Kuna usemi mmoja maarufu sana unaosema “ukiendelea kufanya unachofanya sasa, utaendelea kupata matokeo unayopata sasa”. Kwa lugha nyingine kama unataka kubadili matokeo yako, ni lazima uanze kwa kubadili kile unachofanya.

Ili uweze kufikia mafanikio zaidi ya uliyonayo sasa, kwa sababu mpaka hapo ulipo tayari una mafanikio, unahitaji kubadili njia unazotumia sasa. Na kitu cha kwanza kabisa kubadili ni uzalishaji wako.

Uzalishaji tunaozungumzia hapa ni ile kazi au thamani unayotoa kwa wengine kwa muda unaofanya kazi. Hivyo kama utazalisha thamani zaidi kwa muda mfupi maana yake una uzalishaji mkubwa. Na hii ni njia nzuri ya kufikia mafanikio kwenye chochote unafanya, iwe ni kazi au biashara.

Kiuchumi, utajiri au thamani ya kampuni, mtu binafsi na hata jamii kwa ujumla unapimwa kwa ongezeko la uzalishaji.

SOMA; Sifa TATU Unazohitaji Ili Kufanikiwa Kwenye Ujasiriamali.

Leo UTAJIONGEZA na hatua tano unazoweza kutumia na ukaongeza uzalishaji wako na hatimaye kufikia mafanikio zaidi.

Hatua ya kwanza na rahisi kabisa ya kuongeza uzalishaji wako ni kuwa bora kwenye majukumu yako. Kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na kuendelea kujifunza zaidi. Kama unafanya biashara, ijue vizuri biashara yako na ongeza juhudi. Kama umeajiriwa, unajua majukumu yako kikazi, yatekeleze vizuri.

Hatua ya pili ni kutafuta mtu ambae anaweza kufanya hiko unachofanya na kwa bei rahisi kisha unampa afanye. Kama ni mfanyabiashara maana yake unatafuta watu wa kukusaidia. Kama ni ajira unafanya kazi na watu wengine ambao wanakusaidia. Ukweli ni kwamba kazi inayofanyika kwa timu inafanyika kwa uzalishaji mkubwa.

SOMA; Tabia Mbaya KUMI(10) Zinazopunguza Ufanisi Wako.

Hatua ya tatu ya kuongeza uzalishaji ni kutumia teknolojia iliyopo. Hapa unatafuta njia ambayo teknolojia inaweza kurahisisha kazi unazofanya. Kwa mfano badala ya kuandika kila barua kwa mkono, inaweza kuandikwa moja na zikatolewa kopi na mashine. Kila kazi inaweza kusaidiwa na teknolojia.

Hatua ya nne ni kuvumbua teknolojia mpya inayoweza kurahisisha kazi zako. Na ukifikia hatua hii unakuwa umetatua tatizo la wengi. Inawezekana kwa kila kazi unayofanya kuvumbua njia rahisi ya kiteknolojia ya kuirahisisha.

Hatua ya tano na ya mwisho ya kuongeza uzalishaji wako ni kujua vitu vinavyoleta uzalishaji mkubwa kwako na kufanya hivyo tu. vingine vyote unaacha kuvifanya kwa sababu vinakupotezea muda. Kwa mfano asilimia 80 ya mafanikio yako inatokana na asilimia 20 ya kazi unazofanya. Je ni kazi zipi hizo zinakuletea faida kubwa? Zijue kazi hizi na zifanye kwa ufanisi mkubwa na utaongeza uzalishaji wako.

SOMA; SIRI YA 4 YA MAFANIKIO; Itumie Sheria Ya Wastani Kukuletea Mafanikio.

Mwisho wa siku kinachoongeza uzalishaji ni pale unapojua kile chenye faida kwako na kukifanya. Hii ndio inayoleta faida kwenye makampuni, biashara na hata kazi. Wale wanaojaribu kufanya kila kitu huishia kuwa na uzalishaji mdogo. Wale wanaochagua vichache na kuvifanya vizuri huwa na uzalishaji mkubwa.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz