Habari za siku ndugu msomaji wa mtandao huu wa AMKA MTANZANIA ni matumaini yangu unaendelea vizuri katika harakati zako za kutafuta mafanikio na uhuru wako wa kifedha. Katika kona yetu ya Ujasiriamali na biashara, tutajifunza kanuni muhimu za Ujasiriamali. Tambua kuwa Katika shughuli au biashara yoyote unayofanya au unayotarajia kufanya, ni lazima uwe na mtazamo chanya ili ufanikiwe. Ujasiriamali una kanuni zake ambazo ni muhimu sana kuzijua na kuzifuata ili kuyafikia mafanikio ya kweli. Ili ufanikiwe katika Ujasiriamali kama ilivyo katika shughuli nyingine yoyote, lazima ufuate kanuni na misingi iliyowekwa. Kinyume na hapo, mafanikio huwa magumu sana. Zifuatazo ni kanuni sita muhimu za Ujasiriamali.

1. Jitume na ipende kazi unayoifanya

Ili ufanikiwe katika biashara yoyote, lazima uwe na moyo wa kujituma na uipende kazi unayoifanya. Usisubiri kusukumwa kwa sababu hakuna atakayefanya kazi hiyo. Jifunze kuwahi kuamka asubuhi ili uendane na kasi ya soko, jitume kufanya mambo yatakayoiboresha biashara yako bila kuchoka na fanya kazi kwa moyo wako wote.

2. Kuwa na uwezo wa kuisimamia biashara yako

Wewe Kama Mjasiriamali ni lazima uwe na uwezo wa kuongoza na kusimamia biashara yako na kutoa maamuzi sahihi mara zote. Katika Ujasiriamali, uwezo wa kusimamia na kuwaongoza watu walio chini yako ni muhimu sana kwani hata kama ukianza na biashara ndogo, lazima baadaye itakuwa kubwa hivyo utalazimika kuajiri watu wengine wa kukusaidia. Endapo utakosa uwezo wa kuwasimamia, ni dhahiri kwamba watakuibia, watafanya kazi tofauti na ulivyotegemea na mwisho utaanguka kibiashara.

3. Kuthubutu

Hapa nazungumzia uwezo na utayari wa kufanya uamuzi mgumu wa kuingia katika biashara au mradi fulani huku ukiwa umeondoa nidhamu ya woga. Watu wengi ni waoga wa kuchukua hatua au kuthubutu kuingia katika biashara. Wengi wanaogopa kupata hasara, kuanguka mtaji au kufilisika. Mjasiriamali bora ni lazima awe na uwezo wa kuthubutu kufanya mambo makubwa lakini uthubutu huo uendane na utafiti wa kina. Usiwekeze sehemu ambayo hujafanya utafiti wa kutosha.

4. Kuwa na Nidhamu

Nidhamu ni muhimu sana katika biashara, matumizi ya pesa, muda, nidhamu kwa wateja na kila kitu kinachohusu shughuli zako zinazokuingizia kipato. Nidhamu ni chanzo cha mafanikio kwani ndiyo inayosimamia sehemu kubwa ya biashara zako.

5. Kuwa makini

Wale waliofanikiwa siyo tu walikuwa tayari kufanya kazi bali waliweka umakini mkubwa katika kazi walizokuwa wakifanya. Mjasiriamali anatakiwa kuwa mwangalifu kwa kila jambo, anatakiwa kujua soko linaendaje na pia ni lazima awe na uelewa wa kutambua mabadiliko yanayojitokeza katika soko, uzalishaji na uendeshaji kwa jumla.

6. Kuwa mwaminifu

Uaminifu ni silaha kubwa itakayokulinda mjasiriamali na kuwafanya watu wengi wapende kufanya biashara na wewe. Jifunze kulipa madeni hata kama ni madogo unapodaiwa, wauzie wateja wako huduma au bidhaa kwa bei halali, lipia kodi na vibali vyote muhimu. Kamwe usiwauzie watu bidhaa zilizokwisha muda wake, zenye ubora hafifu au mbovu kwani kwa kufanya hivyo, wateja watakukimbia na huo ndiyo utakuwa mwisho wa biashara yako. Endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa mambo mazuri ya kujielimisha na kujihamasisha na kuwa bora zaidi jiunge na KISIMA CHA MAARIFA.

TUNAKUTAKIA MAFANIKIO MEMA KATIKA UJASIRIAMALI NA BIASHARA YAKO

TUPO PAMOJA.

Makala hii imeandikwa na Geofrey Mwakatika, Unaweza kutembelea blog yake Geofrey Mwakatika kujifunza zaidi.

kitabu-kava-tangazo4323