Siku sio nyingi nilipata nafasi ya kuzungumza na kijana ambaye anatafuta ajira kwa muda sasa bila ya mafanikio. Hali hii ilikuwa inamuumiza sana na alikuwa akihitaji ushauri wa mambo mengine ya kufanya wakati anaendelea na mchakato wa kupata ajira.

Baada ya mazungumzo ya kile cha tofauti alichokuwa akifikiria kufanya, tuligusia swala la ajira na nilitaka kujua anaonaje changamoto hiyo. Alinieleza jinsi ambavyo ajira ilivyo ngumu kupata ila bado hajakata tamaa, anajua siku moja atapata ajira.

Fani aliyosomea kijana huyu ni mahusiano ya umma(public relations). Na aliona kama fani hii haina nafasi nyingi za kazi ndio maana ajira zimekuwa ngumu. Hapa ndipo nilipopata picha tofauti ya changamoto yake. Nilimuuliza kama anajua kampuni nyingi hazina maafisa hawa wa habari au wa mahusiano(PR) na akaniambia anajua hilo. Aliendelea kusema kwamba makampuni haya hayataki kuajiri. Nilimuuliza je makampuni hayo yanajua umuhimu wa mtu wa fani hiyo? Je wakipata mtu wa kuwaonesha kwa nini wanahitaji huduma hiyo na akawa anawapatia na ikawanufaisha huoni kwamba watafurahia?

Hiki ndio kitu kikubwa ambacho nakuandikia wewe kijana mwenzangu unayesoma barua hii maalumu kwako. Na hata kama unasoma ila haupo kwenye changamoto hii bado unaweza kutumia utakachojifunza kwenye kazi yako au hata biashara yako.

SOMA; Hii Ni Kazi Yenye Malipo Makubwa Sana Ambayo Unaweza Kujifunza Kuifanya

Kampuni haziajiri.

Kampuni nyingi haziajiri. Na sio kwamba zote ambazo haziajiri hazina uhitaji, kila kampuni ina uhitaji mkubwa wa rasilimali watu. Ila kuna vikwazo viwili vinavyoweza kuzuia kampuni nyingi zisiajiri.

1. Kuepuka mzigo. Katika nyakati hizi ambapo biashara zimekuwa za ushindani na changamoto nyingi, kila kampuni inajitahidi kupunguza gharama za uendeshaji au uzalishaji. Hivyo hakuna kampuni inayoweka kipaumbele wkenye kuajiri mpaka iwe ni muhimu sana.

2. Kutoona umuhimu. Sababu nyingine muhimu inayoweza kuifanya kampuni isiajiri ni kutokuona umuhimu wa baadhi ya nafasi za kazi. Mara nyingi kampuni inashindwakujua kwamba kwa kuajiri mtu wa fani fulani anaweza kuifanya kampuni ikastawi sana. Na hivyo kutokujisumbua kuajiri watu wa fani hiyo.

Sasa unafanya nini?

Lengo la barua hii ni kutaka kukupa wewe mbinu mbadala ya kulitatua tatizo hili la ajira. Kila mtu anayetafuta ajira, anaandika barua ya maombi, anaweka wasifu wake na kisha kupeleka. Anakaa nyumbani akisubiri kuitwa kwenye usaili. Katika usaili huu anakutana na wenzake wengi ambao wote wana sifa sawa na hivyo nafasi ya kupata ajira ile inakuwa ndogo sana. Hapo bado hujaweka kujuana na upendeleo wa aina nyingine.

Kuendelea na njia hii kutaendelea kukuweka kwenye kundi kubwa ambalo ni vigumu sana wewe kuonekana na kupewa nafasi. Ninachotaka kukushauri hapa ni wewe kuondokana na kundi hili kubwa. Kujiweka pembeni ambapo kutakufanya iwe rahisi kwako kuonekana na kuchukuliwa.

Unachohitaji kufanya kwenye njia hii ninayokushirikisha ni rahisi sana, ila kinahitaji kujituma.

Chagua kampuni au shirika ambalo unataka kulifanyia kazi. Anza kujifunza kuhusu kampuni au shirika hilo. Pata taarifa nyingi uwezavyo. Na wakati huu linganisha utaalamu uliosomea na matatizo ambayo kampuni au shirika linayapata kwa kukosa mtu makini wa fani hii. Baada ya kujua changamoto zote ambazo kampuni hiyo inapitia, andika ni jinsi gani wewe kwa taaluma yako utaweza kuisaidia kampuni hiyo kuondokana na changamoto hizo.

Baada ya kufikiria yote haya andika pendekezo(proposal) ukieleza changamoto za kampuni na jinsi ambavyo wewe unaweza kusaidia kuondokana nazo. Andika vizuri kiasi kwamba mtu yeyote anayesoma pendekezo lako hilo ataelewa vizuri na ataona umuhimu wako. Pia kwenye pendekezo hilo weka njia mbalimbali ambazo kampuni inaweza kufanya kazi na wewe. Unaweza kuweka njia ya kukupa wewe mkataba wa muda kwa ajili ya kusaidia hilo, au wakuajiri ili uweze kuwafanyia kazi hiyo.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Wahitimu Ambao Bado Wanatafuta Ajira.(Kama Bado Unazunguka Na Bahasha Soma Hapa)

Sasa hebu niambie kama ungekuwa ndio unaendesha kampuni ambayo ina changamoto nyingi, halafu ukapokea barua 100, barua 99 wanaomba kazi na barua 1 amekuja na mapendekezo ya jinsi ya kuiondoka kampuni hiyo kwenye changamoto, ungetoa kipaumbele kwa nani? Wale 99 ay huyu mmoja?

Nafikiri unaona ni jinsi gani ambavyo unaweza kubadili nafasi ya wewe kupata ajira kwa kubadili mbinu ambazo unatumia. Kwa kutumia mbinu hii ya kuandika mapendekezo, unaondokana na changamoto zote mbili za kampuni kushindwa kuajiri hapo juu. Kwanza hutakuwa mzigo kwao kwa sababu utapendekeza njia bora ya wao kufanya kazi na wewe na pia utakuwa umewaonesha umuhimu wa fani fulani ambayo wao walikuwa hawajaona umuhimu huo.

Hakuna mtu anayetaka kuajiri mtu aje kuwa mzigo kwake, unapojiweka kwenye nafasi ya kuwa muhimu, nafasi ya kuongeza thamani, watu wengi wataliona hilo.

Kwa kijana mwenzetu ambaye amesomea mahusiano ya umma, nilimwambia aangalie kampuni ambazo hazina taswira nzuri kwa umma na aziandikie mapendekezo ni jinsi gani anawezakufanya nazo kazi na akazisaidia kuwa na taswira nzuri kwa umma.

SOMA; Katika Kula Ujana Usifanye Mambo Haya Matano, Utajutia Maisha Yako Yote.

Unachosema hakiwezekani.

Kama baada ya yote hayo mawazo yako ni kwamba hakiwezekani sina njia nyingine ambayo naweza kukusaidia. Ukweli ni kwamba hutaandikia kampuni moja mapendekezo halafu ukakaa na kufikiri watakutafuta haraka sana. Wanaweza wasikutafute kabisa. Muhimu ni wewe kuandikia kampuni nyingi uwezavyo. Kama umekaa nyumbani kwa mwaka mzima au zaidi ukitembeza tu bahasha, unaona ugumu gani kwa sasa kuanza kufuatilia makampuni mengi na kuyaandikia mapendekezo. Andikia kampuni 10, 20 hata 30. Katika hizi 30 huenda 5 wakakujibu au kukutafuta na huenda ukapata moja ya kuanza nayo.

Kama bado unatafuta kazi, usikatae hili, jaribu kuliweka kwenye mipango yako, jaribu kulifanyia kazi na hata kama hutapata kazi kwa njia hii angalau utakuwa umeshazijua changamoto nyingi za kampuni zinazohusiana na fani yako na hivyo kuweza kutoa ushawishi zaidi wakati mwingine utakapopata nafasi ya kufanyiwa usaili.

Jaribu njia hii niliyokueleza hapa, hakuna utakachopoteza na una vingi sana utakavyopata.

Unapochagua njia hii hakikisha unajituma kweli na unakuwa mtu wa kufikiria, unakuwa mbunifu na usiwe mtu wa kukata tamaa.

Je utatumia njia hii? Kama kuna sehemu ambayo utahitaji maelekezo zaidi niandikie kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Nakutakia kila la kheri kwenye mipango yako unayokwenda kuitekeleza.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

kitabu-kava-tangazo4322