Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Watu wanaoanzia chini kabisa na kufanikiwa, huwa wanasifiwa kama watu waliojenga mafanikio yao wao wenyewe, yaani self made. Lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu anayeweza kujenga mafanikio yake yeye mwenyewe.
Japokuwa mtu atapambana sana ili kufanikiwa, bado anawahitaji watu wengine ndiyo aweze kuyapata mafanikio anayoyataka. Kwa sababu wengi wanakuwa hawahusiki moja kwa moja kwenye mafanikio ya mtu, ndiyo inapelekea kuonekana watu wamejijenga wenyewe kimafanikio.
Unahitaji watu wa kila aina ili uweze kupata mafanikio makubwa unayoyataka. Na siyo tu watu wanaokubaliana na wewe, bali hata watu ambao wanakukwamisha kufanikiwa. Japo unaweza kuona watu hao wanayakwamisha mafanikio yako, wanaweza kuwa ndiyo watu wanaosababisha upate mafanikio makubwa zaidi.
Kushindwa kutambua mchango wa watu kwenye safari yetu ya mafanikio imekuwa moja ya sababu za watu kutokufanikiwa. Wengi wamekuwa wanakazana kuiga na kufurahisha wengine na hilo kuwapelekea kushindwa kufanya vitu vya tofauti na vitakavyowapa mafanikio wanayoyataka.
Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kuangalia jinsi ambavyo marafiki na maadui walivyo muhimu kwenye safari yako ya mafanikio. Utajifunza jinsi ya kuwatumia watu wa aina zote kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

1. Unahitaji Marafiki Ili Ufanikiwe
Marafiki ni watu wanaokubaliana na wewe, watu wanaokutakia mema na wanaokuunga mkono kwenye kupata kile unachotaka. Hawa ndiyo tunaowapenda, kwa sababu wanaendana na sisi na wanaonekana kuwa na mchango kwenye mafanikio tunayoyataka.
Marafiki wanaweza kutupa ushauri mzuri na wanaweza kuwa mfano pia kwenye kile ambacho tunakitaka. Ni wazuri kwenye kututia moyo kwenye safari tunayokuwa tumeichagua, ambayo siyo rahisi.
Marafiki pia wanaweza kutupa rasilimali mbalimbali tunazohitaji kwenye safari ya mafanikio. Inaweza kuwa watu, fedha, mali na vitu vingine tunavyokuwa tunavihitaji ili tupige hatua.
Pamoja na mchango huu mkubwa wa marafiki kwenye safari yetu ya mafanikio, wanakuwa na mchango kwetu kupata mafanikio kwa kiwango cha kawaida. Ni vigumu sana kwa marafiki kukusaidia kupata mafanikio kwa kiwango kikubwa sana.
Sababu kubwa inayopelekea marafiki wasiweze kutusaidia kupata mafanikio makubwa ni wao kutufikisha kwenye hatua ya kuridhika. Tunapokuwa tunaanzia chini kabisa, marafiki wanatusaidia kupambana ili kutoka chini. Tunapoanza kupata mafanikio na kuridhika, marafiki hawawezi kutusukuma zaidi ya hapo. Hivyo kuridhika kwetu na mafanikio madogo kunatuzuia kupata mafanikio makubwa.
Lakini pia marafiki hawawezi kutusaidia kupata mafanikio makubwa kuliko ambayo wao wamepata. Mara nyingi huwa tunaishia kuwa na mafanikio ambayo ni wastani wa watu wanaotuzunguka. Hivyo ukijaribu kwenda juu zaidi ya marafiki wanaokuzunguka, unarudi kwenye kiwango ambacho wao ndiyo wapo.
Ni muhimu sana kuwa na marafiki kwenye safari ya mafanikio, kwa sababu watakuwezesha kutoka chini na kwenda juu. Ila unapotaka kwenda juu zaidi, marafiki pekee hawatoshi, unahitaji maadui pia.
2. Unahitaji Maadui Ili Ufanikiwe Zaidi
Maadui ni watu ambao hawakubaliani na sisi, watu wanaotaka kutunyang’anya kile tulichonacho. Maadui wanakuwa wanatupinga wazi wazi au kutukwamisha tusipate kile tunachotaka.
Huwa tunawachukia maadui, kwa kuwaona kama kikwazo kwetu kupata mafanikio makubwa. Lakini tunapowaangalia maadui kwa ndani, tunaona fursa ya kuwatumia kupata mafanikio makubwa zaidi.
Maadui wanakupa kitu cha kupambania, ambapo usipopambana, unakosa unachotaka na/au kupoteza ulichonacho. Maadui hawana huruma na wewe, wanapambana kukutoa pale ulipo au kukuzuia usifike kule unakokwenda.
Maadui wanakuwezesha kupata mafanikio makubwa zaidi kwa sababu wanakupa hasira. Na hasira unayoipata inakusukuma kufanya kwa ukubwa zaidi na kutokuridhika na chochote unachokuwa umepata.
Kwa sababu kadiri unavyopambana kufanikiwa ndivyo pia maadui nao wanapambana kukuangusha, unapata msukumo wa kufanya zaidi. Kwa sababu kila mafanikio unayopata maadui wanataka kuyaangusha, huwezi kuridhika na kuacha kupambana.
Maadui wanakuweka macho muda wote, wanakufanya uwe kwenye hali ya mapambano muda wote. Na hiyo ndiyo hali inayohitajika kwenye kujenga na kudumisha mafanikio makubwa kwenye maisha.
Kwa mchango huu wa maadui kwenye mafanikio makubwa, hupaswi kuhofia pale maadui wanapojitokeza. Badala yake unapaswa kufurahia, kwani watakusukuma ufanye makubwa zaidi.
Kama binadamu huwa hatupendi magumu na changamoto, ndiyo maana hatupendi maadui. Lakini bila ugumu na changamoto hatuwezi kukua. Hivyo tunawahitaji sana maadui ili tuweze kukua.
Usihofie pale unapopambana kupata mafanikio makubwa halafu watu wanajitokeza kukukwamisha. Badala yake furahia, kwa sababu watu hao ndiyo watakusukuma ufanye makubwa zaidi ili usiweze kukwamishwa na yeyote. Kwa kufanya makubwa zaidi, unajenga mafanikio makubwa ambayo peke yako usingeweza kuyapata.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK122; Marafiki Watakupa Mafanikio, Maadui Watakupa Mafanikio Makubwa Zaidi