3080; Mwili na mazingira.

Rafiki yangu mpendwa,
Tunaweza kuona tuna mambo mengi sana ambayo tunakabiliana nayo kwenye safari yetu ya mafanikio makubwa.

Lakini kiuhalisia, mambo hayo yote yamegawanyika kwenye makundi makubwa mawili; mwili na mazingira.

Mapambano ya kwanza kwetu ni ya kimwili.
Miili yetu ni kikwazo cha kwanza kwetu kuyafikia mafanikio makubwa tunayoyataka.

Kikwazo cha mwili kinatokana na mambo makubwa matatu;
Moja ni uvivu wa mwili kutokutaka kufanya mambo magumu. Huu unavukwa kwa kuusukuma mwili kufanya yale yanayotakiwa kufanyika.
Mbili ni tamaa ya mwili kutaka kupata vile inavyotamani, ambavyo huwa ni vya anasa na vinavyopingana na kile mtu anataka. Hii inavukwa kwa kuwa na udhibiti kwa mwili.
Tatu ni uchovu na udhaifu wa mwili unaotokana na afya kutokuwa imara. Hii inavukwa kwa kujenga afya imara.

Kushinda vikwazo vya mwili pekee haitoshi kupata ushindi tunaoutaka.
Kwani kuna watu wanatumia miili yao vizuri, lakini bado hawafanikiwi.
Hiyo ni kwa sababu wanakuwa wameshindwa kushinda vikwazo vya mazingira.

Mazingira yamekuwa kikwazo kikubwa kwa watu wengi kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao.
Kuyashinda mazingira ni mapambano mengine ambayo yapo kati yetu na mafanikio tunayoyataka.

Kwenye mazingira kuna vikwazo vikubwa vitatu vya kuvuka ili kufanikiwa.
Moja ni kufuata mkumbo. Sisi binadamu ni viumbe wa kijamii na tunapenda kuiga yale ambayo wengine wanayafanya. Lakini hilo ni kikwazo sana kwenye mafanikio makubwa. Kwa sababu ukifanya kile wanachofanya wengine, utaishia kupata matokeo wanayopata, ambayo huwa siyo matokeo bora.

Mbili ni njia za mkato za kufanikiwa. Kuna njia nyingi za mkato za kupata mafanikio ambazo huwa zinapigiwa debe sana. Ni rahisi kushawishika kutumia njia hizo, lakini matokeo yake huishia vibaya. Kitu pekee ambacho watu huwa wanakipata kwenye njia za mkato ni mikato, yaani kupoteza zaidi.

Tatu ni usumbufu.
Kuna usumbufu wa kila aina kwenye mazingira yanayotuzunguka. Usumbufu huo unanasa umakini wetu, kuiba muda wetu na kutumia nguvu zetu kwa namna isiyo sahihi.
Watu wengi hudhani usumbufu ni mpaka kiwe kitu kibaya.
Lakini usumbufu ni chochote ambacho hakina mchango kwenye malengo unayotaka kuyafikia.
Ni lazima uachane na yote yasiyo muhimu ili kuweka kipaumbele kwa yale muhimu tu.

Wajibu wako mkubwa kwenye hii safari ya mafanikio ni kutumia vizuri mwili na mazingira yako badala ya kukubali viwe kikwazo kwako.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe