Njia Sita(6) Za Kudhibiti Matumizi Yako Katika Biashara .

Wafanya biashara na wajasiriamali wengi wamekuwa wakijiuliza ni ipi njia bora ya kudhibiti matumizi katika biashara. Ili kukidhi hitaji la wasomaji wa mtandao huu wa AMKA MTANZANIA, katika kona hii ya Ujasiriamali na biashara, tutaona njia mbalimbali za kudhibiti matumizi katika biashara.

Tambua kuwa Mjasiriamali yeyote ambaye atashindwa kudhibiti matumizi yake katika biashara hawezi kufanikiwa na atajikuta katika matatizo ya fedha kila wakati. Matumizi hasa yasiyo ya lazima ni tatizo kubwa miongoni mwa wajasiriamali na wasio wajasiriamali.

Fahamu kuwa matumizi ambayo siyo ya lazima yanaweza kukusababishia matatizo mbalimbali, kwa mfano matumizi yako yanapozidi unaweza ukajikuta unabaki kuwa mhanga wa madeni kwani mara kwa mara utalazimika kukopa ili kufidia mapengo ya mahitaji yako. Kuna wanaoamini kwamba ili upate fedha inabidi utumie fedha, inawezekana kukawa na ukweli, lakini watu huchukulia tofauti. Ukweli ulio wazi ni kwamba hauhitaji kutumia fedha nyingi ili kulazimisha mambo yako yaende vizuri. Jiulize kila fedha unayoitumia katika biashara yako inakuletea nini, usiwe mjasiriamali mwenye hulka ya matumizi na ambaye hajui fedha inaenda wapi! Kama ukiwa katika mwenendo huu huwezi kudumu katika uwanja huu wa Ujasiriamali na kufanikiwa.

Epuka sana tabia ya kuwa na matumizi yasiyo ya lazima kwani tabia hii itapelekea wewe kutokuweza kuona faida yoyote inayoweza kupatika katika biashara yako.

Zifuatazo ni njia sita unazoweza kuzitumia ili kuweza kudhibiti matumizi katika biashara yako.

1. Weka utaratibu wa kuweka akiba.

Wapo wajasiriamali ambao wameshindwa kujiwekea akiba kutokana na sababu mbalimbali kama vile vipato vidogo, majukumu ya kifamilia, lakini wengine wameshindwa kwakuwa hawana tabia hiyo. Ikumbukwe kwamba utamaduni wa kujiwekea akiba ni njia bora ya kudhibiti matumizi yako. Unapopata mapato toka katika bishara yako, kama ambavyo unafikiria juu ya matumizi yako, fikiria juu ya kuweka akiba kama sehemu ya matumizi.

Kumbuka kuwa wewe kama mjasiriamali, haijalishi unapata mapato kiasi gani toka kwenye biashara yako kitu kikubwa ambacho kinaweza kukukomboa ni uamuzi juu ya matumizi ya fedha ulizopata na kumbuka uamuzi utakaoufanya unaweza kukubomoa au kukujenga.

2. Pata mshauri wa biashara

Kama ambavyo huwa inasemwa maumivu yakizidi muone daktari, ndivyo ambavyo unashuriwa kuwaona wataalamu wa mambo ya biashara ili kuweza kupata msaada juu ya namna ya kudhibiti na kuweka sawa matumizi. Wataalamu wa biashara wanaweza kukusaidia juu ya uandaaji na usimamizi mzuri wa bajeti yako, namna bora ya kupunguza gharama za uendeshaji ili kuweza kupunguza matumizi. Na kumbuka wataalamu wanaweza kukusaidia kadiri ya mahitaji yako.

3. Kubali wewe una tatizo.

Kaa chini utafakari juu ya matumizi yako na jiulize kama ni ya kuridhisha ama la! Kama wewe ni mmoja wa wale wanaofanya matumizi yasiyo ya lazima katika biashara zao huna budi kwanza kukubali kwamba una tatizo. Wajasiriamali wengi hawajagundua kuwa matumizi wanayofanya wakati mwingine katika biashara zao yanachangia kwa kiasi fulani kuwarudisha nyuma, sasa kama hukubali kwamba una tatizo ni vigumu kwako kupata tiba. Fanya mchanganuo wa matumizi mbalimbali unayoyafanya kwa siku, juma au mwezi na uangalie yapi ni ya lazima na yapi si ya lazima. Matumizi ambayo si ya lazima ni yale yanayoweza kuhainishwa bila kuleta athari zozote kwa mtumiaji.

Baada ya kuona yapi ni matumizi ambayo si ya lazima njia pekee ya kuweza kujikwamua ni kukaa chini na kukubali kwamba una tatizo katika matumizi yako na kwa kugundua hivyo yafaa sasa uangalie njia zenye kufaa ili kuweza kutatua tatizo ulilonalo.

4. Simamia bajeti yako.

Bajeti ni taarifa ya fedha kwa kifupi inayoonyesha mapato tarajiwa katika biashara na matumizi yatakayofanyika kutokana na mapato husika. Sasa hapa ndipo kwenye tatizo miongoni mwa wengi. Matatizo hutokea kwa sababu matumizi ya wajasiriamali huzidi mapato wanayoyapata hivyo wakati mwingine hulazimika kukopa ili kuweza kufidia mapengo. Kama ambavyo serikali na taasisi hutengeneza bajeti zao, ndivyo ilivyo muhimu kwa wajasiriamali. Kuwa na utaratibu wa kujitengenezea bajeti utakusaidia si tu kudhibiti matumizi yako bali pia kuhakikisha mapato unayoyapata yanagusa mahitaji mbalimbali ya biashara yako. Weka makisio ya mapato yako na matumizi kwenye maandishi na uyasimamie

5. Weka tofauti kati ya matumizi binafsi na ya biashara.

Wajasiriamali wanashuriwa wakati wote kuhakikisha wanatofautisha matumizi binafsi na yale ya biashara zao. Katika kuendesha biashara kuna matumizi ya biashara mfano kodi, hii inabidi ilipwe kutokana na faida inayotokana na biashara, na yapo pia matumizi binafsi kwa mfano chakula hii inabidi yalipwe kutokana na ujira toka kwenye biashara.

Kwa kuwa wajasiriamali wengi hawajilipi mishahara kutokana na kile wanachofanya, na kwakuwa nao huwa na mahitaji yao, wao huchukua fedha toka kwenye biashara zao kukidhi mahitaji yao, kwa hali hii hupunguza mzunguko wa fedha za biashara wenyewe bila kujua. Pamoja na kutofautisha matumizi yako binafsi na ya biashara, bado unashuriwa juu ya kuwa na nidhamu katika matumizi utakayofanya. Wakati wowote unapotaka kufanya matumizi yafaa kujiuliza baadhi ya maswali ili kuwa na matumizi sahihi.

ni vizuri kujiuliza, je ni kweli unahitaji kufanya matumizi hayo, je hitaji hilo linaweza kuahirishwa, je unaweza kupata sehemu nyingine kwa bei nafuu zaidi? Maswali haya na mengine yakupe changamoto ya kufanya uamuzi na matumizi sahihi. Wakati unapotaka kufanya matumizi jipe nafasi ya kuwa na subira, jiulize hasa juu ya wewe kuwa na hitaji hilo. Wapo watu wanaofanya matumizi kwakuwa tu wameona matangazo au kufuata mkumbo, au kama njia ya kuonyesha uwezo wa kifedha.

6. Acha biashara yako ikupe mwelekeo

Kwa mfano kama biashara yako inaonyesha mwelekeo wa kufanya vizuri kuliko ulivyofikiri, kwa hali kama hii unaweza ukatafuta fedha ili kuweza kuiboresha zaidi. Ila kwa upande mwingine ikiwa biashara yako haitoi mwelekeo wenye kuridhisha huna budi kuangalia namna bora ya kuweza kupunguza matumizi zaidi. Kiasi ulichotumia mwezi uliopita sio lazima ukitumie tena mwezi huu. Sasa kitu kibaya zaidi ni kwamba utakuta biashara haifanyi vizuri na bado mtu anashikilia baadhi ya matumizi ambayo angeweza kuyaacha kwanza. Hili hutokea hasa kwa biashara ambazo ni mpya ambapo watu huamini kutumia fedha ili wapate fedha

Tambua; kuwa mafanikio katika biashara si jambo la kulala na kuamka, bali ni suala linalohitaji uvumilivu wa kweli. Hata kama unakumbana na magumu hapa na pale njia sahihi ni kutafuta namna bora ya kuweza kukabiliana nayo, na si kukata tamaa. Kupata na kupanga matumizi, ni hatua zinazohitaji uangalifu katika Ujasiriamali.

Tunakutakia mafanikio mema katika biashara yako na TUPO PAMOJA

Makala hii imeandikwa na Geofrey Mwakatika, Unaweza kutembelea blog yake Geofrey Mwakatika kujifunza zaidi.

kitabu-kava-tangazo4323

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: