Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kitu kimoja kuhusu sisi binadamu ni pale tunapokwama kupata kile tunachotaka, huwa tunaanza kwa kuangalia nani au nini kimetukwamisha. Na uzuri vitu vya nje vya kulaumu kwenye kukwamisha ni vingi mno.
Huwa nasema sababu za kushindwa tayari zipo, ni wewe kuamua uchague zipi ambazo zinaendana na wewe, au unaweza kujidanganya nazo vizuri.
Ila inapokuja kwenye uhalisia wa kushindwa, inapokuja kwenye kile hasa kinachomkwamisha mtu kupata matokeo anayoyataka, jibu sahihi ni moja tu, yeye mwenyewe.
Haya siyo maneno mazuri kwetu kusikia na tumekuwa tunafanya kila jitihada kuhakikisha tuna sababu za nje za kushindwa, ambazo zina ushawishi mkubwa. Lakini hata tukiwa na sababu nzuri kiasi gani za nje, bado ukweli unakabi kwamba hatujapata kile tunachotaka.
Kutokupata kile ambacho mtu unataka ndiyo maumivu makubwa zaidi kwenye maisha. Na watu wamekuwa wanafanya kila namna kuhakikisha hawayasikii maumivu hayo. Usumbufu mwingi ambao watu wamekuwa wanaingia, starehe, ulevi na mengine, zote ni jitihada za kukwepa maumivu ya kutokupata unachotaka.
Cha kushangaza, dawa ya uhakika ya maumivu hayo ni moja tu, kupata unachotaka. Na ili upate unachotaka, lazima ujue nini kinakukwamisha kukipata, hasa kama umekuwa unapambana kwa muda mrefu na hupati.
Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kujifanyia tathmini sahihi ili kuona ni wapi sisi wenyewe tumekuwa tunajikwamisha kupata kile tunachotaka. Kama utajifanyia tathmini hii na kujipa majibu ya kweli, utakuwa na mengi ya kurekebisha na utakapofanya hivyo, utapata kile unachotaka.

1. Umetoa Kila Unachopaswa Kutoa Ili Upate Unachotaka?
Kila kitu kina gharama, kupata ambacho hujawahi kupata, lazima ufanye na kutoa ambacho hujawahi kutoa. Kama unaendelea kufanya yale yale ambayo umekuwa unafanya na kutoa kile kile ambacho umekuwa unatoa, usishangae unapopata matokeo yale yale ambayo umekuwa unayapata.
Jitathmini ni mambo gani ya tofauti kabisa ambayo umekuwa unayafanya kadiri muda unavyoenda. Jiangalie kwa kipindi cha nyuma na sasa, nini cha tofauti kabisa ambacho unakifanya?
Kila kitu kwenye maisha huwa kina kafara ambayo inatakiwa kutolewa ili kipatikane. Kadiri kitu kinavyokuwa kikubwa, ndivyo kafara ya kutoa inavyokuwa kubwa.
Wewe unataka mafanikio makubwa, sawa. Je ni kafara gani ambayo umeitoa? Ni vitu gani vizuri na unavyovipenda sana ambavyo umeachana navyo ili upate unachotaka?
Wengi wanaposikia kutoa kafara, wanafikiria tu mambo ya kishirikina. Lakini ukweli ni kafara haina chochote cha kufanya na ushirikina. Kutoa kafara ni kuachana na vitu vizuri na unavyovipenda, lakini vinavyokuzuia kupata mafanikio makubwa.
Inaweza kuwa ni kazi na/au biashara unazofanya sasa, ambazo zinakupa pesa ya kuendesha maisha, lakini hupati pesa ya kujenga mafanikio makubwa unayoyataka. Inaweza kuwa ni aina ya mahusiano uliyonayo, ya watu ambao unawapenda na kuwakubali sana, lakini wanakuwa kikwazo kwako kujitoa kikamilifu kufanikiwa.
Kama hujaacha kitu ambacho kinakuumiza kweli kweli, hujayataka kweli mafanikio makubwa unayoyataka. Unaweza kusema sababu nyingi za kwa nini unashindwa, lakini maandisho ni makubwa na yapo wazi kwamba hujatoa kile unachopaswa kutoa ili upate unachotaka kupata.
Unapojifanyia tathmini na kugundua hujaweka kile unachopaswa kuweka, usijicheleweshe, anza mara moja kuweka kila kinachohitajika. Hivyo ndivyo unaweza kubadili matokeo unayopata.
2. Umepambania Kitu Hicho Kwa Muda Mrefu Kiasi Gani?
Tatizo moja kubwa sana kwenye safari ya mafanikio ni kuiga majibu kwenye mitihani ambayo ni tofauti. Yaani mafanikio ni kama watu tupo kwenye chumba kimoja cha mtihani, ila kila mtu ana maswali yake. Unapoiga majibu ya mwingine, unaishia kufeli, kwa sababu maswali hayafanani.
Mara nyingi sana watu wanapoingia kwenye kufanya kitu, iwe ni kazi au biashara, wanajilinganisha na watu ambao siyo sahihi kwao. Mtu ndiyo kwanza anaanza, anajilinganisha na watu ambao wamekuwa kwenye kitu hicho kwa muda mrefu kuliko wao.
Hata kama unaona watu wanavyofanya kitu wamekosea, aliyekutangulia amekutangulia tu. Huwezi kuwa kama yeye, hasa kipindi cha mwanzo. Una mengi ambayo unapaswa kuwathibitishia watu ndiyo waweze kukuamini.
Hivyo unapoona unaweka juhudi lakini matokeo huyaoni, jitathmini una muda mrefu kiasi gani kwenye kitu hicho unachofanya. Kama hujaweka muda mrefu, huenda una haraka kuliko uhalisia unavyotaka.
Warren Buffet amewahi kusema huwezi kugawa ujauzito mmoja kwa wanawake tisa halafu ukapata mtoto ndani ya mwezi mmoja. Vitu vinahitaji muda wa kujengeka ndiyo matokeo yake yaweze kuonekana.
Maendeleo makubwa ya teknolojia na uharaka wa mambo kutokea yametufanya tusahau kabisa kwamba vitu vinahitaji muda na pia tukose uvumilivu pale vitu vinapochukua muda.
Hili ni jambo la kujikumbusha kila unapofika hatua ya kutaka kukata tamaa kwa kuweka juhudi lakini matokeo yasionekane.
Lakini pia haipaswi kuwa sehemu ya kujifariji, kwa kuona unahitaji kuweka muda, huku ukirudia kufanya yale yale. Ni lazima uendelee kufanya kwa ubora na kwa hatua za juu zaidi wakati unaendelea kusubiri muda sahihi wa kupata matokeo.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK118; Jifanyie Tathmini Hii Ili Uone Ni Wapi Unajikwamisha Mwenyewe Kufanikiwa