Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Umetoka kwenye majukumu yako ya kila siku, umechoka kweli kweli na unasubiri usafiri wa umma ili uweze kurejea nyumbani. Siku hiyo daladala ni za shida na umesubiri kwa muda mrefu, giza linaingia na unaona utachelewa kufika. Mara inakuja daladala, iliyoandikwa kule unakoelekea, abiria mpo wengi, unagombania na kuingia ndani ya daladala, tena kwa kubahatika kupata siti.

Safari inaendelea, kondakta anachukua nauli. Mnapofika njia panda, unashangaa daladala inaenda upande ambao siyo unakoelekea wewe. Unashtuka na kumuuliza kondakta mbona daladala inaenda njia tofauti. Anakujibu kwamba hiyo ndiyo safari yao ya mwisho na gari inaenda kulala. Anakusisitiza kwamba siku zote watu wa njia hiyo wanajua usiku gari inaenda mwelekeo wa tofuati na safari yake.

Unafanya nini kwenye hali kama hii? Katika hali ya kawaida, unapaswa kushuka na kusubiri kupanda basi sahihi ambalo litakufikisha kule unakoelekea. Hilo linaeleweka kabisa.

Lakini sasa, cha kushangaza sana, sivyo unavyofanya kwenye maisha yako ya kila siku. Kwenye maisha yako umekuwa unang’ang’ania kubaki kwenye hilo basi, kwa sababu mbalimbali ambazo umekuwa unajipa.

Kwenye barua hii tunaenda kuangalia hizo sababu umekuwa unatumia kujipoteza kwenye safari yako ya mafanikio, kitu ambacho kimekuwa kikwazo kikubwa kwako. Tutaendelea na mfano wa basi, kwa sababu ambazo umekuwa unajikwamisha nazo kwenye maisha.

1. Kugundua Umepanda Basi Lisilo Sahihi.

Kugundua kwamba basi ulilopanda siyo sahihi, kwa maana kwamba aliendi kule unakotaka kufika, ni jambo linalohitaji uwe na umakini mkubwa. Ni lazima kwanza uwe unajua ni wapi unakoenda na kufuatilia mwenendo wa basi kuona kama kweli linaelekea huko.

Kama mtu huna umakini wa kutosha, kama umesongwa na usumbufu mwingi, hutaweza kujua kama basi ulilopanda siyo sahihi. Kwa mfano kama umeingia tu kwenye basi na kuanza kuperuzi simu yako, hutakuwa na umakini wa kuangalia safari nzima ina mwelekeo gani. Kwa njia hiyo utapotea bila kujua kwa haraka kama unapotea.

Kwenye maisha kuna mabasi mengi yasiyo sahihi ambayo tunayapanda, kitu ambacho siyo kosa, kwa sababu mara nyingi tunakuwa hatujajua. Kosa kubwa ni pale tunapochelewa kushuka kwenye mabasi hayo yasiyo sahihi, kwa kujua au kutokujua kwamba tupo kwenye basi lisilo sahihi.

Kwa sehemu kubwa, watu wengi wanachelewa kushuka kwenye basi kwa sababu hawajui kama basi walilopo siyo sahihi. Na hilo linatokana na usumbufu mwingi wanaokuwa wanahangaika nao kwenye maisha, ambao unawakosesha umakini wa kuona ni wapi basi walilopanda linaenda.

Tabia na nidhamu tulizonazo kwenye maisha yetu ni basi ambalo tumepanda. Basi hilo linatupeleka wapi inategemea na matokeo ya tabia na nidhamu hizo. Watu wengi wamekuwa na tabia na nidhamu ambazo zinawapoteza badala ya kuwapa matokeo wanayotaka, lakini hawajui na hata wakijua hawachukui hatua.

Njia unazotumia kuingiza fedha, iwe ni kazi au biashara ni basi unalokuwa umepanda. Basi hilo linaweza kuwa siyo sahihi, kwa sababu ya kiasi cha kipato tunachoingiza na malengo tunayokuwa nayo kifedha, lakini mtu anashindwa kujua mapema na kuchukua hatua. Kadhalika mambo mengine muhimu kifedha kama akiba, madeni na uwekezaji.

Biashara unayokuwa unafanya ni basi umepanda, ambalo licha ya kufurahia safari, linakoelekea inaweza isiwe kule unakotaka kufika wewe. Kama uliingia kwenye biashara ili uwe huru, halafu unaishia kua ndiye tegemezi kwenye biashara, basi ulilopanda siyo sahihi. Kadiri unavyochelewa kujua na kushuka, ndivyo unavyozidi kupotea.

Mahusiano unayokuwa nayo ni basi umepanda, yanakupeleka wapi inategemea na kile unachotaka na kama unafuatilia mwenendo wa mawasiliano hayo.

Afya, maarifa na kila eneo la maisha yako ni basi unakuwa umepanda. Ili uweze kupata matokeo unayotaka, lazima ujue basi ulilopanda linaelekea wapi na kama ndiko kweli unakotaka kufika.

Ili ujue hilo, ni lazima uweke umakini kwenye safari nzima. Uachane na usumbufu unaokuhadaa na kuisahau safari, kwa wewe kuamini ukishapanda kwenye basi ni kusubiri tu kufika mwisho wa safari.

Ni wajibu wako kukagua kila hatua ya safari ili kuhakikisha upo kwenye mwelekeo sahihi na unaendelea kuyapata matokeo uliyokuwa unategemea. Usisubiri mpaka mwisho wa safari ndiyo ugundue ulikofika siyo ulikotaka kwenda. Weka umakini mkubwa kwenye safari nzima, ili ugundue na kuchukua hatua haraka pale unapogundua mwelekeo siyo sahihi.

Kujifunza mambo yote matano, soma #BaruaYaKocha hapa; #BZK072; Msimamo Wa Kijinga Na Kuokoa Hasara Kunavyokupoteza Kimafanikio.