3229; Usivyoweza kununua.

Rafiki yangu mpendwa,
Kuna vitu vingi ambavyo unaweza kuwalipa watu na wakakusaidia kwa namna ambayo unarahisisha na kuharakisha matokeo.

Unaweza kuwalipa watu wakufundishe na kukuonyesha kile unachopaswa kukifanya.
Unaweza kuwalipa watu wakusaidie kwenye kufanya kile unachopaswa kufanya na ukaweza kuzalisha matokeo makubwa zaidi.

Hivyo ndivyo ukuaji mkubwa huwa unapatikana, kupitia kutumia rasilimali za watu wengine ambazo unaweza kuzinunua.

Lakini kuna kitu kimoja kinachohitajika sana kwenye mafanikio ambacho huwezi kukinunua kwa gharama yoyote ile.
Kitu hicho ni ile nia ya ndani ya kutaka kufanikiwa.

Ule msukumo wa ndani wa kutaka kufanikiwa, unaokufanya uwe tayari kuchukua hatua na kuvumilia magumu ni kitu ambacho huwezi kulipa wengine wakakupa.

Hicho ni kitu ambacho kinaanzia ndani ya mtu pekee.
Ndiyo kitu kinachomsukuma mtu kufanya mengine muhimu anayoyahitajika kufanya ili kufanikiwa.

Kuna kitu kingine ambacho pia ni vigumu kuweza kukinunua kwenye safari yako ya mafanikio.
Kitu hicho ni kasi ya kupata matokeo.

Mara nyingi umekuwa unayataka matokeo kwa haraka sana.
Na unakuwa tayari kuingia gharama mbalimbali ili upate matokeo makubwa kwa haraka.

Kitu unachopaswa kujua ni kwamba huwezi kununua kasi ya kupata matokeo makubwa unayoyataka.
Matokeo yote unayopata yanajengwa kupitia mkusanyiko wa hatua mbalimbali zinazokuwa zimetangulia.

Kila juhudi inayowekwa, inakuwa na mchango kwenye matokeo yanayokuja kupatikana.
Hakuna njia ya kuharakisha mchakato huo wa hatua mbalimbali kujikusanya na kuzalisha matokeo makubwa.

Kuna watu wanauza siri mbalimbali za mafanikio.
Vitu vingi kuhusu mafanikio viko wazi, lakini kwa sababu watu wanathamini zaidi siri, kilicho wazi kikiitwa siri wanakuwa tayari kukilipia.

Ukishajikuta unatumia muda mwingi wa kutafuta siri za kitu chochote kile, jua tayari umeanza kupotea.
Utapoteza gharama nyingi kulipia vitu ambavyo haviwezi kufanya kazi kwa namna yoyote ile.

Ijue misingi sahihi ya kila kitu na ifuate hiyo.
Kwa sababu misingi huwa haitetereki, ukiifuata hiyo utakuwa salama muda wote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe