Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kujenga biashara yenye mafanikio, na inayoweza kujiendesha bila kukutegemea siyo jukumu jepesi. Ni kitu kinachohitaji kazi, muda na watu sahihi ndiyo kiweze kutokea.
Kuja na wazo la biashara siyo kitu kigumu, ni rahisi hata kuiga mawazo ya watu wengine. Na kuifanya biashara yenyewe pia inaweza isiwe kazi ngumu, hasa pale inapokuwa kwa ngazi ndogo.
Ni kujenga na kukuza biashara ndiyo kunahitaji kazi kubwa na ambayo wengi huwa wanashindwa kuifanya.
Pamoja na mengine mengi yanayohitajika kwenye kujenga biashara, watu sahihi, hasa ambao ni wataalamu wanahitajika sana. Na biashara nyingi zimeshindwa kukua kwa sababu zinakosa watu hao sahihi watakaoziwezesha kukua.
Unaweza kudhani biashara ikiwa na watu sahihi, ambao ni wataalamu kwenye maeneo yao ndiyo itakuwa na uhakika wa kufanikiwa. Lakini historia inaonyesha biashara nyingi zimeshindwa licha ya kuwa na wataalamu sahihi.
Tena zipo biashara ambazo zimeshindwa kwa sababu ya uwepo wa wataalamu. Na hilo limekuwa linatokana na viongozi wa biashara hizo kushindwa kujua wapi matumizi ya wataalamu kwenye biashara yanapopaswa kuishia.
Kwa kuwa moja ya madhumuni ya #BaruaZaKocha ni kujenga biashara zenye mafanikio na zinazoweza kujiendesha bila kutegemea waanzilishi, hapa tunaenda kujifunza matumizi sahihi ya wataalamu kwenye biashara.

1. Biashara Zinaanzishwa Na ‘Wahuni’ Na Kukuzwa Na Wataalamu
Kumekuwa na mafunzo na mifano mingi inayoonyesha tofauti ya wanaosoma na kufaulu sana na wale wasiosoma sana au wasiofaulu. Takwimu zinaonyesha biashara nyingi zimekuwa zinaanzishwa na watu ambao hawakupata elimu kubwa sana au kama walipata elimu basi hawakuwa na ufaulu mzuri.
Nimekuwa nasema biashara huwa zinaanzishwa na ‘wahuni’ na kukuzwa na wataalamu. Inahitaji ujasiri mkubwa sana kuanza biashara, na mara nyingi kushindwa kuona hatari zinazokuwepo kwenye kuanza biashara. Kusoma kwingi kunaondoa huo ujasiri kwa kuwafanya watu wazione hatari za kuanzisha biashara.
Lawama ambazo zimekuwa zinatolewa kwa wasomi ambao wanakosa kazi na kushindwa kuanzisha biashara au wanakuwa kwenye ajira na kushindwa kuanzisha biashara, ni kuwaonea tu. Hawana ‘uhuni’ wa kuwatosha kuanzisha biashara. Na hata wanapoanza biashara, hawana ‘uhuni’ wa kutosha kuzisukuma zikue.
Pamoja na kuhitajika kwa ‘uhuni’ kwenye kuanza biashara, haziwezi kupata ukuaji mkubwa kama zitabaki kwenye hali hiyo. ‘Uhuni’ unawezekana mwanzo na hatua za chini, lakini kama biashara inahitaji kukua, lazima iwe na wataalamu.
Ninaposema ‘uhuni’ simaanishi kitu chochote kibaya, bali ule ujasiri wa kuanza kitu bila kujua hatari na madhara yake. Kufanya kitu ambacho kina hatari kubwa, lakini mtu anafanya kwa kutokujua.
Kwenye biashara, ‘uhuni’ ni mtu kuingia kwenye biashara bila kukaa chini na kuandika mpango wa biashara uliokamilika, bila kufanya utafiti wa soko na bila kuzingatia sheria za biashara na kodi. Biashara nyingi zinaanza katika hali hiyo mwanzoni.
Lakini ili biashara ikue, ili iweze kuaminika na watu, lazima ifanye mambo sahihi ya kibiashara. Biashara inapotaka mkopo benki itahitajika kuwa na mpango wa biashara na kuwa na nyaraka mbalimbali za kuonyesha biashara imerasimishwa.
Ili biashara iweze kukamilisha mahitaji yote yanayohitajika kwenye kuziendesha kwa usahihi, wataalamu wengi wanahitajika. Hapo ndipo biashara inapopaswa kuhakikisha inao hao wataalamu na kuwatumia vizuri.
2. Wataalamu Wanaohitajika Kwenye Ukuaji Wa Biashara
Unapoanza biashara, wewe mwenyewe ndiye unayekuwa kila kitu kwenye biashara. Unafanya majukumu mengi, kama siyo yote kwenye biashara hiyo. Na unapoelemewa na majukumu, unaanza kuajiri watu wa kukusaidia kuyatekeleza. Wengi unaowaajiri mwanzo wanakuwa siyo wataalamu, bali watu wanaoweza kutekeleza majukumu unayowapa.
Ni katika kuikuza biashara zaidi ndiyo unahitaji wataalamu wafuatao;
Unahitaji wahasibu kwa ajili ya kusimamia fedha za biashara na kuzingatia mambo ya kodi. Katika wataalamu wengi wanaohitajika kwenye biashara, wahasibu ni kipaumbele cha kwanza, kwa sababu eneo la fedha ndiyo eneo nyeti zaidi. Usimamizi wa fedha za biashara ni tofauti kabisa na fedha binafsi, hivyo bila wataalamu unaweza kujikuta unafanya makosa ambayo yatakugharimu sana kadiri biashara inavyokua.
Unahitaji wanasheria kwa ajili ya kusimamia uzingatiaji wa sheria na taratibu mbalimbali za kuendesha biashara. Kuna sheria nyingi ambazo kila biashara inapaswa kuzizingatia ili iwe salama, sheria ambazo waanzilishi wengi hawazijui. Na pale biashara inapoajiri, kuna sheria na taratibu mbalimbali za kukaa na wafanyakazi kwenye biashara.
Kwa nafasi za wataalamu hao wawili, unaweza usiajiri moja kwa moja, badala yake ukawa na watu ambao wanakupa huduma hizo kwa makubaliano maalumu. Na kwa biashara ambayo bado haijapata ukuaji mkubwa, haihitaji kuingia gharama kubwa kuajiri wataalamu hao. Badala yake inapaswa kuhakikisha inao wataalamu hao na kuwatumia pale inapohitajika.
Wataalamu wengine ambao biashara itaendelea kuwa nao kadiri inavyokuwa ni watendaji ambao wana uzoefu kwenye maeneo yao. Mwanzo biashara inaajiri watu wanaopatikana na wanaoweza kulipwa kidogo. Lakini ili ikue, lazima iajiri watu wenye uwezo na uzoefu mkubwa, ambao malipo yao yatakuwa makubwa pia.
Kuna utaalamu mpaka kwenye uongozi wa biashara. Mara nyingi mwanzilishi wa biashara anajikuta akiwa ndiye kiongozi, kwa sababu tu ameanzisha. Lakini siyo mara zote anaweza kuwa kiongozi sahihi. Hivyo inafika hatua ambapo biashara inahitaji kuwa na viongozi ambao ni wataalamu. Hapa nazungumzia mameneja na wasimamizi ambao ni wataalamu waliobobea kwenye hayo.
Ili biashara ikue, lazima iendelee kupata wataalamu kwenye maeneo mbalimbali yenye uhitaji. Kutegemea mwanzilishi pekee, au watu walioajiriwa mwanzo kwa urahisi wa kupatikana hakuwezi kuipa biashara ukuaji mkubwa unaoweza kupatikana.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK123; Mafanikio Ya Biashara Yanahitaji Hawa Wataalamu, Lakini Haipaswi Kuchukua Ushauri Wao Kuhusu Biashara