiyo maana sehemu ya kwanza kuwa na imani nayo ni mchakato.
Hakikisha wewe na timu yako mnaamini na kukaa kwenye mchakato bila kuyumbishwa na chochote kile.

Maisha ni kuchagua na unapochagua unapaswa kuwa na imani kubwa kwenye kile unachochagua.
Bila ya imani, hakuna kingine kitakachowezekana kwenye safari yako.
Na kwenye hili swala la imani usijiangalie wewe peke yako, bali waangalie wale wanaokufuata, unaowahitaji zaidi ili kufika unakotaka kufika.
Wao kuambatana na wewe inategemea zaidi imani uliyonayo kwenye safari uliyopo.
Ikiwa huna imani au imani yako inayumbishwa, watakukimbia haraka sana.

Wape watu uhakika kupitia imani kali uliyonayo na wataambatana na wewe popote unapokwenda.
Imani inakupa wewe ujasiri na watu wanapenda kuwafuata wale ambao ni jasiri.
Usisubiri mpaka uwe na uhakika ndiyo uwe na imani.
Wewe anza na imani na uhakika utajitengeneza kadiri unavyokwenda.

Wakumbushe watu wako mara kwa mara kuhusu kule mnakokwenda na mchakato mzima wa kuwafikisha kule.
Wape uhakika wa kufika mnakokwenda kupitia mchakato uliopo.
Kisha kuwa mfano kwa kukaa kwenye mchakato.
Hilo litawapa watu imani kubwa ya kuendelea kukufuata na kukaa kwenye mchakato.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe