3046; Wapambanie kombe.

Rafiki yangu mpendwa,
Kadiri chochote kile unachofanya kinavyokuwa rahisi kupatikana, ndivyo wengine wanavyokidharau na kukipuuza.

Kama muda wako unapatikana kwa urahisi, watu watautumia hovyo kwa mambo yasiyokuwa na tija.
Watakuzamisha kwenye mambo ya hovyo, yanayokula muda wako na yasiyokuwa na tija yoyote kwenye yale unayofanya au unayotaka kufikia.

Kadhalika kadiri chochote unachouza kinavyokuwa rahisi kupatikana, yaani wateja unaowalenga wanaweza kukipata kwa wengine wengi na kwa urahisi, ndivyo wasivyokithamini kitu hicho.
Kwa kuwa wanajua wanaweza kukipata kwa wingi na urahisi muda wowote, hawasukumwi kwenda hatua ya ziada ili kukipata.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwa watu unaoshirikiana nao, hasa wafanyakazi unaowaajiri. Kadiri majukumu unayowapa yanavyokuwa rahisi, ndivyo wanavyoyafanya kwa mazoea na matokeo wanayozalishwa kuwa hafifu sana. Lakini majukumu unayowapa yanapokuwa yanawapa changamoto, ndivyo wanavyosukumwa kuwa bora na kuyafanya kwa viwango vya juu.

Kwa watu wote wanaohusika na wewe kwa namna yoyote ile, waweke kwenye hali ya kupambania kombe. Fanya kile wanachofanya kiwe na ugumu fulani ambao utawasukuma kwenda hatua ya ziada ili kuweza kukikamilisha kwa ubora wa hali ya juu.

Mara zote waweke watu kwenye hofu ya kupoteza kile wanachopata kwako, hilo linawafanya wakithamini na kukipambania.
Tamaa ya kupata pia ni njia yenye nguvu ya kuwasukuma watu kupambania kombe, lakini peke yake haina nguvu kama hofu ya kupoteza.

Msingi mkuu wa uchumi ni kanuni ya mahitaji (demand) na upatikanaji (supply). Kitu kinapokuwa na mahitaji makubwa na upatikanaji wake kuwa mdogo ndivyo kinavyokuwa na thamani kubwa zaidi.
Hii pia tunaweza kuichukua kama moja ya kanuni kuu za maisha.
Cheza vizuri karata zako za kuhitajika kwa kile unachotoa (demand) na upatikanaji wake (supply).
Hakikisha kwa namna yoyote ile, uhitaji ni mkubwa kuliko upatikanaji ulivyo.
Hilo linatosha kukuza sana thamani ya chochote ulichonacho na kujiweka kwenye nafasi ya kupata matokeo bora zaidi.

Hii dhana tuliyojifunza hapa inahitaji umakini na ujasiri wa hali ya juu katika kutekeleza.
Wengi huona kurahisisha mambo na kutoa kwa wingi ndiyo itawapa uhakika wa kuwapata wanaowalenga.
Ni kweli kwa kutokuweka vikwazo vyovyote utawapata walio wengi, lakini pia wengi wa hao utakaokuwa umewapata, hawatakuwa watu sahihi kwako.

Unapochukua hatua kwenye dhana hii ya kuwafanya watu wapambanie kombe, utaona kama unapoteza, hasa mwanzoni. Na hilo ni kweli kwa sababu kuna wengi ambao siyo sahihi ulikuwa nao.
Ni lazima uwaondoe hao kwanza ili kupata bafasi ya wale walio sahihi na bora.

Kwenye huu msimu wa HAPANA ambao tupo, sema hapana kwa yote yaliyo chini ya viwango unavyokuwa umejiwekea.
Usihofie kukosa unachotaka kupata, changa vizuri karata zako za mahitaji na upatikanaji ili kuwapa watu msukumo wa kuweka juhudi ili wapate yale unayoyatoa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe