Rafiki yangu mstoa,
Wote tunajua ukingo wa mto au bahari jinsi ulivyo, mara nyingi mawimbi ya bahari au hata mto huwa yanapiga kwenye ukingo wa mto au bahari. Lakini hata ukingo wa mto au bahari upigweje na mawimbi haujawahi kuacha kazi yake ya kusimama imara na kuyatuliza mawimbi ya maji.
Mawimbi ya maji ni kama vile yale magumu ambayo tunakutana nayo kwenye maisha yetu ya kila siku. Na sisi ndiyo tunapaswa kuwa kingo imara katika maisha yetu ili yale magumu yanayotukuta yanatuacha kuwa imara huku tukisimama na kuyatuliza mawimbi ya maji ambayo ndiyo changamoto zenyewe.
Kwenye maisha unapaswa kuwa mstahimilivu, kwa sababu maisha siyo rahisi, hakuna chochote kwenye maisha yako kitaenda kama vile unavyotaka wewe au ulivyopanga wewe.
Kwenye maisha utakutana na changamoto na magumu ambayo yatakuangusha na kujaribu kukukatisha tamaa. Lakini wewe unapaswa kuwa mwamba, mstahimilivu ili uweze kukabiliana na mikikimikiki ya maisha.
Moja ya shabaha ya falsafa ya Ustoa kwenye safari yetu ya kuelekea UBILIONEA ni kutujenga tuwe wastahimilivu kwani tutakutana na magumu mengi lakini falsafa hii inatuandaa kukutana na magumu na hata kuyavuka bila kukata tamaa.
Mwanafalsa wa Ustoa Marcus Aurelius kwenye moja ya nukuu yake anasema,
Kuwa kama ukingo wa mto au bahari ambao unapigwa na mawimbi ya maji kila mara lakini unaendelea kusimama imara kuyatuliza mawimbi ya maji. Chochote kibaya kinapotokea, usijiambie nina bahati mbaya hiki kimetokea kwangu, badala yake jiambie nina bahati nzuri hiki kimetokea kwangu kwa sababu nitaweza kukikabili bila kukasirika au kuumizwa nacho kwa sasa au wakati ujao. Kitu kama hicho kingeweza kutokea kwa yeyote, lakini siyo kila mtu anaweza kukipokea.
Nukuu;
Be like the headland, on which the waves break constantly, which still stands firm, while the foaming waters are put to rest around it. ‘It is my bad luck that this has happened to me.’ On the contrary, say, ‘It is my good luck that, although this has happened to me, I can bear it without getting upset, neither crushed by the present nor afraid of the future.’ This kind of event could have happened to anyone, but not everyone would have borne it without getting upset. – Marcus Aurelius
Ili kuzuia mabaya yanayotokea yasituvuruge, tunapaswa kuwa na maandalizi ya mabaya na magumu yanayoweza kutokea.
Jiandae kwa magumu kwa kuishi magumu yenyewe kwa kujiweka katika nyakati ngumu hata kama hujafikia ugumu huo.
Pia, jijengee taswira hasi ya magumu kabla hata hayajatokea.
Siyo kwamba kujiandaa na magumu ni kujifanyia uchuro ila unajiandaa na matokeo ya pande zote mbili hata yakitokea hayatakushtua.
Chochote ambacho kinakuja kwako bila ya wewe kutegemea jiulize swali hili, hili nalo limekuja kwangu kwa kusudi gani?
Kila jambo ambalo asili inakuletea kwako huwa na kusudi ndani yake. Usikimbilie tu kujiambia una bahati mbaya bali kimbilia kujiambia nina bahati nzuri na hili limekuja kwangu kwa sababu nitaweza kukabiliana nalo.
Chochote kinachokuja kwako hebu jiulize kwa nini hajapelekewa mtu mwingine na umepewa wewe? Kama jambo limekuja kwako jua wewe umeandaliwa kulipokea.
Hatua ya kuchukua leo; kuwa mstahimilivu.
Kitu kimoja zaidi, kuwa kama ukingo wa mto au bahari ambao unapigwa na mawimbi ya maji kila mara lakini unaendelea kusimama imara na kuyatuliza mawimbi ya maji.
Rafiki na mstoa mwenzako,
Mwl Deogratius Kessy
Be like the headland, on which the waves break constantly, which still stands firm, while the foaming waters are put to rest around it. ‘It is my bad luck that this has happened to me.’ On the contrary, say, ‘It is my good luck that, although this has happened to me, I can bear it without getting upset, neither crushed by the present nor afraid of the future.’ This kind of event could have happened to anyone, but not everyone would have borne it without getting upset. – Marcus Aurelius
LikeLike
Asante sana mwl Deo,kuwa kama ukingo wa mto wa mto au bahari,tunaishi kwenye jamii, familia na ktk kufanya biashara zetu,haya yote kweli tunakutana nayo,kama uluvyosema muhimu ni kuwa wavumilivu
LikeLike