Mpenzi msomaji wa mtandao huu wa AMKA MTANZANIA ni siku nyingine tena tunakutana hapa katika kushauriana na kushirikishana mambo mbalimbali yatakayotusaidia katika kuboresha masiha yetu ya kila siku. Tambua kuwa bahati yako ya kupata mafanikio ipo mikononi mwako na ili uweze kuiona bahati yako ni lazima ufanye kazi kwa bidii na maarifa. Fahamu kuwa mtu yeyote anayependa mafanikio na kuamua kupambana ili kufikia malengo yake, ni lazima atafanikiwa. Mafanikio hayo yatatokana na jitihada pamoja na bidii anayoionyesha mtu huyo. Mtu ambaye hataki kujikwamua kutoka katika hali ya dhiki aliyonayo, atabakia kuwa maskini na tegemezi. Utajiri wa watu wale wanaofanya jitihada na hata kufanikiwa hautamsaidia mtu ambaye hapendi kujishughulisha.

BIASHARA2

SOMA; Mambo 5 Yanayoashiria Kuwa Hutaki Mafanikio.

Fahamu kuwa Kama hautapenda kujikwamua kutoka katika hali ya dhiki uliyonayo, na kuendeleza kutotaka kujifunza ili kuondoka katika tabu yako, wenye akili watatumia juhudi na maarifa yao na kukuzidi katika hali ya kuwa na mafanikio. Kama utakuwa mwenye upumbavu, busara za wengine hazitakuongoza. Kama utapoteza muda na pesa zako, uchumi wa wengine utafikia kikomo na kukufedhehesha. Unapokuwa na mafanikio binafsi unakuwa na nguvu katika kufanikisha mambo mbalimbali unayotarajia, ndiyo maana kila mtu peke yake anafanya jitihada za kutaka kujikwamua kutoka kwenye umaskini. Katika jamii tunayoishi, kila mmoja wetu ni mjasiriamali. Kila mmoja ni kiongozi wa maisha yake. Hivyo atawajibika katika mafanikio na kushindwa ambako kutaweza kutokea katika maisha yake.

SOMA ;Kama Una Tabia Hizi 30 Tayari Wewe Ni Mjasiriamali, Chukua Hatua

Tambua kuwa Wewe na familia yako ni wadau katika biashara yako, na ni jukumu lako kuhakikisha kuwa thamani ya mahitaji ya biashara zako yanakuwepo kwa miaka yote.Wakati unaendelea kuendesha biashara yako inayoendelea kukua, inawezekana kabisa kama utaamua kupunguza mahitaji makubwa uliyonayo, ili uwezekusimamia vizuri pesa ulizonazo, kusimamia vizuri suala la uzalishaji, mauzo na kufanya utafiti. Pasipokuwa na mtaji wa kutosha, hakuna uzalishaji. Bila uzalishaji, biashara yako itakuwa haina kitu cha kuuza. Bila bidhaa, shirika lako litasimamisha uzalishaji. Na bila utafiti, washirika wako hawatakuwa na imani ya kuendelea kuwepo katika biashara hiyo kwa siku zijazo.

SOMA ; Njia Bora Ya Kusimamia Fedha Zako Katika Biashara.

Suala la kutumia akili yako ya kuzaliwa ni la muhimu sana. Utafiti unaonyesha kuwa mara nyingi mtu anayefanikiwa ni yule ambaye anatumia akili yake katika kumpatia faida. Na Kufanikiwa kwa mtu huyo kusikufanye na wewe ukaanzisha biashara kama yake, kwani unaweza kukwama. Kinachotakiwa ni kuchekecha akili yako na kuamua kufanya biashara ambayo utaimudu.

SOMA;Hivi Ndivyo Mawazo Hasi Yanavyoua Biashara Yako.

Mafanikio katika biashara yako ya kifedha yanakuja kutokana na uongozi mzuri katika biashara yako unayoisimamia. Hakuna milango iliyo wazi katika suala la mafanikio, ni lazima ufanye utafiti, uweke malengo na kutimiza ndoto yako uliyoipanga. Japo kuna misuko suko mbalimbali katika kufikia mafanikio hayo. Ukosefu wa nafasi isiwe sababu ya kutoa udhuru katika mipango yako inayoshindikana kutokana na kuwepo kwa vikwazo mbalimbali unavyoviruhusu wewe mwenyewe.

Kila maisha unayoyaishi yana nafasi nzuri ya mafanikio. tunaishi katika dunia ambayo wakati wote ina uwezekano wa kuwa na utajiri mwingi. Pia fahamu kuwa Maisha ni somo, na kila somo, linapokujia ni nafasi kwako ya kujifunza. Kila biashara unayoipitia ni nafasi kwako ya kujifunza. Unapowaza juu ya watu unaowafahamu waliofanikiwa, hiyo ni nafasi nzuri kwako ya kujifunza kutoka kwao. Uwepo wako ni upendeleo wa pekee wa kukufanya uongeze bidii katika mipango yako, na pale unapopata bahati hiyo, nafasi yako ya mafanikio inakuja kwa haraka.

SOMA;Hatua Sita Za Kubadili Maisha Yako Na Kufikia Mafanikio Makubwa.

Watu wenye mafanikio wanaamini kuwa kila kitu kinawezekana. Wote hao ambao binafsi wameyakubali maisha na changamoto zake na kuzifanyia kazi changamoto hizo katika mafanikio. Acha kulalamika kutokana na bahati mbaya uliyokumbana nayo au jambo baya lililokupata, amua kuwa na nafasi ya kubadilika. Kuna kitu ambacho unaweza kukifanya vyema zaidi ya mtu mwingine. Ni nini hicho? Tafuta mpaka pale utakapopata eneo lako ambalo utafanya vizuri na kuzidi wengine. Halafu upange mipango yako ukinuia kuwa utafanikiwa. Kamwe usipende kuwa mtu wa kushindwa ila wewe ndiye unayeweza kupata mafanikio. Inawezekana kabisa mtu aliyezaliwa katika familia maskini, akakua katika hali ya umaskini, akasoma kwa shida na matatizo mengi, hatimaye mtu huyo akaja kuwa tajiri mkubwa. Mifano mingi tunayokutana nayo ni ya watu walioishi katika hali duni, kutokana na hali ile wakaamua kubadilika na kuwa watu tofauti katika dunia tunayoiishi na wengi wao wamefanikiwa, ni matajiri wanaishi maisha ya raha. Watu hao mara zote wamekuwa wakiwausia watoto wao kuishi maisha ya kujituma na kufanya bidii ili watakapokua waweze kuwa na mafanikio, pia wasitegemee utajiri wa wazazi wao.

SOMA ; Tabia KUMI Za Watu Waliofanikiwa Sana

Kamwe usikate tamaa, wala kuvunjika moyo. Utavuna kesho kile ulichokipanda leo. Kila siku unatakiwa kujiuliza: “Siku hii ya leo kwangu ina maana gani?” Utakapofanya maamuzi juu ya siku hiyo, utakuwa tayari kwa kutumia uzoefu ulionao wa kufanya jambo lile ambalo umelipanga. Uamuzi wa mafanikio upo kwako, hivyo usivunjike moyo katika hatua unayoichukua ya kufanikisha malengo yako. tunakutakia mafanikio mema katika maisha yako, daima tupo pamoja katika safari hii ya kuboresha maisha yetu. Endelea kutembelea mtandao huu kwa makala bora zaidi na pia unaweza kujipatia kitabu chaBIASHARA NA UJASIRIAMALI, hakikisha unajipatia kitabu hiki ili uweze kuwa bora katika uwanja huu wa biashara na Ujasiriamali .kupata kitabu hiki bonyeza hapa BIASHARA NA UJASIRIAMALI, daima tupo pamoja katika safari hii ya kuboresha maisha yetu. TUPO PAMOJA

Makala hii imeandikwa na Geofrey Mwakatika, Unaweza kutembelea blog yake Geofrey Mwakatika kujifunza zaidi.