3142; Sikosi hela ya kula.

Rafiki yangu mpendwa,
Matokeo yoyote ambayo mtu unayapata yanalingana na fikra ambazo mtu unakuwa nazo.
Unachopata ni sawa sawa kabisa na picha uliyonayo kwenye fikra zako.

Kwa mfano kama kwenye fikra zako unajisifu kwamba kwenye shughuli zako hukosi hela ya kula, hicho ndiyo utakachoishia kupata, hela ya kula.
Hata upambane kiasi gani, bado utaishia tu kupata hela ya kula.
Siyo kwa sababu huna uwezo wa kupata zaidi, bali kwa sababu hicho ndiyo unachoridhika nacho.

Kwenye maisha huwa hatupati kile tunachostahili kupata, bali tunapata kile tunachokubali na kuvumilia kupata.
Hivyo kama ukipata hela ya kula unakubali na kuridhika, hakuna namna utapata zaidi ya hapo.
Na hata ikitokea kwa bahati umepata zaidi ya hiyo hela ya kula, utaishia hata kuumwa, ili tu usiendelee kutafuta zaidi ya hapo.

Hivyo basi rafiki, kabla ya kuhangaika na matokeo unayopata, anza na fikra ulizonazo juu ya matokeo hayo.
Ni kitu gani huwezi kukubali au kuvumilia? Hicho ndiyo utakachoishia kupata.

Huwa natoa mfano huu wa maeneo ya mjini. Huwa ni nadra sana kusikia mtu amekufa kwa njaa mjini, lakini ni kawaida kuona watu wakiwa wamelala nje, yaani hawana pa kulala.
Watu hao ambao hawana pa kulala, huwa wanahakikisha wanapata chakula, kwa namna yoyote ile.
Lakini wakishapata chakula, wanaridhika, hata kulala nje hakuwaumizi sana.

Kiwango ambacho watu wanakulipa na hata heshima ambayo watu wanakupa, huwa vinaanzia kwenye kile unachokubali kupokea.
Utapata kile tu ambacho umekubali kupokea, unaweza kuvumilia na siyo zaidi ya hapo.
Hata aina ya watu unaowapata kwenye maisha yako, ni wale unaoweza kuwavumilia.

Unaweza kuwa na ndoto na malengo makubwa sana kwenye maisha yako, lakini kama utakubali kupokea chochote chini ya hapo, hicho ndiyo utaishia kukipata.
Kama kupata hela ya kula kunakuridhisha, kimuujiza utakuwa unaishia kupata hela ya kula tu na siyo zaidi ya hapo.

Chochote kile unachotaka kupata, kataa kata kata kupokea na kuvumilia kilicho chini yake.
Utaona wengine wakipata na kufurahia kiwango hicho, lakini wewe hupaswi kufanya hivyo.
Tena wengi watakuambia uridhike kwa sababu unapata vizuri, hupaswi kukubaliana nao.
Ng’ang’ana kupata kile unachotaka na siyo chini ya hapo na hivyo ndivyo utakavyoweza kupata matokeo makubwa zaidi.

Hilo linakwenda hata kwa juhudi unazoweka, kama unaridhishwa na juhudi za kawaida, hizo ndiyo utajikuta unaziweka muda wote.
Ukishaweka juhudi hizo za kawaida, utachoka kabisa na kuona umefanya makubwa sana.
Lakini pale unapokataa kuridhika na juhudi za kawaida, unapata nguvu na hamasa ya kuendelea kuweka juhudi kubwa zaidi.

Maisha ni maigizo, tunachopata ni matokeo ya uhusika tuliochagua kuuvaa.
Kama unataka kupata matokeo ya tofauti na unayoyapata sasa, anza kwa kuvaa uhusika wa tofauti na unaouvaa sasa.
Kuwa na fikra mpya kabisa,
Jione wa tofauti kabisa,
Na kataa kata kata kupokea chochote chini ya kile unachotaka.

Utaanza kwa kupata chini ya kile unachotaka, lakini kwa sababu hutaridhika na hilo, utaendelea kujisukuma zaidi na kupata kile unachotaka.

Adui mkubwa kwenye kupata makubwa ni kuridhika na kujivunia kwa madogo.
Ukishajiona uko na shauku ya kujisifia kwa matokeo madogo unayoyapata, jua hutapata zaidi ya hayo.
Kama huoni aibu na kukasirishwa na matokeo unayoyapata, hutaweza kupata zaidi ya hapo.

Wengi wanataka sana kupata matokeo makubwa, lakini fikra zao zinawasaliti. Ile picha wanayokuwa nayo kwenye fikra zao ndiyo wanayoishia kuipata.
Anza na fikra zako na picha unayokuwa nayo na kataa kata kata kukubali chochote chini ya hapo.

Kama unaridhika kupata hela ya kula, kwa uhakika hutakufa njaa. Lakini pia kwa uhakika hutapata zaidi ya hiyo hela ya kula. Siyo kwa sababu Mungu au asili inakupenda sana usife njaa, bali kwa sababu wewe ndiye umepokea na kuvumilia hayo. Chochote ambacho hutaki, usikubali kukivumilia kwa namna yoyote ile.

Hii dunia ina utele wa kila kitu.
Kuna fursa za kila mtu kuweza kupata kile anachotaka.
Lakini hilo linaanzia ndani ya mtu kwanza kabla ya kile ambacho dunia inampa.
Kama unataka dunia ikupe zaidi, kataa kupokea chochote ambacho ni chini ya unachotaka.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe