Habari za siku nyingi ndugu msomaji wa AMKA MTANZANIA ni matumaini yangu unaendelea vyema katika safari ya kuboresha maisha yako na kama ni hivyo basi ni vizuri sana na pia endelea kuweka juhudi katika kila jambo unalolifanya kwani hakuna nguvu yoyote ile inayopotea. Kuna mafanikio makubwa sana yanakungoja wewe kwa hiyo endelea kupambana na wala usikate tamaa.

Baada ya kusema hayo tugeukie katika mada yetu ya leo ambayo itazungumzia suala zima la furaha. Tambua kuwa Unaweza ukafanya maisha yako yakawa na furaha, ni chaguo lako tu. Ni tabia yako ndiyo inaweza kufanya maisha yako yakawa na furaha au huzuni. Tunakutana na hali mbalimbali kila siku, na baadhi ya hizo hazina mchango wa kuleta furaha. Hata hivyo, tunaweza kuchagua kuendelea kufikiria matukio yanayotukosesha furaha, na pia tunaweza kuchagua kukataa kuyafikiria, na badala yake, kufikiria juu ya mambo ya furaha na amani.

Sote tunakutana na mambo mengi katika maisha ambayo yanaweza kutusababishia ukosefu wa furaha, lakini, tunapaswa kutoyaruhusu yalete athari hii katika maisha yetu. Kama tukiruhusu matukio yetu yaingilie hali zetu, tutakuwa watumwa. Tutakosa uhuru. Tutaruhusu furaha zetu zitegemee matukio ya nje. Kwa upande mwingine tunaweza kujikomboa kutoka katika hali za nje. Tunaweza kuchagua kuwa na furaha. Na tunaweza kufanya kila liwezekanalo kuongeza furaha katika maisha yetu.

SOMA; Mambo KUMI Ya Kufanya Ili Usiishi Maisha Ya Majuto.

Furaha ni nini?

Furaha ni hisia za amani ya ndani na kuridhika nafsi. Siku zote huonekana, wakati ambao hakuna hofu, woga au fikra za kuwa na woga. Siku zote hili hutokea pale tunapofanya kitu tunachokipenda, au pale tunapopata, tunaposhinda au kufanikisha kitu tunachokithamini. Inaonekana kuwa ni matokeo ya hali nzuri kabisa katika maisha. Lakini hii hutoka ndani ya nafsi yako ikiamriwa na matukio ya nje.

Kwa watu wengi sana furaha huonekana ni jambo la muda mfupi sana, kwasababu huruhusu matokeo ya nje kuathiri mfumo wa furaha yao. Moja ya njia bora kabisa ya kuidumisha ni kwa kuongeza amani ya ndani ya nafsi kwa kufanya meditation kila siku. Kadiri akili inavyozidi kuwa na amani, ndivyo jinsi urahisi wa kuchagua tabia yenye furaha unavyokuwa.

SOMA; Kauli Mbili Za Kuacha Kutumia Leo, Maana Zinaashiria Kushindwa.

Jitahidi siku zote kuangalia mambo mazuri, hata kama akili yako itakulazimisha kuangalia mambo mabaya, usiiruhusu kabisa kufanya hivyo. Angalia upande chanya katika kila hali unayokutana nayo. Hii ni rahisi ikiwa utajitahidi kuwa na nguvu ya hiari pamoja na dhana ya kujiheshimu. Fikiria juu ya utatuzi wa tatizo na sio kufikiria juu ya tatizo. Angalia vipindi vyenye kuleta furaha na kuchekesha katika TV. Kila siku, tenga muda wa kusoma kitabu chenye hadithi zenye kuvutia au makala zenye mvuto. Kuwa mwangalifu na fikra zako, pale utakapoona unaangukia katika kufikiria upande hasi, haraka sana geuza fikra zako katika upande chanya.

SOMA; Sababu TATU Kwa Nini Watu Wengi Wanashinda Kufikia Mafanikio.

Siku zote angalia juu ya kile ulichokifanya na sio kile ambacho hukukifanya. Unaweza kuwa na mipango yako unayotaka kukamilisha katika siku yako, hatimaye mwisho wa siku unajikuta hujakamilisha yote hivyo hali hii inaweza kukukosesha furaha kufikiria yale uliyoshindwa kuyakamilisha. Yatengee siku nyingine kwani kuyafikiria sana na kuumiza kichwa kunaweza kukukatisha tamaa na kuacha kuyafanya tena. Usikae ukafikiria juu ya mambo yasiyowezekana hata kidogo, mfano kukaa unafikiria juu ya kupaa angani. Jifanyie kitu fulani kizuri kila siku. Inaweza kuwa kitu fulani kidogo,kama vile kununua kitabu, kula kitu unachokipenda. Kuangalia kipindi cha TV unachokipenda zaidi, au kwenda kutembea sehemu unayoipenda. Kama unaweza kila siku fanya kitu au kitendo ambacho kitawafurahisha wengine. Mfano inaweza kuwa ni neno, kuwasaidia wanafunzi wenzako au wafanyakazi wenzako, kusimamisha gari yako kuruhusu watu wavuke, kumpisha mtu katika kiti ndani ya gari, au kumpa zawadi hata kama ndogo tu Yule unayempenda. Unapomfanya mtu kuwa na furaha, wewe pia vilevile utakuwa na furaha, na watu watajitahidi kukufanya uwe na furaha.

SOMA; Unataka Kuiona Dunia? Vua Miwani…

Tarajia kuwa na furaha siku zote na sio huzuni. Weka fikra za mafanikio yako mbele na uhakika wake bila ya kufikiria vikwazo. Jiunge na ujumuike na watu wenye furaha, na jaribu kujifunza kutoka kwao kuwa na furaha, wachunguze sababu zao zinazowafanya wawe na furaha ili ujue ni jinsi gani ya kuwaiga. Usiwachukize watu wenye furaha, kinyume chake, kuwa na furaha kwa furaha zao. Fanya kila uwezalo kuepukana na hisia za kushawishika na hali fulani au jambo fulani, hii itakusaidia kuwa mtulivu na kudhibiti hali yako na matendo yako. Hali ya kutoshawishika ni nzuri sana kwani huongeza amani ya ndani ya nafsi, na amani ya ndani ndiyo matokeo ya furaha. Tabasamu siku zote. Usiwe mtu mwenye hasira na kununa hovyo.

Tunakutakia kila kheri katika safari yako ya mafanikio, daima kuwa na mtizamo chanya katika kila jambo unalolifanya ili uweze kujiletea mafanikio yenye furaha tele maishani.

TUPO PAMOJA

Makala hii imeandikwa na Geofrey Mwakatika, Unaweza kutembelea blog yake Geofrey Mwakatika kujifunza zaidi.

kitabu-kava-tangazo4323