3571; Dunia ni katili sana kwa watu hawa.
Kutoka mezani kwa Kocha,
Rafiki yangu mpendwa,
Watu wengi wamekuwa wanalalamika jinsi ambavyo dunia imekosa usawa.
Wamekuwa wanaonyesha kwa mifano halisi jinsi ambavyo baadhi ya watu wanapata upendeleo kuliko wengine.
Ipo wazi jinsi ambavyo wale wenye fedha huwa wanapata fursa nzuri za kupata fedha zaidi kuliko ambao hawana fedha.
Au wale waliotokea familia zenye uwezo mkubwa, wamekuwa wakipendelewa kwenye baadhi ya mambo kuliko waliotoka familia za chini.
Watu wanaweza kulalamikia kukosekana kwa usawa, lakini malalamiko hayo hayatatatua hilo.
Dunia haitakuja kuwa sawa hata siku moja.
Ni kanuni ya asili kwamba chenye nguvu kitanufaika zaidi kuliko kisichokuwa na nguvu.
Uzuri ni kwamba, kwetu sisi binadamu tunao uwezo wa kujijenga wenye nguvu badala ya kubaki dhaifu.
Dunia huwa ni katili sana kwa watu masikini na dhaifu.
Dunia inawageuza kutumiwa na wengine na kuwanufaisha hao huku wao wakizidi kuwa masikini na dhaifu.
Wajibu wako namba moja ni kutoka kwenye hali hizo zinazoifanya dunia iwe katili kwako.
Kwanza pambana sana kutoka kwenye umasikini. Ukatae umasikini na mambo yake yote kwa kila namna.
Hakikisha unaondoka kabisa kwenye umasikini.
Uzuri ni njia za kutoka kwenye umasikini zipo wazi kwa watu wote.
Ni wewe kuzifanyia kazi ili dunia iache kuwa katili kwako.
Baada ya kutoka kwenye umasikini, ondoka kwenye udhaifu. Usikubali kabisa kuwa dhaifu na unayeweza kuonewa na yeyote.
Kuwa imara kiasi cha watu kuogopa kukuchezea na kukutumia vile wanavyotaka wao.
Wafanye watu wajifikirie kabla hawajafanya chochote kinachokuhusisha.
Uzuri ni ukishatoka kwenye umasikini, ni rahisi pia kutoka kwenye udhaifu.
Maana kama wanavyosema, hakunaga maskini jeuri.
Ukiwa masikini huwezi kusema hapana, kwa sababu njaa haina huruma.
Ukishatoka kwenye umasikini, unaweza kusema hapana kwenye mengi na hilo likawafanya watu wakuheshimu.
Rafiki, ni mara ngapi umekuwa unalalamika kwamba dunia haina usawa? Kwamba kuna watu wanapata upendeleo kuliko wewe?
Kila unapolalamika au kufikiria hilo, jikumbushe kutoka kwenye umasikini na kuacha kuwa dhaifu.
Tambua ni wajibu wako namba moja kutoka kwenye umasikini na kutokuwa dhaifu ili dunia iache kuwa katili kwako.
Kutoka kwa rafiki yako anayekupenda na kukujali sana,
Kocha Dr. Makirita Amani, MD, CFE
+255 678 977 007 | http://www.amkamtanzania.com
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
#UpekeeUdadisiUbunifu
#UshirikianoUtegemeanoUwajibikaji
#NajengaBiashara
#HakunaKingineMuhimu
#BilioneaMafunzoni
#LazimaNitoboe
#NawekaKaziNifanikiwe