3071; Maamuzi na utekelezaji.

Rafiki yangu mpendwa,
Tunajua jinsi ambavyo wanaoyataka mafanikio ni wengi, lakini wanaoyapata wakiwa wachache sana.

Tumeshajifunza sababu nyingi zinazowatofautisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa.

Hapa tunakwenda kuangalia eneo moja ambalo siyo kwamba halifanyiki kabisa, bali halifanyiki kwa usahihi.

Eneo hilo ni kufanya maamuzi na utekelezaji wa maamuzi hayo.

Watu wasiofanikiwa huwa wanachelewa sana kufanya maamuzi.
Na hata wakishayafanya, hawayawekei mkazo kwenye utekelezaji.
Na wapo haraka sana kwenye kuvunja maamuzi hayo pale wanapokutana na magumu.
Kwa njia hii, wanafanya mengi, lakini hawafanikiwi.

Mafanikio yanataka vitu vitatu vifanyike kwa uhakika kwenye eneo la maamuzi.
Moja ni maamuzi kufanyika haraka.
Mbili ni maamuzi kutekelezwa kwa juhudi kubwa.
Na tatu ni maamuzi kutekelezwa kwa msimamo bila kuacha.

Ni muhimu sana kufanya maamuzi haraka kwa sababu huwa kuna dirisha dogo sana la muda wa kunufaika na fursa yoyote inayokuwa imejitokeza.
Wengi huchelewa kufanya maamuzi kwa sababu wanasubiri mpaka wawe tayari kwa kila kitu.
Kusubiri uwe tayari ni kujichelewesha na kujipotosha.
Unapaswa kufanya maamuzi kwanza halafu kuendelea kujiandaa kadiri unavyokwenda.
Kama kitu ni muhimu, fanya maamuzi hata kama bado hujawa na maandalizi ya kila kitu.

Ukishafanya maamuzi, kinachofuata ni kuyafanyia kazi kwa uhakika.
Wengi wakishaamua wanakuwa kama wanajaribu.
Hawaweki juhudi zao zote kwenye maamuzi waliyofanya.
Badala yake wanakuwa kama wanabahatisha.
Kinachotokea ni wanakutana na magumu na changamoto, ambazo zinawayumbisha sana.
Chochote unachoamua, lazima ukifanyie kazi kwa juhudi kubwa sana, hata kama huna uhakika nacho.
Fanya kila kinachopaswa kufanyika ili maamuzi uliyofanya yazalishe matunda mazuri.

Msimamo kwenye kutekeleza maamuzi yaliyofanyika ni kitu ambacho kinakosekana sana kwa walio wengi.
Wengi hufanya maamuzi kwa kuchelewa, hawayafanyii kazi kwa uhakika na pale wanapokutana na vikwazo au changamoto, wanaacha kufanya.
Kama kukutana tu na changamoto kunakukatisha tamaa na unaacha, hautaweza kufanikiwa kwenye jambo lolote lile.
Kwa sababu magumu, vikwazo na changamoto ni sehemu ya safari ya mafanikio.
Na kwa sababu unafanya maamuzi kwa haraka, kuna mengi utakuwa huna maandalizi nayo.
Unatakiwa kuwa na msimamo mkali sana kwenye kuyatekeleza maamuzi uliyoyafanya.
Umefanya maamuzi kwa sababu kuna matokeo unataka kuyapata, usivunje maamuzi hayo kama hujapata matokeo uliyotaka.
Unachoweza kufanya ni kuendelea kuboresha kadiri unavyokwenda.
Unapoyafanyia kazi maamuzi yoyote yale kwa msimamo bila kuacha, unajiweka kwenye nafasi ya kupata matokeo bora.

Ni hayo ya msingi kabisa kwenye maamuzi,
Fanya maamuzi haraka, usisubiri mpaka uwe umekamilika.
Weka juhudi kubwa kwenye maamuzi unayofanya, usijaribu, fanya kwa uhakika.
Kuwa na msimamo kwenye kufanyia kazi maamuzi yako, usiache kwa sababu ya changamoto, badala yake endelea kama ulivyoamua, matokeo mazuri huwa yapo mbele.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe