Nilipoandika kitabu KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIO TAJIRI na kuanza kukiuza kwa watu kuna baadhi ya watu walinipa upinzani mkubwa sana. Nakumbuka nilipokea email moja ndefu sana kutoka kwa msomaji mmoja akieleza ni jinsi gani hajapendezwa na mimi kuandika kitabu cha kuwashawishi watu wawe matajiri.

Tukiachana na watu hawa wachache neno utajiri kwenye jamii zetu hasa za kimasikini halipewi picha nzuri sana. Ukiwaambia watu unataka kupata pesa nyingi wanaanza kukuona ni mbinafsi, una tamaa ya hela na wakati mwingine kukuona kama unafanya dhambi kubwa. Lakini ni jamii hiyo hiyo utakuta imekaa na kuanza kuwajadili matajiri wakubwa kama kina Mengi na Bakhresa, kujadili wasanii au wanamichezo waliofanikiwa na kuwa na fedha nyingi sana. Ni jamii hiyo hiyo ambapo watu wanafanyishwa kazi kama watumwa huku wakilipwa fedha kidogo kuliko kazi wanayofanya na ambayo haitoshi matumizi yao. Ukiwaambia wewe unataka kuwa na fedha nyingi wanakuona wewe umepotoka, ukiwashawishi watafute njia za kupata fedha nyingi sana hawataki.

Wanapopinga kuwa na fedha nyingi kama kawaida yao wanatumia maneno yale yale kwamba fedha sio kila kitu, na fedha haiwezi kuleta furaha. Ni kweli fedha sio kila kitu ila inakuwezesha kupata karibu kila kitu unachohitaji kwenye maisha yako. Ni kweli fedha haiwezi kukupa furaha ila pia haiwezi kukuondolea furaha, na ni afadhali kulia kwenye benzi kuliko kulia kwenye baiskeli.

Kutaka kuwa na fedha nyingi sio tatizo na wala sio dhambi kubwa kama jamii inavyojiaminisha. Ila tabia mbaya ya mtu baada ya kupata fedha ndio tatizo kubwa. Hivyo kama unataka kupata fedha nyingi ili uweze kuwasaidia watu wengi soma hapa sababu kumi za kwa nini unahitaji kuwa na fedha nyingi na yeyote anayekukatisha tamaa usimsikilize.

1. Unastahili kuwa tajiri.

Kama kweli unafanya kazi kwa bidii na maarifa na kazi yako ina msaada kwa watu wengine unastahili kupata fedha nyingi. Fedha isiwe msukumo  wa wewe kufanya kazi bali unapofanya kazi ya kuwasaidia wengine ni lazima fedha zitakuja kwako. Tatizo linakuja pale aliyekuajiri anafaidia zaidi ya wewe, hapo ndipo unapodhulumiwa.

2. Fedha zipo nyingi sana.

Inakadiriwa kwenye mzunguko wa fedha wa dunia kuna dola trilioni 41. Hizi ni hela nyingi sana ambazo zinazunguka kwa wachache ila wewe umeaminishwa kuna uhaba wa hela na ukaamini. Sio kweli kwamba kuna uhaba wa hela ila kuna uhaba wa watu wanaotaka kuwa na hela nyingi kupitia kusaidia kuboresha maisha ya wengine.

3. Utaishi muda mrefu.

Japokuwa ni vigumu kuzuia kifo kwa asilimia 100, watu wenye fedha nyingi wanaishi muda mrefu kuliko watu wenye uhaba wa hela. Ili uweze kuwa na maisha marefu ni lazima upate chakula bora, uwe na huduma nzuri za afya na uepuke mazingira hatarishi. Masikini ndio wanaoshindwa kupata mlo bora, ndio wanaopata huduma mbovu za afya na ndio wanaofanya kazi na kuishi kwenye mazingira hatarishi. Yote haya yanapunguza miaka yao ya kuishi, na wewe unataka hili kweli? Hapana, tafuta fedha nyingi.

4. Mfumuko wa bei utakumeza ukiwa mzima.

Unafanya kazi yako na unapata mshahara wako wa kukutosha unasema sihitaji fedha nyingi kwa sababu hizi zinanitosha. Na kwa kuwa una uhakika utapata pensheni utakapostaafu hivyo maisha yataendelea kuwa mazuri. Uko sahihi kabida, ila naomba nikuulize swali moja, elfu kumi ya mwaka 2000 ndio elfu kumi ya mwaka huu 2014? Mfumuko wa bei unapanda kwa kasi kubwa na unashusha sana thamani ya fedha. Kama umepiga hesabu zako na kuona ukistaafu utapewa milioni 50, kumbuka miaka kumi au ishirini ijayo milioni 50 itakuwa na thamani ndogo kushinda sasa, unahitaji kutengeneza fedha nyingi zaidi.

kitabu kava tangazo

5. Usipokuwa wewe tajiri kuna mwingine atakuwa tajiri na atakutumia wewe.

Hili halina ubishi kama wewe umegoma kutafuta fedha nyingi kuna mwenzako atazitafuta na atazipata na mbaya zaidi watakutumia wewe kuzipata.

6. Utakuwa huru zaidi.

Kwa kuwa na fedha nyingi na kuwa tajiri unakuwa huru zaidi. Unaweza kupanga maisha yako yanakwendaje na unaweza kuweka vipaumbele kwenye maisha yako. Ila kama bado unatumikia mtu ili upate kuishi una mamlaka kidogo sana juu ya maisha yako. Mtoto wako anaweza kuwa anaumwa na anakuhutaji sana ila bosi wako akakuambia chagua kazi au kukaa na mtoto, huu ni unyanyasaji wa hali ya juu sana, tafuta fedha nyingi kuepuka hili.

7. Utapata huduma nzuri zaidi.

Nadhani wote ni mashahidi kwamba wenye fedha nyingi ndio wanaopata huduma nzuri kwenye kila kada ya kijamii. Huduma nzuri za afya. huduma nzuri za elimu, huduma nzuri za usafiri na kadhalika.

8. Utasikilizwa.

Jamii ya sasa japokuwa inapinga sana kuwa na hela nyingi ila wenye hela nyingi ndio wanaosikilizwa, huu ni unafiki wa kipekee unaotakiwa kukusukuma kutafuta hela nyingi zaidi. Nenda hata kwenye vikao vya familia au vya ukoo, wenye hela wakizungumza wanasikilizwa zaidi. Nenda hata kwenye nyumba za ibada wenye hela nyingi wanasikilizwa zaidi. Utalalamika na kujipa moyo kwamba na wewe ni binadamu kama wao ila nachokushauri ndugu yangu tafuta fedha zaidi.

9. Utawasaidia wengi.

Kila mmoja wetu anawatu ambao wanamtegemea au wanahitaji msaada wake. Wanaweza kuwa wazazi, ndugu wa karibu na hata familia yako. Kama una hela za kuungaunga utaishia kugombana nao au hata kukosana. Kwa sababu wewe mwenyewe una shida ya hela na ukiangalia wao wanakutegemea wewe. Hivyo kama unataka kuwasaidia watu hawa muhimu kwako kuwa na fedha nyingi na uwafundishe na wao kutengeneza fedha nyingi. Moja ya falsafa zangu kwenye maisha ni NJIA BORA YA KUMSAIDIA MASIKINI NI WEWE KUTOKUWA MASIKINI. kuwa na fedha nyingi na uwasaidie watu kwa moyo mmoja.

10. Japo fedha sio kila kitu itakupatia karibu kila kitu unachohitaji, na japo fedha haileti furaha pia haikuondolei furaha. Na unapokuwa huna furaha na wakati huohuo huna fedha unakuwa kwenye wakati mgumu sana kuliko ambae hana furaha ila ana fedha nyingi.

Kama unataka kutengeneza fedha nyingi ili uwe tajiri na kuondokana na adha tulizozungumzia hapo juu nakushauri uchukue hatua mara moja, sasa hivi sio kesho. Weka mpango wa kukupatia fedha hizo nyingi na anza kufanya kazi mara moja.

Jipatie kitabu KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIO TAJIRI na kitakuwa nguzo nzuri sana kwako kuanza safari ya kupata fedha nyingi. Kitabu hiki kinaeleza sababu 25 ambazo zinakuzuia wewe kufikia utajiri unaostahili. Kitabu kipo katika mfumo wa PDF na kinatumwa kwa email. Gharama ya kitabu ni tsh elfu tano na unatuma fedha hiyo kwa mpesa au tigo pesa(0755953887/0717396253) kisha unatuma email yako kwa meseji kwenye moja ya namba hizo na unatumiwa kitabu.

Tuache unafiki wa kujifanya kwamba hatuhitaji fedha nyingi wakati kila siku tunalalamika maisha ni magumu.

Nakutakia kila la kheri kwenye harakati zako za kuboresha maisha yako.

Kumbuka TUKO PAMOJA.