3279; Uhakika wa ushindi.

Rafiki yangu mpendwa,
Watu wamekuwa wanahangaika sana kupata ushindi, lakini wamekuwa hawaupati.

Hiyo ni kwa sababu wengi wamekuwa hawauelewi ushindi.
Wanahangaika na mengi na kutaka kupata matokeo makubwa na ya haraka.
Wakichelewa kupata matokeo wanayotaka, wanaacha na kwenda kwenye kitu kingine.

Uhakika wa ushindi siyo kupata kile unachotaka, bali kutokuacha kufanya kile unachofanya ili kupata ushindi.
Kama utafanya kitu kwa muda mrefu zaidi, kupata ushindi ni uhakika kabisa.

Wengi wanakosa ushindi kwa sababu wanaacha kufanya mapema.
Kama wangeendelea wangeweza kukutana na fursa nzuri ya kushinda.
Lakini wanakuwa wameacha mapema.

Lakini pia wengi wanadhani ushindi ni kufanya mambo makubwa na magumu.
Wanahangaika na hayo na bado hawashindi.
Ukweli ni ushindi ni kufanya mambo rahisi na ya msingi, kwa msimamo bila kuacha.
Kwa kufanya yale mambo ya msingi kabisa mara zote, matokeo makubwa na ya tofauti yanapatikana.

Kwa vigezo hivi viwili vya ushindi tulivyoona, vinafanya ushindani kuwa mdogo sana.
Siyo kwa sababu ushindi ni mgumu, bali kwa sababu wengi ni wepesi sana na hawawezi kukabiliana na hali hizo.

Watu wengi hawawezi kufanya kitu kwa muda mrefu, hasa kama hawaoni matokeo ya haraka.
Hivyo wengi wanaacha haraka kufanya na kuacha uwanja wa ushindani ukiwa tupu.
Kama utajiambia tu kwamba huachi kufanya hata iweje, huo tayari ni ushindi.
Maana wengi hawawezi hilo.

Na pia, wengi hudhani kama kitu siyo kigumu basi hakiwezi kuleta matokeo makubwa.
Hivyo huwa wanahangaika na magumu ambayo yanawachosha na kuwapoteza.
Wewe ukisimamia yale ya msingi, ambayo pia ni rahisi, unakuwa mbele sana ya hao wengine.

Ushindi ni wa uhakika kwako kama utayazingatia hayo ya msingi kabisa.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#BilioneaMafunzoni
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe