Kwa Nini Siwezi Kujiunga Na Telexfree.

Mwishoni mwa mwaka jana (2013) bwana mmoja aliwasiliana na mimi kupitia Facebook na kuniambia kuna biashara mpya imeingia mjini(akimaanisha Tanzania), hakunieleza kwa undani sana ila aliniambia ni ya njia ya mtandao na unapata fedha kwa kufanya kazi kidogo. Baada ya kuniambia tu hivyo hata sikutaka kuendelea kuuliza maana kumekuwa na upotoshwaji mkubwa sana juu ya kutengeneza fedha kwenye mtandao(soma; kabla hujaanza kutengeneza pesa kwenye mtandao soma hapa), makala hiyo niliiandika mwezi wa nane mwaka jana ambapo kulikuwa kumeshamiri sana wimbi la taarifa za kutengeneza fedha kirahisi kupitia mtandao.

Mwanzoni mwa mwaka huu(2014) rafiki yangu ambae nimewahi kufanya nae biashara ya mtandao(network marketing) alinitafuta na kuniambia kuna fursa mpya imeingia mjini. Alinieleza fursa hiyo na nilipatwa na shauku kubwa sana ya kutaka kuingia kwenye fursa hiyo, lakini baadae niliamua kutoingia(kwa sababu ambazo nitakueleza baadae kidogo).

Baada ya kusahau kabisa kuhusu fursa hii, hivi majuzi kuna mtu mwingine kutoka kwenye mtandao wangu amenishirikisha fursa hii na kuniambia jinsi ilivyo nzuri na yenye faida. Nilimpa sababu zangu za kutoingia kwenye fursa hiyo, ila sina hakika kama alinielewa au aliona sijaiona fursa.

Fursa hiyo ni ipi?

Fursa ambayo nimekuwa nikipewa na watu hawa ni kampuni inayoitwa TELEXFREE. Kulingana na maelezo kampuni hii inajihusisha na matangazo ya kwenye mitandao na kuuza bidhaa ya mawasiliano inayoitwa VOIP. Kampuni hiyo kwa sasa inafanya biashara kwa mfumo wa mtandao(network marketing/ multilevel marketing).

telexfree

Nilipopewa maelezo kuhusiana na kampuni hii nilipata shauku kubwa ya kutaka kujiunga nayo. Ila kabla ya kufanya hivyo ilibidi nifanye uchunguzi wangu kabla ya kuingia. Pia nilipata nafasi ya kuhudhuria semina zao na kuuliza baadhi ya maswali.

Fursa ya kampuni hii ni kwamba unaweza kujiunga kwa dola 400/1500/16000 kwa mwaka na kila wiki wakakulipa dola 20/100/1100 kwa kuweka matangazo ambayo itakuchukua kama dakika tano tu. Kwa nilivyoziandika hizo namba kama utajiunga kwa kulipa dola 400 kwa mwaka kila wiki utalipwa dola 20 hivyo kwa wiki 52 kwa mwaka unapata dola 1040, faida zaidi ya mara mbili. Pia kuna upande wa pili wa biashara ambapo watu wakiingia kupitia wewe unaendelea kupata kipato kikubwa.(nimeeleza kwa kifupi ili nisikutese na hizi namba).

Kwa nini nimeamua kutochangamkia fursa hii?

Pamoja na fursa hii kuonekana nzuri hivi na yenye faida kubwa niliamua kwa roho moja kutojihusisha nayo. Ningeweza kujiunga siku hiyo hiyo kwa dola 400, maana nilikuwa nazo ila sikufanya hivyo. Kuna sababu kuu nne ambazo zimenifanya nisijiunge na biashara hiyo.

1. Kampuni hii inahusishwa mchezo wa upatu.

Ukitafuta taarifa za kampuni hii kwenye mitandao sehemu nyingi wanaihusisha na michezo ya upatu ambapo kuna watu wachache wanafaidika na mwishowe wengi wanapata hasara. Kwa maelezo ya kampuni hii wanakataa kuhusika na upatu na wanatoa sababu za msingi sana. Tatizo langu linakuja kwamba kuna kampuni nyingi duniani zinazofanya biashara ya mtandao lakini hazijawahi kuhusishwa na upatu kwa kiwango kikubwa kama inavyohusishwa kampuni hii.

2. Haijafikia vigezo vyangu vya kufanya biashara.

Pamoja na kwamba nafanya biashara nipate fedha ila nina viwango vyangu vya kuingia kwenye biashara yoyote. Ili nifanye biashara ni lazima bidhaa ama huduma ninayouza iwe na msaada kwa mtu anayeitumia, kinyume na hapo siwezi kufanya biashara hiyo. Sasa kwa kampuni hii ya Telexfree bidhaa inayouzwa kwanza haina watumiaji hapa Tanzania na hata duniani kuna bidhaa nyingi za bure ambazo zinafanya kazi sawa na hiyo bidhaa yao(VOIP). Pia kazi ya kuweka matangazo hujui ni tangazo la nini unaweka na huko unakokwenda kuweka hujui kunahusiana na nini. Vipi kama unatangaza vitu ambavyo vinakwenda kinyume na imani au utamaduni wako?

3. Fedha inayopatikana haiendani na kazi unayoifanya.

Mimi ni muumini mzuri wa kwamba HAKUNA KITU CHA BURE(there is no free lunch). Naamini kwamba ili upate fedha ni lazima ufanye kazi yenye maana kwa watu wengine, kinyume na hapo ni wizi au utapeli. Ukiangalia fedha ambazo unapata kwenye fursa hii ni nyingi sana ukilinganisha na kazi unayoifanya. Japo kwenye maelezo yao wanasema Watanzania tumezoea kazi ngumu ndio maana tukiona kazi rahisi tunaogopa, mimi najua tokea kuundwa kwa misingi ya dunia haijawahi kutokea fedha ikapatikana kirahisi kwa njia za halali. Maendeleo ya kweli yanapatikana kwa kufanya kazi yenye maana kama uzalishaji wa bidhaa zinazotumiwa na watu au huduma zinazowasaidia watu kuboresha maisha yao. Kitu hiki sikioni kwenye kampuni hii ya Telexfree.

4. Najali sana haiba, utu na heshima yangu.

Naheshimu sana wale ambao wananiheshimu na kuniamini. Siwezi kuvunja heshima au imani yangu kwa sababu ya kuangalia fedha tu. Kwa mfano wewe msomaji wangu umekuwa ukisoma makala na mafundisho ninayotoa mara kwa mara. Kama unafuatilia kwa muda mrefu ina maana tayari una imani na mimi, hivyo nikikushawishi kwamba ingia kwenye biashara hii inalipa ukaingia na baadae ikagundulika kwamba biashara hiyo ni utapeli utaendelea kuniamini? Utasoma tena chochote nitakachoandika au kufundisha? Nina malengo makubwa sana kwa ninachofanya na siwezi kupoteza malengo hayo kwa kukimbilia fedha za haraka.

Hayo ndiyo maoni yangu kuhusiana na kampuni hii ya TelexFree, kama ni woga wangu kama wanavyosema wanaoifanya, nimekubaliana na hilo. Kama ni fursa ya kweli sitojutia kuiacha kwa kuwa nimeamua kwa moyo mmoja kutokujihusisha nayo. Naamini kuna fursa nyingi sana zinapatikana na nyingine nyingi tayari nimeshazifaidi.

Ufanye nini?

Huenda na wewe umeshasikia kuhusu biashara hii au huenda umeshaianza. Unajiuliza uifanye au uachane nayo? Unataka ushauri wangu kuhusiana na biashara hii?

Kama unataka ushauri wangu rudia tena kusoma hayo maelezo hapo juu kisha tafuta taarifa nyingine kwenye vyanzo vingine halafu ufanye maamuzi kulingana na malengo na mipango yako na pia vigezo vyako.

Kwa upande wangu siwezi kujiunga kwa sababu inaweza kuniharibia malengo yangu makubwa niliyo nayo na pia haijafikia vigezo vyangu vya kibiashara.

Nakutakia kila la kheri kwenye harakati zako za kuboresha maisha yako.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: