Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Kama kuna neno moja linalowakwamisha watu wengi kupata mafanikio makubwa ni; Nilidhani…. Mara zote neno hili huwa linakuja baada ya mtu kukosa kile ambacho angeweza kukipata. Lakini kwa kudhani, kuna vitu hakufanya kwa namna alivyopaswa kufanya na matokeo yake anakosa matokeo.

Kwa bahati mbaya sana, neno nilidhani huwa linakuja wakati ambapo mtu anaona hana tena namna ya kubadili matokeo ambayo ameshapata, au kupata matokeo ambayo ndiyo hasa aliyoyataka. Japo hilo siyo kweli, lakini wengi wakishafika kwenye hatua ya kusema nilidhani, nayo pia inakuwa ni kudhani.

Ukweli ni kwamba, kila tunachopaswa kufanya ili tupate mafanikio tunayotaka tunakijua na pia kipo ndani ya uwezo wetu kufanya. Tunapokosa mafanikio ni kwa sababu ya kudhani tunaweza kuyapata kwa njia nyingine tofauti na iliyo halisi. Na hiyo ni kwa sababu njia halisi haisisimui na watu wanapenda kusisimka.

Nani asiyejua matokeo yanaanza na tabia sahihi ambazo mtu unapaswa kuzijenga? Lakini wengi wanahangaika na njia za mkato za kupata matokeo. Licha ya njia hizo kuwaletea matokeo yasiyo sahihi, kila wanapokutana na njia mpya wanadhani hiyo ni sahihi.

Kadhalika kwenye fedha, njia za kujenga utajiri na uhuru wa kifedha zinajulikana kabisa, ongeza kipato, weka akiba, fanya uwekezaji. Lakini kila mara huwa inatokea michezo ya kitapeli, ambayo inawaahidi watu kupata utajiri wa haraka bila kuhitaji kufanya kazi sana. Na watu wanaingia, licha ya historia ya michezo ya aina hiyo kuwaliza watu. Ukiwauliza watakuambia walidhani hiyo mpya ni sahihi.

Kama unayataka mafanikio makubwa, na tena yatakayodumu kwa muda mrefu, ni lazima uachane kabisa na kudhani. Kwa sababu kudhani siyo tu kunakukwamisha, bali pia ndiyo kunawaangusha wengi wanaopata mafanikio.

Mtu asiye na fedha anaweza kudhani akipata fedha shida zake zote zinaisha. Ni mpaka unapowaangalia wengi wanaopata fedha bila kuzifanyia kazi kubwa, mfano wanaoshinda bahati nasibu, wanaopata mirathi au fidia ya kifedha. Wengi huwa wanaishia kuzipoteza zote ndani ya muda mfupi na kurudi kwenye hali zao za awali za kifedha.

Tatizo kubwa ni moja tu, kudhani. Walidhani kupata fedha ndiyo suluhisho pekee. Wakadhani kwa kuwa wana fedha basi wataendelea kuwa nazo. Kwa kudhani na kuendelea kudhani, wengi sana wamezama kwenye kushindwa.

Kwenye barua hii tunaenda kuangalia jinsi ya kufuta kudhani kwenye maisha yako ili ufanye yaliyo sahihi mara zote na kupata mafanikio yatakayodumu.

1. Fungua Kila Ukurasa, Usidhani Chochote.

Robert Caro ni mwandishi na mwanahistoria ambaye ameandika vitabu vya wasifu wa watu wawili waliowahi kuwa na mamlaka makubwa, Robert Moses and Lyndon B. Johnson. Amepata tuzo nyingi kupitia vitabu vyake, ambavyo huwa anaviandika kwa kina sana na vikiwa na kurasa zinazozidi elfu 1 kwa kitabu. Pia amekuwa anachukua muda mrefu kukamilisha kuandika kitabu, tofauti na anavyokuwa amepanga. Mwaka 2026, akiwa na umri wa miaka 90, anakamilisha kuandika kitabu cha 6, ambacho ni sehemu ya 5 ya mfululizo wa vitabu vya Lyndon B Johnson.

Robert Caro alianza kama mwandishi wa habari, akiwa ripota wa chini kabisa wa gazeti la Newsday. Akiwa hapo alipenda kufanya kazi mpaka mwisho wa wiki, ambapo mara nyingi alijikuta ofisini mwenyewe. Jumamosi moja jioni, akiwa ofisini peke yake, ilipigwa simu inayohusu taarifa muhimu za kiuchunguzi ambapo mwandishi alitakiwa kwenda kuzipata. Alipiga simu kwa mhariri ambaye alitafuta waandishi wazoefu wa kwenda na wakakosekana. Mhariri akamwambia inabidi aende yeye.

Caro alienda na kupata taraifa hizo nyeti, ambapo alizipitia kwa kina na kuandika habari husika kwa kutumia taarifa hizo. Kazi aliyoandika ilipita kwanza kwa mhariri, ambaye alimwita baada ya kuwa ameisoma. Mhariri akamwambia sikujua unaweza kuandika vizuri hivi, kuanzia sasa utakuwa unaandika habari za uchunguzo.

Caro alishtuka kusikia hivyo, na akamwambia mhariri; “Lakini sijui chochote kuhusu kuandika habari za uchunguzi.” Mhariri huyo alimpa jibu ambalo Caro amekuwa analitumia maisha yake yote na ndiyo limempa mafanikio makubwa kwenye uandishi wake.

Mhariri alimwambia; “Fungua kila ukurasa. Usidhanie chochote. Fungua kila aina ya ukurasa.”

Nilipokutana na hiyo kauli, nilijiambia wazi, huu hapa ni moja ya misingi muhimu sana ya mafanikio, kutokudhania chochote na kuhakikisha kinachopaswa kufanywa kinafanyika.

Yaani hata kama mtu hujui chochote kuhusu mafanikio unayotaka, ukishajua tu kwamba unataka mafanikio, kinachofuata ni kufungua kila ukurasa unaokutana nao katika kuyaendea mafanikio hayo. Kamwe usidhanie chochote, fanya kila kinachopaswa kufanyika, bila ya kujali ni kigumu au kinachukua muda mrefu kiasi gani.

2. Usiache Jiwe Juu Ya Jiwe.

Ni jambo moja kupewa ushauri na ukaona ni mzuri na unaweza kukupa matokeo. Lakini ni kazi kubwa kutekeleza ushauri huo kwa namna ambayo utakupa kweli matokeo unayoyataka.

Wakati Robert Caro ana anza kuandika kuhusu Lyndon B Johnson, alienda kwenye maktaba yenye maandiko yake yote. Alipotembezwa kwenye maktaba hiyo, alielezwa maandiko yote ya Lyndon yanazidi kurasa milioni 30. Aliposikia hivyo kichwa kilipata moto, akajiambia hakuna namna ataweza kutimiza ushauri wa kufungua kila ukurasa.

Lakini alipoanza kufanya kazi ya utafiti na uandishi, ilimchukua miaka 7 mpaka kutoa kitabu cha kwanza cha Lyndon. Na alijikuta akifungua kurasa nyingi zaidi kuliko alivyodhani. Matokeo yake ni alitoa kitabu ambacho kilikuwa cha kipekee sana kuhusu Lyndon, ambacho kilikuwa ni tofauti na vitabu vingi vilivyokuwa vimeandikwa.

Moja ya vitu vilivyonifurahisha kwenye Caro kufuata ushauri wa kufungua kila ukurasa ilikuwa ni zoezi la kwenda kufanya utafiti eneo alilozaliwa na kukulia Loyndon. Alipoenda kufanya huo utafiti kwa kuhoji wakazi wa eneo hilo, hakuwa anapata ushirikiano alioutaka. Alijaribu sana kuwashawishi wampe taarifa sahihi, lakini hakuzipata. Alipochunguza akagundua watu hao wamekuwa wanahojiwa na waandishi wengi, ambao huwa wanakuja na kuwahoji kisha wanaondoka. Hivyo walimwona Caro kama mtu wa kuja kuchukua taarifa na kuondoka.

Alipojua hicho ndiyo kikwazo, Caro alimwambia mke wake itabidi wahamie na kuishi kwenye eneo hilo. Kitu ambacho walikifanya, wakahamia na kuishi kwenye eneo hilo kwa miaka mitatu. Walipoonekana nao ni wakazi wa eneo hilo, alipata ushirikiano mkubwa na kupewa taarifa ambazo hakuna mwandishi mwingine amewahi kupewa.

Sidhani kama nimewahi kukutana na mtu mwingine aliyeweza kufuata ushauri sahihi kwa kiwango cha juu kiasi hicho. Na kwa kufanya hivyo, matokeo yamejidhihirisha wazi.

Watu wengi wanajifunza na kupata ushauri na mwongozo sahihi kuhusu mafanikio. Lakini inapofika kwenye utekelezaji, wanachagua nini wafanye, kile ambacho hakiwataki wasumbuke sana.

Mafanikio ni kugeuza kila jiwe unalokutana nalo kwenye safari yako, kutokuacha jiwe lolote kuwa juu ya jiwe jingine. Ni kufanya kila kinachopaswa kufanyika, kwa viwango vya juu sana.

Kwenye safari yako ya mafanikio, unaweza kusema kwa kujiamini kabisa kwamba umefanya kila kinachopaswa kufanyika ili kupata matokeo unayotaka?

Kwenye kujenga tabia na nidhamu sahihi ya mafanikio, je umekuwa unarudia rudia kufanya tabia zilizo sahihi hata pale ambapo hujisikii kufanya au una vitu vinakukwamisha?

Kwenye fedha, je umekuwa unatoa thamani kubwa na kuitoa kwa walio wengi ili uweze kuongeza kipato chako kwa uhakika? Na kwenye kila kipato, je umekuwa unaweka akiba na kuwekeza kwa msimamo bila kuacha?

Kwenye biashara, je umekuwa unapiga kelele kwa ukubwa kufikia wateja wengi? Na je umekuwa unaongea na wateja wengi zaidi kuwaonyesha thamani uliyonayo na kuwaambia wanunue? Na je kwa wanaokubali kununua, umekuwa unawapa huduma bora na kuendelea kuwafuatilia ili waendelee kununua?

Ukijitafakari na kuwa mkweli kwako, eneo lolote ambalo hujapata matokeo makubwa unayoyataka, hujafungua kila ukurasa, hujageuza kila jiwe. Na hiyo ni habari njema sana, kwa sababu unajua nini unachopaswa kufanya. Wajibu wako ni kwenda kufanya.

Kwenye #BaruaYaKocha unapata fursa ya kujifunza mambo mengine matatu yatakayokusaidia uache kudhania ili uweze kufanya makubwa na kufanikiwa.

Soma barua hiyo hapa; #BZK074; Hivi Ndivyo Kudhania Kunavyokukwamisha Wewe Kupata Mafanikio Makubwa