Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kwenye kila eneo, huwa ni watu wachache sana wanaopata mafanikio makubwa, licha ya wengi kuwa wanayataka mafanikio hayo. Na katika hao wachache wanaoyapata mafanikio makubwa, ni wachache zaidi wanaoweza kudumu na mafanikio hayo kwa muda mrefu. Na katika hao wachache wanaodumu na mafanikio, ni wachache mno ambao mafanikio yao yanaweza kuendelea kuwepo hata baada ya wao kuwa hawapo tena.
Ni kitu ambacho kipo wazi kabisa na tumekuwa tunakiona kwenye safari ya wengi. Unakuta mtu anaanzia chini kabisa, anapambana sana kufanikiwa na mapambano hayo yanamwezesha kupiga hatua. Kwa kuwa amepiga hatua, anaona hahitaji tena kufanya yale yaliyomfikisha kwenye mafanikio anayokuwa ameyapata. Na hapo ndipo anguko kubwa linapotokea na mtu kujikuta amepoteza kila alichopata.
Kila anayeanzia chini na akawa tayari kuweka juhudi kubwa kwenye kitu anachokuwa amechagua, lazima atapiga hatua fulani. Hatua anazopiga zinaweza kumshawishi kwamba hahitaji kuendelea kuweka juhudi alizokuwa anaweka. Na ni kweli kabisa kwamba mafanikio yanakosa maana kama mtu bado utalazimika kuendelea kuteseka ndiyo ubaki kwenye mafanikio ambayo umeyapata.
Kinachofanya mafanikio ya watu kuanguka pale wanapoacha kufanya kile kilichowapa mafanikio siyo kwa sababu mafanikio wanayokuwa wameyapata hayana nguvu, bali jinsi wanavyokuwa wameyapata ndiyo inakuwa tatizo.
Watu wengi wanapata mafanikio yao kwa kufanya, hivyo ili mafanikio hayo yadumu, ni lazima waendelee kufanya. Wao wanakuwa hawajui hilo, ndiyo maana wanashawishika kuacha kufanya na hilo kupelekea anguko lao.
Mafanikio yanayodumu kwa muda mrefu na hata kuendelea baada ya mtu kuwa ameondoka ni yanayotokana na kujenga. Kitu kinapojengwa, kinaweza kuendelea kusimama chenyewe bila kutegemea uwepo wa yule aliyekijenga.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza jinsi ya kupata mafanikio yatakayodumu kupitia kujenga na siyo kufanya. Kupitia barua hii utaona ni wapi umekuwa unakosea na kujikuta kwenye gereza la kulazimika kufanya ndiyo mambo yaweze kutokea.

1. Kufanya Ni Rahisi, Kujenga Ni Kugumu.
Kufanya biashara ni rahisi, nunua au zalisha kwa bei ndogo, kisha uza kwa bei kubwa na upate faida. Kila mtu anaweza kufanya hilo kwa ngazi anayokuwa amechagua.
Kujenga biashara ambayo inaweza kununua au kuzalisha kwa bei ndogo, kisha kuuza kwa bei kubwa na kupata faida bila kukutegemea wewe moja kwa moja ni kitu kigumu.
Watu huwa wanakimbilia kufanya mambo rahisi, kwa sababu yanawapa matokeo ya haraka, lakini matokeo hayo huwa hayadumu. Imekuwa inaonekana ni kama ujanja pale mtu anapoweza kupata matokeo makubwa kwa urahisi, kitu ambacho hakipo.
Ambacho watu wanapaswa kukubali ni kuyaendea mambo magumu, ambayo yana fursa ya kutoa matokeo yatakayodumu kwa muda mrefu. Hakuna juhudi zinazowekwa na zikawa zimepotea bure. Kila kinachofanyika ni uwekezaji ambao baadaye utakuwa na marejesho mazuri.
Kila unapojikuta njia panda, na mbele yako kukawa na njia mbili, moja rahisi na nyingine ngumu, mara zote chagua njia iliyo ngumu. Najua hilo ni kinyume kabisa na vile ambavyo wengi wanafikiri, lakini ndiyo kitu kitakacholeta mafanikio makubwa tunayoyataka.
Hatua ya kwanza ya kupata mafanikio ni kuepuka mambo ambayo wengi wanapenda kuyafanya. Na mambo ambayo wengi wanapenda kuyafanya ni ambayo ni rahisi kufanya.
2. Mafanikio Yako Yanategemea Vikubwa Na Vizuri Unavyojenga.
Watu huwa wanashindwa kuyaelewa mafanikio, hasa wanapoangalia watu wanaoonekana kuweka juhudi kubwa sana lakini hawapati mafanikio kama wanaoonekana kuweka juhudi ambazo siyo kubwa.
Ambacho hawaelewi ni kwamba mafanikio hayategemei juhudi pekee. Mafanikio yanategemea kile ambacho mtu anajenga na kina thamani kiasi gani kwa watu wengine. Hatulipwi kwa mateso tunayopata pekee, bali tunalipwa kwa kile tunachojenga kwa mateso hayo.
Watu wengi wanateseka, lakini ni mateso yanayopotea kwa sababu hayajengi kitu chochote. Yanakuwa ni mateso ya kufanya, ambayo yanapita bila kuacha alama yoyote.
Mafanikio yetu yanategemea kwenye kujenga, lakini siyo kila kinachojengwa kinaweza kuchangia kwenye mafanikio. Kujenga kunakoleta mafanikio ni kule kwenye sifa mbili.
Sifa ya kwanza ni kitu kinachojengwa kinapokuwa kikubwa. Hakuna mafanikio makubwa yanayotokana na vitu vidogo. Ni lazima kitu kinachojengwa kiwe kikubwa na kiguse wengi kwa kuwapa thamani. Hata kama kitu kitaanza kwa udogo, lazima kiwe na nafasi ya kukua na kiweze kukuzwa.
Watu wengi wamejikwamisha kwa kufikiri kwa udogo sana, na hivyo kuishia kujenga vitu ambavyo vina ukomo kwenye ukuaji. Wengi wanajenga vitu vinavyowategemea wao, kitu ambacho kinakuwa na ukomo kwenye ukuaji.
Sifa ya pili ni kitu kinachojengwa kinapaswa kuwa kizuri. Ukubwa pekee hautoshi kuleta mafanikio makubwa, uzuri pia unahitajika. Kwa bahati mbaya sana, vitu vingi huwa ni vizuri vinapokuwa vidogo, lakini vikikua vinakuwa vibaya. Mafanikio makubwa na ya kudumu ni yale yanayotokana na vitu vikubwa ambavyo pia ni vizuri.
Hapa uzuri haimaanishi mwonekano pekee, bali manufaa na thamani ambayo inapatikana kwenye kitu husika. Lengo hasa la kujenga kitu ni kiweze kuwa na manufaa kwa watu wengine. Kitu chenye manufaa ndiyo kitu kizuri. Kitu kinapokosa manufaa au kikawa na ugumu kwenye kupata manufaa hayo kinakuwa siyo kizuri.
Ni muhimu sana unapokuwa unakazana kujenga, kuhakikisha unaendelea kutunza uzuri ambao unafanya kitu kiwe na thamani kubwa kwa wale wanaolengwa.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK119; Kila Mtu Anaweza Kufanya, Wachache Sana Wanaweza Kujenga, Kuwa Mmoja Wa Hao Wachache