Ushauri; Ni Jinsi Gani Unaweza Kufikia Malengo Yako Kama Una Idadi Kubwa Ya Wategemezi?

Katika utafiti mfupi uliofanyika kuwajua wasomaji wa AMKA MTANZANIA moja ya maswali ilikuwa kujua ni changamoto gani inayowazuia wengi kufikia malengo yao. Moja ya changamoto zilizotajwa na wengi ni kuwa na idadi kubwa ya wategemezi huku kipato kikiwa hakitoshi.

Katika kona hii ya USHAURI jumatatu ya leo tutazungumzia hili na kila jumatatu tutakuwa na changamoto moja tutakayoijadili.

Kwa maisha yetu ya kitanzania familia zetu zinaishi kindugu sana. Hivyo mtu mmoja anapoonekana ana mafanikio kidogo kuliko wenzake huwa ndio anakuwa tegemeo la ndugu wengine.

Wakati mwingine wategemezi hawa wanakuwa muhimu sana kama wazazi ambao walikulea na kukusomesha mpaka hapo ulipofika au watoto ambao wanakutegemea wewe moja kwa moja katika maisha yao.

Pamoja na wategemezi wako hawa kuwa wa muhimu sana, kipato unachopata nacho hakitoshi hata matumizi yako tu mwenyewe achilia mbali kwa wanaokutegemea. Hapa ndipo changamoto kubwa inapoanza na wengi kuona ndoto zao zimezima kabisa.

Badala ya kuchukulia changamoto hii kama mwisho wa malengo yako ifanye kuwa kichocheo za wewe kufikia malengo yako.

Hapa nitazungumzia mambo matano unayoweza kufanya kukabiliana na changamoto hii ya kuwa na utegemezi mkubwa na kuweza kufikia malengo uliyojiwekea .

1. Acha kulalamika kwamba wategemezi ndio wanakurudisha nyuma.

Hatua ya kwanza kabisa ni kuondoa hali ya kulalamika kuhusiana na changamoto hii. Unapolalamika unakosa nguvu ya kuchukua hatua na kuona kwamba maisha yako hayawezi kwenda tena mbele kwa sababu wanaokutegemea ni wengi na wewe kipato chako hakitoshi. Kwa kuwa na malalamiko haya huwezi kukaa chini na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hii. Kwa mfano kama una watoto wadogo wanaokutegemea, ni dhahiri kwamba wataendelea kukutegemea kwa miaka 20 ijayo, je unachagua kuendelea na malalamiko kwa miaka 20? Kwa kuchagua njia hii utaishi maisha yenye msongo wa mawazo kila siku wakati kuna njia nyingi za kutatua changamoto hii.

kitabu kava tangazo

2. Angalia uwezekano wa wategemezi wako kujishughulisha kidogo.

Kama wanaokutegemea ni watu wazima kama wazazi wako ila bado wana nguvu kidogo au wadogo zako au watoto wako ambao wanaweza kufanya shughuli ndogo ndogo weka mkakati wa kuwawezesha. Kama ni wazazi au ndugu wapo kijijini unaweza kufikiria mradi unaoweza kuwaingizia fedha kidogo na kuwapa mpango wa kuufanya huku wewe ukiwawezesha. Kwa mfano maeneo ya kijijini unaweza kuwapa mpango wa mradi wa kufuga kuku, ukawajengea miundo mbinu mizuri na kuwawekea hao kuku na pia kuwapa elimu ya kutosha kuhusiana na mradi huo. Kwa njia hii unakuwa umewasaidia kujipatia kipato chao, kujua ugumu wa kutafuta fedha na pia kuwa na nidhamu ya fedha. Hata kama una vijana wako ambao wamemaliza shule ila wako nyumbani na wanakutegemea kwa kila kitu watafutie kitu cha kufanya hata kama wataingiza fedha kidogo. Tabia moja ya kushangaza kuhusu binadamu ni kwamba mtu akijua akiwa na shida ya fedha utamsaidia hatofikiria njia nyingine ya kutatua matatizo yake ya kifedha zaidi ya wewe. Hivyo wasaidie waweze kutatua matatizo yao ya kifedha wenyewe. Kuna usemi unasema ukimpa mtu samaki kesho atataka tena umpe, ila ukimpa ndoano na kumfundisha kuvua kesho hatokuja tena kuomba samaki. Waangalie wategemezi wako na kama kuna ambao wanaweza kufanya shughuli ndogo ndogo watengenezee mradi wa shughuli hizo.

3. Jua na wewe unahitaji kutengeneza maisha yako.

Hata kama unawapenda ndugu na wazazi wako kiasi gani lazima kuwe na kiwango katika usaidizi wako. Usiwasaidie watu kwa kiwango ambacho wewe utabaki huka kitu kabisa au maisha yako yakawa magumu zaidi. Jua na wewe unahitaji kuwa na maisha na kufikia malengo yako hivyo weka kiwango maalumu cha kipato chako ambacho utatoa kwa wategemezi wako ambao sio watoto wadogo. Kama utawasaidia watu kiasi cha wewe kuwa na maisha magumu mwishowe utashindwa kuwasaidia kabisa, hivyo unahitaji kipindi ambacho ujayaimarisha maisha yako ili uweze kuwasaidia wengi zaidi. Moja ya falsafa zangu kwenye maisha ni NJIA BORA YA KUWASAIDIA MASIKINI NI WEWE KUTOKUWA MASIKINI. Hivyo kama utawasaida watu kiasi cha wewe kubaki masikini wewe utahitaji msaada zaidi ya hao unaojaribu kuwasaidia.

4. Punguza matumizi yasiyo ya msingi.

Kama wategemezi wako ni watoto ambao huna njia ya kukwepa na huwezi kuwapa mradi wa kujishughulisha basi angalia jinsi unavyoweza kupunguza gharama zako za maisha. Kitu kimoja nilichojifunza kwenye maisha ya mijini hasa kwenye matumizi, karibu kila mtu ananunua kitu ambacho sio hitaji kubwa kwenye maisha yake. Jua mahitaji ya msingi ni yapi na punguza matumizi mengine yote ambayo sio ya msingi. Fedha utakazookoa kwenye matumizi haya zitumie kukusaidia kufikia ndoto zako. Tabia ya kununua nguo, simu, gari na vingine vingi kwa sababu ya kwenda na wakati au kwa sababu wengine wanavyo ni matumizi mabovu ya fedha zako. Kuna kipindi kwenye maisha inabidi uishi kwa kugharamia matumizi ya msingi tu na usahau kuhusu starehe na anasa. Kabla hujanunua kitu jiulize nikikosa kitu hiki maisha yangu yatakuwa magumu sana?

5. Ongeza kipato chako.

Hili ndio suluhisho la msingi kwenye changamoto hii ya utegemezi hasa pale wanaokutegemea ni watoto wadogo. Kwa kuongeza kipato chako utaweza kukabiliana na changamoto ya utegemezi napia kufikia malengo yako. Najua unajiuliza utaongezaje kipato chako wakati changamoto hiyo ndio inakuzuia kufikia malengo yako ambayo ndiyo yangekuwezesha kuongeza kipato? Kuna fursa nyingi sana za kuongeza kipato zinazokuzunguka. Kwa sasa huzioni kwa sababu unalalamika sana kuhusiana na matatizo unayopata, hebu kwa mara moja acha kulalamikia matatizo na angalia ni njia gani unaweza kuzitumia kuongeza kipato chako. Kama una ndoto ya kuanzisha biashara anza kidogo, anza kwa fedha utakayookoa kwenye matumizi uliyopunguza na anza kuifanyia kazi biashara yako ikue.

Hizi ni baadhi tu ya njia ambazo unaweza kutumia kukabiliana na changamoto ya kuwa na wategemezi wengi na kipato kidogo. Changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha ndizo zinazotakiwa kutusukuma ili kufanya makubwa zaidi kwenye maisha yetu. Hivyo acha kulalamika na kutumia changamoto ya kuwa na wategemezi wengi kama sababu ya wewe kushindwa kutimiza ndoto zako.

Kama una ushauri wa njia nyingine muhimu za kukabiliana na changamoto hii ya utegemezi tafadhali tushirikishe kwenye maoni hapo chini ili tuweze kusaidiana .

Kama una changamoto inayokuzia kufikia malengo yako na ungependa kupata ushauri tafathali bonyeza maandishi haya na ujaze fomu.

Nakutakia kila la kheri katika harakati zako za kuboresha maisha yako.

Kumbuka TUKO PAMOJA.

3 thoughts on “Ushauri; Ni Jinsi Gani Unaweza Kufikia Malengo Yako Kama Una Idadi Kubwa Ya Wategemezi?

 1. Mwalimu Jennifer May 6, 2014 / 5:23 am

  Engine wanajitengenezea au kuwaalika wategemezi iliwapate sofa kipato kikipungua wategrmezi wanakuwa mzigo name MTU anaanza kulalamika. No bora kusaidia inapokua lazima

  Like

 2. Mwalimu Jennifer May 6, 2014 / 5:23 am

  Engine wanajitengenezea au kuwaalika wategemezi iliwapate sofa kipato kikipungua wategrmezi wanakuwa mzigo name MTU anaanza kulalamika. No bora kusaidia inapokua lazima

  Like

 3. Mwalimu Jennifer May 6, 2014 / 5:24 am

  Engine wanajitengenezea au kuwaalika wategemezi iliwapate sofa kipato kikipungua wategrmezi wanakuwa mzigo name MTU anaanza kulalamika. No bora kusaidia inapokua lazima

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s