Kutafuta fedha ni kazi moja, na kuzitunza au kuzilinda fedha zako ni kazi nyingine ngumu zaidi ya hiyo ya kwanza. Nasema ni kazi ngumu kwa sababu wengi wetu tunajitahidi sana kutafuta fedha ila mwisho wa siku zinakokwenda hatuelewi. Hii inatokana na kushindwa kutunza fedha zetu wenyewe na kuamini kuna mtu anayeweza kuwa na uchungu na fedha zetu. Hili ni kosa kubwa sana tunafanya.

Katika kipengele hiki cha ushauri wa changamoto zinazokukabili leo tutaona kuhusu changamoto ya kutunza fedha zako mwenyewe.

Kabla hatujajadili changamoto hii, hebu tuone maoni ya baadhi ya wasomaji wenzetu walioomba ushauri kuhusiana na changamoto hii.

Mimi ni mfanya kazi wa salon lakini nikijitahidi sana kuweka pesa ya kuanzisha biashara zangu ndogo ndogo ila ndugu huja kunikopa na kunilipa inakuwa shida sasa nifanyeje?

Changamoto inayo ni rudisha nyuma ni watu wangu wakaribu wanapo nikopa pesa kurudisha inakuwa shida, ni hayo tu.

Kama tulivyoona kwa wasomaji wenzetu hapo juu kuna tatizo kubwa sana pale unapomkopesha ndugu yako fedha. Na sio ndugu pekee siku hizi mtu yeyote unayemkopesha fedha kumekuwa na tatizo kubwa sana inapofika wakati wa kulipana. Hii ni changamoto ambayo inawarudisha watu wengi sana nyuma.

Tunawezaje kuepuka changamoto hii?

Changamoto hii inaanzia pale tunapofikiri kuna mtu anaweza kuwa na uchungu sana na fedha zetu zaidi yetu sisi wenyewe, kitu ambacho hakipo kabisa. Yaani unafikiri anayekuja kukukopa anaweza kuwa na matumizi mazuri ya fedha hiyo halafu baadae atakurudishia, ni imani nzuri sana ila sio kinachotokea.

Mpaka inatokea mtu anakuja kukukopa kwa sehemu kubwa ni kwamba tayari hana matumizi mazuri ya fedha zake, na hivyo hizo unazompatia nazo hatoweza kuzitumia vizuri. Na kama huyo unayemkopesha fedha zako ni ndugu tatizo linakuwa kubwa zaidi kwa sababu sio rahisi sana kuweza kumbana akurudishie fedha zako.

Na kama mtu anakukopa fedha kwa ajili ya matumizi hapo ndio tatizo kubwa zaidi. Kwa sababu baada ya kutumia bado matatizo yake yanakuwa hayajaisha kwa sababu matumizi yake ya fedha sio mazuri.

Kuna mambo matatu unaweza kuyafanya kuepukana na changamoto hii.

1. Usikopeshe sehemu ya akiba yako.

Kama tulivyozungumza kwenye kujilipa wewe kwanza, asilimia kumi ya kipato chako unatakiwa kujilipa wewe, na fedha hii usiitumie kwenye shughuli yoyote. Kwa kuwa fedha hii huwezi kuitumia kwenye matumizi yako binafsi nakusihi pia usimkopeshe mtu kwenye sehemu hii. Hii ndio fedha unayoihifadhi kwa ajili ya kuweza kuiwekeza zaidi baadae.

Unapopata kipato chako, toa sehemu yako ya akiba, inayobaki kwa ajili ya matumizi ndio unaweza kuangalia ni kiasi gani unaweza kumkopesha ndugu yako. Usifikirie kabisa kukopesha sehemu ya akiba yako, utakufa masikini, nakuhakikishia hilo.

2. Jua matumizi ya fedha ambazo unakopwa.

Unaweza kuwa na huruma na upendo sana kwa ndugu zako wanaokukopa lakini ni vyema sana kujua fedha wanayokukopa wanakwenda kufanyia kitu gani. Kama ni kwa ajili ya kula, nakushauri usikopeshe kwa sababu, kwanza hawatakurudishia, pili hawatakufa njaa. Unapomkopesha mtu kwa ajili ya kwenda kufanya matumizi ni vigumu sana kuweza kukurudishia fedha yako kwa sababu matumizi hayana mwisho.

Angalau kama mtu anakwenda kufanya biashara au kuongeza mtaji wa biashara yake unaweza kuwa na imani kwamba utarejeshewa fedha zako.

3. Kopesha kama unatoa msaada.

Baada ya kuona unaweza kumkopesha ndugu yako sehemu ya fedha ambayo sio akiba yako na ana mpango mzuri wa kutumia fedha hiyo anayokuomba umkopeshe, mkopeshe ila hesabu umetoa msaada. Wewe usifikirie kulipwa fedha hiyo ila usimwambie kama umempa kama msaada, mwache ajue umempa kama mkopo. Hii ina faida gani, kama akikulipa utakuwa na uaminifu nae, kama atakusumbua kwenye kulipa utakuwa umejipunguzia mzigo kwa sababu hataweza kukukopa tena ikiwa hajalipa deni la nyuma.

Kwa njia hii mkopeshe mtu fedha kidogo ili kupima umaninifu wake na kama hatakuwa mwaminifu wewe ndio unakuwa umefaidika zaidi kwa sababu umempa msaada ambao hautojirudia tena.

Hizi ni baadhi ya njia chache unazoweza kutumia kukabiliana na changamoto hii ya kukopehsa ndugu.

Jambo la msingi kabisa kumbuka fedha zako unaweza kuzilinda wewe mwenyewe, usitegemee mtu mwingine akulindie.

Kwa mengi zaidi juu ya kujenga tabia nzuri ya matumizi ya fedha zako na kuweza kuongeza kipato chako jiunge na KISIMA CHA MAARIFA. Ndani ya kisima cha maarifa mwezi huu wa saba na wa nane tunajadili kuhusu kujenga tabia nzuri za matumizi ya fedha. Ni kitu kizuri sana ambacho hutakiwi kukosa, kwa sababu huu ndio utakuwa ukombozi wako wa matumizi mabovu ya fedha ambayo yanakufanya uendelee kuwa masikini.

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA tuma fedha tsh elfu kumi (10,000/=) kwa mpesa au tigo pesa 0755953887/0717396253, kama una airtel money unaweza kutuma moja kwa moja kuja tigo pesa(nenda kwenye menyu yako ya airtela money na chagua kutuma kwa tigo pesa). Baada ya kutuma fedha unatuma email yako na unaunganisha na KISIMA CHA MAARIFA.

Wahi nafasi hii nzuri ya kuboresha maisha yako, mwezi wa nane gharama za kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA zitaongezeka na mambo yatakuwa mengi na mazuri zaidi, fungua hapa kujua zaidi.

Nakutakia kila la kheri kwenye kuboresha maisha yako.

KARIBU SANA, TUKO PAMOJA.

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa kwa email amakirita@gmail.com au simu 0717396253/0755953887.

kitabu-kava-tangazo432