3016; Usiwe wa kawaida.

Rafiki yangu mpendwa,
Kwa chochote unachofanya kwenye maisha yako, usikubali kuwa mtu wa kawaida.
Watu wa kawaida huwa wanaweza kuonekana ni wema kwenye jamii, lakini huwa hawapati mafanikio makubwa.

Mafanikio makubwa huwa yanapatikana kwa kufanya mambo kwa utofauti na ukubwa kuliko ilivyozoeleka.
Mafanikio makubwa ni zao la kwenda kinyume na kundi kubwa la watu.
Wakati watu wengi wanafanya vitu kwa namna fulani, unapaswa kwenda kinyume nao ili kupata matokeo ya tofauti.

Kukataa kuwa kawaida ni rahisi kusema kuliko kufanya.
Inataka mtu uwe na uvumilivu mkubwa, kwa sababu kitendo cha kukataa kuwa kawaida unakuwa umeanzisha vita na kundi kubwa la watu wa kawaida.
Utashutumiwa kutokujali wengine, kutokuzalisha vilivyo sahihi na kuonekana unajisumbua.

Lakini hayo yote ndiyo yanachangia kupatikana kwa matokeo ya tofauti na makubwa zaidi.
Mafanikio makubwa kwenye maisha hayatokei kama ajali, bali yanatengenezwa.
Watu wanaoyapata mafanikio makubwa kwenye jamii ni wachache sana.
Kwa sababu hao ndiyo wanaokuwa na uthubutu wa kutosha kukataa kuwa wa kawaida.
Wakati wengi wakifuata kundi na kufanya kwa ukawaida, wanaofanikiwa sana wanakwenda wenyewe na kufanya kwa ukubwa na utofauti.

Kawaida ni nzuri kufanya, haina ugumu kufanya na wala haina hatari.
Kawaida inaleta uvivu na uzembe ambavyo ni vikwazo vikubwa kwa mtu kupiga hatua kubwa.
Kawaida ni adui mkubwa wa mafanikio makubwa kwenye maisha.

Kama hujui uanzie wapi kwenye kukataa kuwa kawaida, anza kwa kwenda kinyume na kundi kubwa la watu.
Angalia ni vitu gani ambavyo kundi kubwa la watu linafanya, kisha wewe nenda tofauti na wanavyoendana wao.
Ona picha ya tofauti kwenye fikra zako na chukua hatua kubwa, tofauti na kwa wingi zaidi ya wengine wanavyofanya.

Utaweza kupiga hatua kubwa sana kwenye maisha kama utakwenda kinyume na watu wengi wanavyoenda.
Watu wengi wanafuata mkumbo, wewe simama peke yako.
Watu wengi wanahangaika na mambo mengi, wewe weka mkazo kwenye mambo machache yaliyo muhimu zaidi.

Ona wasichoona wengine,
Fanya wasivyofanya wengine,
Weka mkazo mkubwa kwenye kila unachofanya.
Na jipe muda wa kutosha kupatikana kwa matokeo ya tofauti unayoyataka.
Matokeo bora kabisa yatapatikana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe