Naomba niweke wazi kwamba mimi sio msikilizaji mzuri wa redio na hivyo nyimbo nyingi zinazotoka siku hizi huwa sipati nafasi ya kuzisikia vizuri. Niliamua kuacha kusikiliza nyimbo hizi za wasanii wetu wa Kitanzania baada ya kugundua hakuna kikubwa ninachojifunza zaidi ya kuongezewa mtizamo hasi. Muda wangu ni wa thamani sana, siwezi kuthubutu kuupoteza kwa kusikiliza mtu anayeuliza nani kamwaga pombe yake au anayetaka kulewa. Mbaya zaidi ni pale mtu anapokuimbia ukiwa mjanja kuchapiwa na siri ya ndani, kwa haya na mengine yalinichosha na hivyo kupunguza mapenzi yangu juu ya nyimbo za aina hii.

Hivi karibuni nimekutana na wimbo mmoja mzuri sana ambao niliusikiliza na baadae kuutafuta na nikausikiliza mara nyingi sana. Wimbo huu ni mzuri sana na natamani kila mtanzania ausikilize na pia auelewe vizuri. Mambo mengi yaliyosemwa kwenye wimbo huu tumekuwa tukiyajadili kila siku kwenye AMKA MTANZANIA. Kuusikiliza tu na kufurahia bado haitakusaidia, ila utakapousikiliza na kuuelewa ndio unaweza kupata ujumbe mzima.

Wimbo ninaozungumzia hapa ni STAKI KAZI ulioimbwa na msanii Nikki Wa Pili. Kama bado hujasikiliza wimbo huu nitaweka link hapo chini ambapo utaweza kuupata. Kama ulishausikia nakushauri uusikilize tena na tena na tena kisha uchukue hatua.

STAKI KAZI

Hapa nitajadili mistari sita muhimu ya kujifunza kwenye wimbo huu;

1. Nimekataa kuwa mtumwa, najituma. Kataa kuwa mtumwa, jitume.

Ni kweli kwamba kuna tofauti ndogo sana kati ya kuajiriwa na utumwa. Tofauti ni kwamba kuajiriwa ni utumwa ambao huujui na hivyo kuendelea kuufurahia. Kama mtu atakupangia ni muda gani uamke, muda gani ule na hata aweze kukupangia ni kiasi gani cha fedha utapata, huwezi kujitofautisha na mtumwa. Uzuri ni kwamba nguvu ya kuondoka kwenye utumwa huu unayo, ni wewe kuamua kuchukua hatua. Soma; kama umeajiriwa na siku moja ungependa kujiajiri soma hapa.

2. Mishahara imejaa makato, biashara mjini ndio zimejaa mapato.

Kama ambavyo tumewahi kujadili hapa kwenye AMKA MTANZANIA ni vigumu sana kupata uhuru wa kifedha kupitia kuajiriwa. Hii inatokana na sababu nyingi sana ikiwemo mazingira ya kazi kuwa magumu, makato, na mishahara isiyoendana na hali ya kiuchumi. Kutokana na haya ni vyema kufanya kazi kwa malengo ili baadae kuweza kujiajiri au kuanzisha biashara ambayo itakupa uhuru mkubwa wa kifedha na maisha kwa ujumla.

3. Kazi ni mpaka wa akili yako, mpaka ufukuzwe kazi ndio ugundue kipaji chako.

Hili limekaa wazi kabisa, moja ya vitu ambavyo aliekuajiri anavifanya ili aendelee kukufanya mtumwa ni kufanya akili yako iamini kwamba maisha yako hayawezi kwenda bila ya ajira yako. Hii imewafanya wengi kudumazwa kiakili na kutumikia ajira kwa maisha yao yote. Kuonesha kwamba anachokwambia mwajiri wako ni uongo kuna watu wengi wamefukuzwa au kukosa kuajiriwa ila maisha yao ni mazuri kushinda wewe uliyeajiriwa. Hii inaonesha kwamba inawezekana kufanya mambo makubwa hata kama hujaajiriwa, hivyo kuliko kukazana kuomba kazi au kung’ang’ania kazi ambayo haikuridhishi, hebu jua vioaji vyako na uanze kuvitumia kutengeneza ajira yako mwenyewe. Kama bado hujajua vipaji vyako soma makala hii; jinsi ya kugundua vipaji vilivyoko ndani yako.

4. Elimu bongo imekosa plani ya pili, kosa la pili haufundishwi kuwa tajiri.

Hili tumeshalizungumza mara nyingi sana kwamba mfumo wetu wa elimu ni mbovu na hauendani na wakati. Hili linaashiriwa na idadi kubwa ya wahitimu tulionao huku tukiwa na nafasi finyu sana za ajira. Kama elimu yetu ingekuwa inafundisha jinsi mtu anavyoweza kutoka kimaisha bila hata ya ajira, vijana wengi wangeingia mtaani wakiwa na mtazamo tofauti. Pamoja na kukosa elimu hii muhimu usilalamike, jiunge na KISIMA CHA MAARIFA na utapata elimu hii muhimu ya maisha na utajifunza kuwa tajiri. Kwenye KISIMA CHA MAARIF mwezi huu wa saba na wa nane tunajadili jinsi ya kujenga tabia nzuri kwenye matumizi ya fedha. Kujiunga niandikie email kwenye amakirita@gmail.com nitakutumia maelekezo ya kujiunga.

5. Nakuza network najuana na watu, nauza network naunganisha watu.

Mafanikio yako kwenye kazi na hata biashara yanatokana na idadi ya watu ulionao kwenye mtandao wako. Hivyo badala ya kukazana kutafuta kazi ni vyema kutafuta mtandao mzuri ambao utakusaidia sana kwenye kujiajiri na hata biashara. Kujua zaidi kuhusu mtandao soma makala; haijalishi unajua nini bali unamjua nani.

6. Sitafuti kazi, nataka nitafutwe na wanaotafuta kazi.

   Sitaki kazi, natengeneza ajira mtaa niupe kazi.

Utakapoamua kujiajiri hutajisaidia tu wewe mwenyewe bali utaweza kuwasaidia wengine ambao hawajaweza kupata ufahamu kama wa kwako wa kuweza kujiajiri au kuanzisha biashara. Hivyo badala ya kuwa mbinafsi na kutengeneza mshahara wako tu, hebu tengeneza ajira ambazo zitakuwanya wewe kuwa huru na kuwasaidia wengi zaidi.

Wimbo huu ni mzuri sana kwa watu wote ambao wanatafuta kazi ila bado hawajapata na hata wale ambao wanafanya kazi ila hawaridhishwi na mazingira ya kazi zao au kipato wanachopata. Unao uwezo mkubwa sana wa kuweza kuchukua hatua juu ya maisha yako. Miaha hayatakuwa na maana kwako kama hufurahii kile unachokifanya.

Kwa wahitimu ambao bado mnatafuta kazi soma makala hii; Barua ya wazi kwa wahitimu ambao bado wanatafuta ajira, utapata mambo machache unayoweza kuanza kuyafanya sasa na ukasahau tatizo la ajira linalokukabili.

Kupata wimbo huu SITAKI KAZI by NICK WA PILI bonyeza maandishi hayo ya wimbo na utaupakua(download).

Nakutakia kila la kheri katika harakati zako za kuboresha maisha yako.

TUKO PAMOJA.