Ninaposema moja ya malengo yangu kwenye maisha ni kuwa Bilionea kuna watu wengi sana wananipinga. Wengi wananiambia haiwezekani kwa mazingira yetu ya kitanzania labda niwe Fisadi. Nafurahi sana watu wanaponipinga hivi kwani kunipinga kwao kunanidhihirishia ni jinsi gani nahitajika kuendelea na malengo yangu ili kufikia Ubilionea.
Wengine wanafikiri kuwa bilionea ni kama dhambi. Kwamba itabidi uwadhulumu wengine na wanatumia kauli moja kwamba tamaa ya fedha ndio chanzo cha maovu. Haya yote ni mawazo ya kimasikini na yanatokana na kutojua ni kitu gani kinahitajika kufanya ili kuwa bilionea.
Kama na wewe una mawazo haya ya kimasikini naomba niyaondoe kwa kukupa mpango wa kuelekea kwenye Ubilionea. Sio kitu rahisi ila pia sio kwamba haiwezekani.
Kama unataka kuwa bilionea fanya mambo haya saba muhimu;
1. Amua kuwa Bilionea.
Kila kitu kwenye maisha kinaanza na maamuzi. Uko hapo ulipo na jinsi ulivyo kutokana na maamuzi uliyofanya siku za nyuma. Na ili uwe bilionea ni lazima ufanye maamuzi ya kuwa bilionea. Ubilionea hauji kama ajali, ni lazima ufanye maamuzi kisha uwe na malengo na mipango ya kufikia maamuzi hayo.
2. Achana na mawazo ya kimasikini.
Hakuna kitu kinachowarudisha nyuma watu kama mawazo ya kimasikini. Mawazo kama, fedha sio kila kitu, fedha haiwezi kuleta furaha, au fedha ndio chanzo cha maovu ni mawazo ambayo yanakuzuia wewe kutengeneza fedha nyingi na kuwa bilionea. Ni kweli fedha sio kila kitu ila itakuwezesha kupata mahitaji muhimu kwenye maisha yako. Ni kweli fedha haiwezi kuleta furaha ila kuwa nazo kunafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Wazo jingie kubwa la kimasikini ni kufikiri kuna upungufu wa hela duniani. Hela zipo nyingi sana ila kuna upungufu mkubwa wa watu wanaofikirir jinsi ya kuzipata hela hizo.
3. Fanya kazi kwa bidii na maarifa.
Pamoja na mipango yote kitu kimoja muhimu ni kufanya kazi. Ili uwe bilionea ni lazima ufanye kazi kwa juhudi kubwa na maarifa makubwa kuliko watu wengine wote wanavyofanya kazi zao. Kama unaona ufanyaji kazi wako au biashara zako hautofautiani na wengine nakuhakikishia hutoweza kuwa Bilionea. Fanya kazi, sio kwa nguvu, bali kwa juhudi na maarifa.
4. Kaa karibu na mabilionea.
Huwezi kuwa bilionea kama watu wanaokuzunguka sio mabilionea au hawana mawazo ya kuwa mabilionea. Kwa sababu utapokuwa nao mtazungumza mambo ambayo hayawezi kukufikisha kwenye ndoto zako na pia watakukatisha tamaa. Hivyo kama unataka kuwa bilionea hakikisha unazungukwa na mabilionea. Unajiuliza utapata wapi mabilionea wakukaa nao? Rahisi sana, soma vitabu vilivyoandikwa na mabilionea na kuelezea siri zao za mafanikio, njoo kwenye mtandao huu wa AMKA MTANZANIA ili uendelee kupata mawazo ya kufika kwenye ubilionea. Kwa mfano hivi majuzi niliwatumia wasomaji kitabu cha bilionea Richard Branson ambaye anamiliki kampuni zaidi ya 400 ambapo ameelezea siri zilizomfikisha kwenye ubilionea. Unaweza kukipata kwa kubonyeza maandishi haya.
5. Badili mpangilio wako wa matumizi ya fedha.
Uwezekano mkubwa ni kwamba mpango wako mkubwa kwenye fedha ni matumizi. Unanunua vitu vya kisasa ili uende na wakati. Hivi sivyo mabilionea wanavyofanya. Mabilionea wanawekeza fedha zao badala ya kuzipeleka kwenye matumizi yasiyo ya msingi. Anza sasa kuwekeza ili uelekee kwenye ubilionea.
6. Kuwa na vyanzo vingi vya mapato.
Kama una chanzo kimoja tu cha mapato sahau kuhusu kuwa bilionea. Kama umeajiriwa na hujaweka mpango wowote wa kuwa na vyanzo vingine vya mapato uko pabaya zaidi. Kama bado hujawa na vyanzo hivi usikate tamaa anza kufikiria ni sehemu zipi nyingine utawekeza ili kuwa bilionea.
7. Kuwa na matumizi mazuri ya muda wako.
Tofauti kubwa kati ya mabilionea na watu wengine ni kwenye matumizi ya muda. Mabilionea wanakazana kununua muda wa watu wengine wakati watu wengine wanakazana kuuza muda wao. Huwezi kuwa bilionea kwa kuuza muda wako kwa mtu mwingine. Kama hujaelewa kuuza muda ni nini ni kuajiriwa. Muda una thamani kubwa sana zaidi ya fedha. Yeyote anayenunua muda wako anapata mara tatu ya anachokulipa wewe. Kuwa na matumizi mazuri ya muda wako ili uwe bilionea.
Hakuna dhambi kwa wewe kuwa bilionea, hasa kama utapata ubilionea wako kwa njia za halali. Na hakuna cha kukuzuia wewe kuwa bilionea zaidi ya wewe mwenyewe. Twende pamoja kwenye safari hii ya kuwa mabilionea. Moja ya falsafa zangu kwenye maisha ni NJIA BORA YA KUMSAIDIA MASIKINI NI WEWE KUTOKUWA MASIKINI. Falsafa hii ina ukweli mkubwa sana, huwezi kumsaidia masikini kama na wewe ni masikini, mtaishia kudanganyana tu. Hivyo kama na wewe unapenda kuwasaidia wengine kuwa bilionea.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia ubilionea.
Kumbuka TUKO PAMOJA.
yap nice advice
LikeLike