INATOSHA SASA, ANZA VITENDO

  Nakumbuka kipindi nakua hakuna jambo lililokuwa la fahari kama kuendesha baiskeli. Kila mtu kwa wakati ule alikuwa na shauku kubwa ya kujua jinsi ya kuendesha baiskel na kutoweza ulikuwa unanekana mshamba. Hapo hata baiskeli huna hivyo ni kuomba ama kukodi kwa fedha kidogo. Sheria moja ya kujifunza baiskeli ni huwezi kujua kuiendesha bila ya kuanguka na hata kuumia mara kadhaa. Pamoja na kuumia lakini hatukuacha kujifunza kwa maana tulikuwa na shauku kubwa ya kujua kuendesha baiskel. Hakuna mtu anaeweza kuanza kuendesha baiskeli siku ya kwanza na akawa mtaalamu hapo hapo. Lazima uyumbeyumbe na kuanguka mara kadhaa ndipo uweze kuimudu. Wakati mwingine inabidi ushikiliwe na mtu ili uweze kupata ‘balance’. Na uzuri mmoja ni huwezi kujua kuendesha baiskeli bila ya kuiendesha. Hata ukisoma kiasi gani na ukaangalia video za mafunzo ya baiskeli mara ngapi lazima uende nje ukaumie ndio ujue kuendesha baiskeli.

  Maisha yetu ya kila siku hayana tofauti na kujifunza kuendesha baiskeli, katika jambo lolote tunalotaka kufanya kwenye maisha mfumo wake ni sawa na kujifunza baiskeli. Jambo lolote kubwa unalotaka kufanya kwenye maisha mwanzo wake huwa ni mgumu, utayumba sana na kuanguka hapa na pale. Unaweza kuwa na maandalizi ya kutosha, umejifunza vyote vinavyohusika ila siku utakapoanza kufanya jambo lenyewe kuna changamoto nyingi zitakazoibuka ambazo zitakuyumbisha na nyingine zitakuangusha. Hivyo kwa lolote unalokwenda kufanya jambo la kwanza kujipanga ni jinsi ya kuzikabili changamoto. Watu wengi wanakuwa na mipango ya kufanya jambo fulani ila wanapokutana na changamoto wanashindwa kuendelea, sababu kubwa ni kwa sababu hawakuweka mpango wa kukabiliana na changamoto.

  Kwa kuona wengine wanavyopitia changamoto, wengi husita kuanza na kusema wanajiandaa zaidi, ama wanajipanga zaidi. Hivyo mtu anaahirisha kufanya jambo kwa wakati huo kwa sababu tu anahisi hana maandalizi ya kutosha hivyo anaendelea na maandalizi na kuahirisha kuanza. Ukweli ni kwamba hata ukijiandaa kwa miaka kumi bado siku utakayoanza utakutana na changamoto.

  Naomba nisieleweke vibaya, sisemi upate tu wazo halafu ukurupuke na kuanza kufanya kwa sababu tu hata ukijiandaa vipi bado utakutana na changamoto. Kama umepata wazo ama una ndoto yako, usome mchezo, elewa kila unachotakiwa kuwa nacho ama kufanya ili kufikia malengo yako, elewa changamoto utakazokutana nazo na njia ya kukabiliana nazo, anza mara moja. Ukitaka kusubiri mpaka uwe mtaalamu wa kitu ambacho hujakianza itakuchukua maisha yako yote. Anza sasa, fanya chochote ambacho kitakupeleka unakotaka kuelekea.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: