Kuishi maisha ya wengine ndiyo chanzo cha wengi kuwa na maisha magumu. Angalia hata maisha yako binafsi, ukiishi kwa mahitaji yako ya msingi na ukiishi maisha yako wala hutajikuta unaumia.
Ili tuweze kuishi maisha yetu, falsafa ya ustoa inatusisitiza sana tujitambue sisi wenyewe ili tusisumbuke na mambo yasiyo sahihi kwetu.
Kwa nini? Kwa sababu kuna mambo wengine wanaweza kufanya na wakafanikiwa vizuri tu, ila wengine wakifanya hawafanikiwi kabisa.
Ili kuepuka kupoteza muda na nguvu falsafa ya ustoa inatufundisha na kutualika tujitambue na kuishi kulingana na upekee na utofauti wetu ambao tunao na siyo kuiga maisha ya wengine kwani kuiga maisha ya wengine ndiyo chanzo cha wengi kuwa na maisha magumu.
Na kikwazo kikubwa kinachofanya watu kushindwa kuishi maisha halisi kwao ni kutokujitambua na hivyo kujikuta wakiiga watu wengine.
Kujitambua ni zawadi kutoka kwenye asili au kutoka kwa Mungu.
Ni muhimu sana kujitambua wewe mwenyewe ili uweze kuishi maisha yako halisi kwako.
Kwa sababu, zama tunazoishi ushauri wa maisha umekuwa mwingi. Wengi wanajikuta wakiiga maisha ya wengine kwa namna mbalimbali na hivyo licha ya kuweka juhudi kubwa na muda bado watu hawafanikiwi.
Kwenye falsafa ya ustoa, kuna vitu vinne muhimu ambavyo mtu anapaswa kuvijua kuhusu yeye mwenyewe ili aweze kujitambua na kuishi maisha halisi kwake.
Kitu cha kwanza ni asili yetu kama binadamu.
Sisi binadamu tuna asili inayotutofautisha na viumbe wengine wote hapa ulimwenguni. Na asili yetu kubwa ni uwezo wa kufikiri na kufanya maamuzi. Hicho ndiyo kitu ambacho kinapatikana kwa binadamu pekee na chenye nguvu kubwa.
Lazima uijue asili hii na uweze kuitumia ili kuishi maisha halisi kwako. Kila mara jiulize kama umefikiri na kufanya maamuzi au unafuata tu mkumbo. Wanyama huwa wanafuata mkumbo, wewe usiwe kama wao.
Kitu cha pili ni uwezo na vipaji ulivyonavyo.
Kila mtu ana uwezo wa kipekee na mkubwa sana ambao amezaliwa nao. Uwezo ambao hauwezi kupatikana kwa mtu mwingine yeyote. Na kila mtu ana vipaji vyake, vitu anavyoweza kuvifanya vizuri na kwa upekee mkubwa.
Jua uwezo wako na vipaji vyako na kuvitumia, maana hiyo ndiyo njia pekee ya kuishi maisha halisi kwako. Uzuri ni kwamba uwezo mkubwa na vipaji vyetu huwa havipotei, vinabaki na sisi maisha yetu yote na hakuna mtu anaweza kutunyang’anya.
Kitu cha tatu bahati tunazokutana nazo kwenye maisha.
Kuna mambo mengi yanayotokea kwenye maisha yako ambayo hayapo ndani ya udhibiti wako. Hayo yote huwa yanakuja na fursa nzuri ambazo ukiweza kuzitumia utaishi maisha halisi kwako.
Bahati zinaweza kuwa eneo ulilozaliwa, elimu uliyopata, watu unaokutana nao na kadhalika. Tangu umezaliwa mpaka sasa umepitia mambo mengi ambayo ukiweza kuyatumia vizuri utaishi maisha halisi.
Kitu cha nne ni utashi wetu ambao unabebwa na kusudi na ndoto tunazokuwa nazo.
Yale unayochagua kufanya kwenye maisha yako, ambayo yanatokana na msukumo ulio ndani yako yanakufanya uishi maisha halisi kuliko yale unayoiga. Hivyo ni muhimu sana ulijue kusudi lako na uwe na ndoto kubwa zinazotoka ndani yako ili kuwa na maisha halisi kwako.
Hatua ya kuchukua leo; Jitambue wewe mwenyewe kwanza na zingatia hivi vitu vinne vitakavyokusaidia kujitambua.
Ustoa unasisitiza sana tujitambue sisi wenyewe ili tusisumbuke na mambo yasiyo sahihi kwetu.
Rafiki na Mstoa mwenzako
Mwl Deogratius Kessy
Asante sana Mwalimu Deo, kukitambu kwenye maisha yetu ni muhimu ili tusiishi maisha ya wengine badala yake tuishi maisha yetu. Kufikiri na kufanya maamuzi, uwezo na vipaji, bahati tunazokutana nazo pamoja utashi wetu ni nyenzo muhimu za sisi kujitambua. Na tusipojitambua, tutajitaidi kujitambulisha bila mafaniko: Asante sana
LikeLike
Kujitambua mwenyewe ni hutaji muhimu sana kuelekea kuwa na maisha ya mafanikio ya kweli.
LikeLike
Haya mambo manne ni muhimu sana
LikeLike
Asante mwl Deo kwa Elimu nzuri ya ustoa, nitaendelea kujifunza zaidi
LikeLike