Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Wakati wa vita ya pili ya dunia, wamarekani walikuja na mkakati wao wa kivita ambao haukuwa umezoeleka kabisa kwenye vita nyingi. Mkakati huo uliwashangaza wazungu, ambao walizoea mbinu zilizokuwa zinawapa ushindi huko nyuma.
Mkakati wa Wamarekani ambao uliwashangaza Wazungu ni pale walipokuwa wanakutana na tatizo au kikwazo. Wazungu walikuja na usema hii; ‘Wamarekani hawalitatui tatizo, bali hulizidi nguvu.’ Walichokiona ni mtindo wa Wamarekani kupeleka nguvu nyingi sana kwenye tatizo au kikwazo chochote kiasi cha kukiondoa kabisa.
Kwa Wazungu, walikuwa wamezoea kukagua tatizo kwa kina, kujua chanzo chake na kutatua kwa kufanyia kazi kwenye chanzo. Njia ambayo ilitumia rasilimali kidogo, lakini ilichukua muda na kuchelewesha matokeo. Kwa Wamarekani, kasi ilikuwa ndiyo kila kitu, hivyo kwa kutumia nguvu na rasilimali za ziada, waliweza kupata matokeo ya haraka.
Nimetafakari huu mkakati wa kivita kwa kina, na nikaona ndiyo mkakati pekee ambao mtu yeyote mwenye kiu ya mafanikio makubwa anapaswa kuutumia. Tena pale unapokutana na vikwazo na changamoto, ambacho ni kitu cha lazima, kwa mkakati huu wa kuzidi nguvu, matokeo yanakuwa uhakika.
Kwenye barua hii tunaenda kuuchambua zaidi mkakati huu wa kulizidi tatizo nguvu ili kulitatua na kupata mafanikio ambayo tunayataka.

1. Vikwazo Havikwepeki.
Kabla hatujaenda kwenye kuupeleka moto wenyewe, ambao ni kulizidi tatizo nguvu, nataka tukubaliane kitu kimoja kwanza. Kwa sababu tusipokubaliana kwenye hicho, utahangaika na kupoteza muda na nguvu zako nyingi.
Iwapo utayakimbia matatizo na vikwazo, hakuna lolote kubwa utakaloweza kufanya. Unapofanya jambo moja na kukutana na vikwazo, ukiacha na kwenda kwenye jambo jingine, huko nako pia utakutana na vikwazo. Hata pale unapoona kitu ni rahisi kabisa, mpaka uingie ndiyo utajua matatizo na vikwazo vyake.
Hivyo basi, kama utaenda ukikimbia matatizo na vikwazo, jua utahangaika na mengi mno. Na huo muda na nguvu unazopoteza kwenye kuhangaika na mengi, ungechagua kuweka kwenye tatizo au kikwazo kimoja, lazima ungekivuka na kupiga hatua.
Ni sawa na kuchimba kisima cha maji, kama umechimba na kukutana na mwamba, ukaacha na ukaenda kuanza kuchimba mahali pengine tena, nako ukakuta mwamba, ukaacha na kwenda kuanza pengine. Sehemu zote tatu unakuwa umekwama na maji huna. Lakini kama ungepeleka nguvu zote kwenye sehemu moja, ungevunja mwamba na kuyapata maji.
Kwa sababu matatizo na vikwazo havitakuja kukoma kwenye safari yetu ya mafanikio, njia pekee tuliyonayo ni kuhakikisha tunavishinda nguvu. Tusikimbie kwa namna yoyote ile, na wala tusifukie vichwa tukidhani vikwazo vitaondoka vyenyewe.
Sisi ndiyo wa kuondoa kila kikwazo na kutatua kila changamoto na tatizo linalotukwamisha kufanikiwa. Na pamoja na njia nyingine nyingi tulizonazo, njia ya kuzidi nguvu ni lazima itumike, kwa sababu inaleta matokeo mazuri na kwa haraka.
2. Weka Kila Kinachohitajika, Na Zaidi.
Moja ya kauli za hovyo sana kwenye kuyapambania mafanikio makubwa ni hii; ‘Nimefanya kadiri ya uwezo wangu ila imeshindikana.’ Ukisikia tu hiyo kauli, jua hakuna namna mtu angeweza kupata matokeo ya tofauti na aliyopata.
Ili kupata matokeo makubwa, hupaswi kufanya kadiri ya uwezo wako, bali unapaswa kufanya kadiri ya inavyohitajika, kisha kwenda zaidi ya hapo. Kufanya kadiri ya uwezo wako ni kujidanganya, kwa sababu hujui hata huo uwezo wako unaenda mpaka wapi.
Namna sahihi ni kufanya kadiri ya inavyohitajika, kuweka kila kinachotakiwa kuwekwa ili matokeo yapatikane. Na huishii hapo tu, lazima uende hatua ya ziada, kwa kufanya zaidi ya inavyohitajika. Hapa ndipo unapozidi nguvu chochote kinachokuwa mbele yako au kinachokukwamisha.
Hii ni kulazimisha ushindi pale mambo yanapoonekana kushindikana, ni kuhakikisha hakuna sababu yoyote ya kukwama, kwa sababu kila kilichohotajika kimewekwa, tena kwa kuzidi.
Fanya maandalizi ya kutosha, ambapo huachi chochote ambacho kinaweza kusababisha matokeo yasipatikane. Jiandae kwa kila kitu, hata kama kuna vitu ambavyo ni nadra kutokea, jiandae kana kwamba vitatokea. Kuwa na maandalizi ambayo hakuna kinachoweza kukukwepa.
Fanya kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyozoeleka au kutegemewa. Kama bado hujapata matokeo unayotaka, endelea kufanya. Endelea kuweka kazi kubwa, umakini mkali na muda unaohitajika ili kupata matokeo unayoyataka.
Hujaingia kwenye hii safari kwa kubahatisha, kuna kitu unataka kupata, kina gharama zake. Sasa wajibu wako ni kulipa hiyo gharama, na kubakisha kabisa chenchi huko, ili usiwe unadaiwa chochote.
Kujifunza mambo yote matano, soma #BaruaYaKocha hapa; #BZK071; Tatizo Likikushinda, Lipelekee Huu Moto, Litasalimu Amri Lenyewe.