3011; Unaweza kufanya zaidi.

Rafiki yangu mpendwa,
Ukiwa ardhini na ukatazama angani, unaona anga au mawingu kama ndiyo ukomo.
Lakini ukipata njia ya kupanda juu zaidi, unagundua ukomo ulioona ukiwa chini siyo mwisho, bali unaweza kwenda zaidi na zaidi.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye mambo mengi ya maisha, ukomo unaokuwa unauona siyo halisi, unaweza kwenda zaidi ya ukomo huo.

Pale unapoona umefika mwisho wa ufanyaji, tambua kwamba unaweza kufanya zaidi.
Pale unapojiona umechoka kufanya kile unachofanya, bado unaweza kuendelea kufanya zaidi.

Asili huwa haina uhaba wala ukomo.
Ukomo wowote tunaouona ni wa kufikirika, yaani umeanzia kwenye fikra zetu wenyewe.

Hatua ya kwanza ya kuweza kufanya makubwa kwenye maisha yako ni kuamini bila ya shaka yoyote kwamba unaweza kufanya zaidi.
Haijalishi kwa sasa unafanya kwa kiasi gani, jua unaweza kufanya zaidi.
Haijalishi ni juu kiasi gani umeshafika, jua unaweza kwenda juu zaidi.
Pale unapokuwa umechoka na kuona umefika mwisho, jua hapo ndiyo kwanza unaanza.
Ukiwa tayari kwenda hatua ya ziada bila ya kukubaliana na ukomo wowote, utaweza kufanya makubwa.

Dunia imejengwa na wale waliokataa kukubaliana na ukomo unaowazuia wengi. Ni wale wanaokuwa na picha ya tofauti na kung’ang’ana nayo bila kukubali kushindwa ndiyo wanaoweza kufikia picha hiyo.

Ipo kauli maarufu inayosema; ‘Watu wa kawaida huwa wanaenda na dunia inavyoenda, watu wasio wa kawaida huwa wanailazimisha dunia iende vile wanavyotaka wao. Hivyo basi, maendeleo yote hapa duniani yanatokana na watu wasio wa kawaida.’

Usikubali kufuata mkumbo kwenye maisha, utajikwamisha kwa mengi sana unayotaka kufikia.

Jua kabisa ya mwamba;
Ndoto zozote kubwa ulizonazo zinawezekana.
Hatua zozote ambazo umeshapiga mpaka sasa unaweza kupiga
Na chochote ambacho umeshafanya, unaweza kufanya zaidi.
Kwa kifupi ni kwamba hakuna ukomo wala kikwazo chochote kinachoweza kukuzuia kupata kile unachotaka.

Ukomo pekee wenye nguvu ya kukuzuia wewe usipate matokeo unayotaka ni wa ndani yako mwenyewe na siyo nje.
Kama kuna vitu unataka kupata ila hujakipata mpaka sasa, jua ni wewe mwenyewe unajizuia.
Anza kwa kuvunja ukomo uliojiwekea mwenyewe ili uweze kufanya makubwa zaidi.
Haijalishi umefika ngazi gani, unaweza kufanya zaidi na kupiga hatua kubwa zaidi.

Chochote unachotaka kipo ndani ya uwezo wako kukipata.
Ni kuamini bila ya shaka yoyote kwamba unakipata,
Kisha kuchukua hatua stahiki ili kuweza kukipata.
Mara zote nenda hatua ya ziada ili uweze kupata kile unachotaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe