3243; Vitu vinavyokupa ushindi.

Rafiki yangu mpendwa,
Msukumo wa kwanza kwetu kwenye chochote tunachofanya ni kupata ushindi.
Kila mtu anapenda ushindi, ni kiashiria kwamba mambo yamefanyika kwa usahihi.

Lakini watu ambao wamekuwa wanapata ushindi mzuri na unaodumu wamekuwa ni wachache sana.
Zipo sababu nyingi ambazo zimekuwa zinawakwamisha wengi wasipate ushindi mkubwa wanaoutaka.

Moja ya sababu kubwa inayowazuia wengi kupata ushindi ni kutokujua vitu sahihi vinavyoleta ushindi wanaotaka.
Wengi wanajikuta wakihangaika na mambo ambayo kwa nje yanaonekana ndiyo yanawapeleka kwenye ushindi, lakini kwa ndani mambo yanakuwa tofauti.

Wengi ambao hawapati ushindi wamekuwa wanahangaika na vitu ambavyo kwa nje vinaonekana kuwa vipya na vya tofauti.
Wanakuwa wanahangaika na vitu vinavyovutia na kusisimua kufanya.
Lakini ushindi halisi unatokana na kufanya mambo ya msingi kwa ukubwa na muda mrefu bila kuacha.

Mambo hayo ya msingi ndiyo yamekuwa yanapuuzwa na wengi ambao hukimbizana na mambo mapya na ya kusisimua kila mara.
Wanajikuta wakiwa wamefanya vitu vingi, lakini ushindi hakuna.

Tuangalie mfano kwenye eneo la biashara.
Unapata ushindi kwenye biashara kwa kufanya vitu vya msingi kwa ukubwa na msimamo.

Unakazana kuongeza mapato kwa kukuza mauzo ya biashara. Kwa kuwa mauzo ndiyo moyo wa biashara, yanapaswa kupewa kipaumbeke kikubwa.

Matumizi yanatakiwa kudhibitiwa ili yasimeze kipato chote. Huwa ni rahisi kwa matumizi kuongezeka pale mapato yanapoongezeka. Hilo linapotokea, ukuaji unakuwa mgumu.

Unatakiwa kuwa na timu nzuri ya watu wanaoiendesha biashara yako. Huwezi kufanya kila kitu peke yako kwenye biashara na ikapata mafanikio makubwa.
Unahitaji watu, na siyo tu watu ni watu, bali watu bora. Na hapa ndipo unapohitaji kuwa unaajiri vizuri.

Kuwajali sana wateja wa biashara ni kitu kingine cha msingi na muhimu kinachopaswa kufanyika.
Kila kinachofanywa kwenye biashara kinalenga kutoa thamani kubwa zaidi kwa wateja. Kwa umakini mkubwa kuwekwa kwa wateja, inakuwa rahisi kuwabakisha kwa muda mrefu na kuwavutia wengine.

Mwisho ni kujipa muda kwenye kila kinachoamuliwa kufanyika, kufanya kwa ukubwa na msimamo kwa muda mrefu bila kuacha.
Wengi wanashindwa siyo kwa sababu wanachofanya hakiwezekani, bali kwa sababu wanakuwa wamekata tamaa na kuacha kabla hawajafikia ushindi.

Rafiki, acha kuhangaika na vitu vya kusisimua ambavyo ndivyo kila mtu anahangaika navyo.
Badala yake fanya yale mambo ya msingi kwa ukubwa na msimamo.
Hayo ndiyo yatakayokupa ushindi mkubwa na wa ukahika mara zote.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe