Habari ndugu msomaji wa makala za kilimo. Natumaini waendelea vyema na Safari ya mafanikio. Niwashukuru sana kwa kuendelea kufuatilia makala hizi za kilimo na kuwaeleza wengine nao wazifutilie. Ninafarijika sana kuona watu wanasaidika na kile kinachoandikwa hapa japo hua tunaweka kwa kifupi na kwa lugha nyepesi ambayo kila mtu anaweza kusoma na kuelewa. Wiki hii nimepokea simu, ujumbe mfupi na hata barua pepe kadhaa za watu kuonyesha kunufaika na mafundisho haya. Wiki iliyopita tuliweza kujifunza kutokana na ripoti inayoonyesha mauzo ya mazao ya bustani yalivyoongezeka kuuzwa nchi za nje. Leo hii nitapenda tujifunze kwa ufupi teknolojia ya mbegu na hasa tutakwenda moja kwa moja katika kuzitambua aina za mbegu na matumizi yake.

kilimo2

Bila kumumunya maneno kufanikiwa katika kilimo kunategemea sana na ubora wa mbegu ulizo tumia. Watu wengi kwa kutokutambua wamekua na mazoea ya kutumia mbegu ni mbegu pasipokutambua kwamba ubora wa mazao unategemea sana ubora wa mbegu. Kama ukitumia mbegu zisizofaa, lazima utakua na mavuno duni. Mavuno bora yanatokana na mbegu bora.

SOMA; Tabia Saba Za Watu Wasiokuwa Na Mafanikio.

Mbegu za mazao kwa Tanzania

Takwimu zinaonyesha kwamba Tanzania inauhitaji wa tani 120,000 za mbegu kwa mwaka lakini zinazopatikana kwa wakulima ni chini ya tani 30,000 ambapo ni sawa na asilimia 25 ya uhitaji ndio inapatikana. Pia kwa Tanzania katika kiasi kinachopatikana cha mbegu asilimia 30 ndio inayozalishwa hapa nchi wakati asilimia 70 ya mbegu zinaagizwa kutoka nje ya nchi kupitia makampuni mbalimbali binafsi. Hapa nchini kuna zaidi ya makampuni 55 yaliyosajiliwa kwa ajili ya shughuli za uzalishaji na uuzaji wa mbegu. Pamoja na kuwepo kwa makampuni hayo 55 bado suala la mbegu bora ni changamoto kubwa sana. Kwanzachangamoto kubwa ni ukosefu wa elimu/uelewa kwa wakulima kuhusu umuhimu wa mbegu bora. Pili Upatikanaji wa mbegu bora haukidhi uhitaji uliopo, hii imepelekea kuibuka kwa biashara ya mbegu feki na biashara hii inakua kwa kasi, hivyo wakulima wengi kukosa imani na hizo zinazoitwa mbegu bora.

SOMA; Weka Mayai Yako Yote Kwenye Kikapu Kimoja, Halafu Fanya Hivi….

Mifumo ya mbegu

Kuna aina mbili ya mifumo ya upatikanaji wa mbegu katika nchi yetu ya Tanzania. Kwanza ni mfumo rasmi wa mbegu ambao unaendeshwa na soko. Katika mfumo rasmi tafiti zinafanyika na kugundua uhitaji wa soko na hivyo mbegu kuzalishwa kuendana na soko. Lakini pia mbegu zinazalishwa kulingana na uhitaji wa ki hali ya hewa. Ndio maana utasikia mbegu hii ni ya ukanda wa juu, au ukanda wa chini au wa kati. Au unasikia mbegu hii inavumilia ukame, au haishambuliwi na wadudu n.k. Hii ni utafiti unafanyika na kugundua uhitaji uliopo na kuzalisha kukidhi uhitaji huo.

Mfumo usio rasmi: Huu ndio mfumo uliotawala ijapokua siku zinavyozidi kwenda unapungua. Katika mfumo huu watu wanatumia mbegu marejeo (yaani mazao waliyovuna msimu uliopita walihifadhi baadhi na kufanya kua mbegu). Kaika mfumo huu watu wamekua wakiazima mbegu kutoka kwa jirani zao au marafiki bila kujua chanzo cha mbegu au pia bila kujua aina haswa ya mbegu, na hii ipo sana kwa wakulima hasa wa mpunga, maharagwe, mahindi n.k Mfumo huu unakabiliwa na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabia nchi.

SOMA; BIASHARA LEO; Njia TANO Rahisi Za Kutangaza Biashara Yako.

Aina za mbegu

Kuna aina mbili za mbegu; Mbegu za kawaida (OPV) na mbegu chotara (Hybrid). Wakulima wengi wamekua wakishangaa kwanini kuna tofauti mkubwa wa bei kati ya mbegu na mbegu ya zao moja. Mfano mbegu ya mahindi ya STUKA mfuko wa kilo 2 ni shilingi 4,000 wakati mbegu ya PIONEER, au FARU ya ujazo huohuo ni shilingi 7,500 mpaka 8,000.

Mbegu za kawaida: Hizi ni mbegu ambazo zinazalishwa kwa njia ya kawaida, uchavushaji wake haudhibitiwi sana. Ni rahisi kushambuliwa na wadudu na magonjwa, Ila pia mavuno yake huwa ya kawaida.

Mbegu chotara: Hizi ni aina ya mbegu ambazo uchavushaji wake unathibitiwa kwa kiwango cha juu kuhakikisha kwamba hakuna mwingiliano wowote wa poleni nje ya chanzo kilichokusudiwa. Mimea ya mbegu chotara hua na mfanano wa hali ya juu (uniformity) na hivyo kuwa na ubora unahitajika na soko rasmi. Pia Mbegu chotara huweza kuvumilia au kua na ukinzani dhidi ya baadhi magonjwa. lakini kikubwa katika mbegu chotara ni uhakika wa mazao, uzalishaji unaongezeka zaidi ya mara 2 ukilinganisha na mbegu za kawaida. Japo kua mbegu zake ni ghali tunashauriwa kutumia mbegu za chotara kwa uhakika wa mazao, ughali wake unatokana na gharama kubwa za kutengeneza na kuzalisha mbegu chotara.Zipo kampuni mbili ambazo ni za kiholanzi (Enza Zaden na RIJK ZWAAN) zinafanya vizuri sana katika uzalishaji wa mbegu chotara za mbogamboga duniani na moja wapo nimewahi kufanya kazi kwenye tawi lake la Tanzania.Kwa Tanzania zipo kampuni kadhaa ambazo zinazalisha mbegu chotara. Mfano ni BaltonTanzania,EastAfricaseed, Kibo seed, SEED CO, SUBA AGRO n.k Baadhi ya mazao ana mbegu za kawaida na mbegu chotara (Mfano Mahindi, Nyanya, Vitunguu, mpunga, matikiti maji, kabeji pilipili hoho n.k ), na juhudi zinaendelea kufanyika kwa mazao mengine kupata mbegu chotara. Kuweza kutambua kwa urahisi mbegu nyingi za chotara zinaishia na jina F1, Mfano Anna F1.

SOMA; Kitu Hiki Kimoja Ni Muhimu Kuliko Kiwango Cha Fedha Unachotaka.

Ushauri: Zingatia yafuatayo

1. Hakikisha mbegu unayonunua imethibitishwa. Mbegu kabla haijaruhusiwa kutumika lazima ithibitishwe na taasisi ya kuthibitisha mbegu TOSCI. Hakikisha mfuko wa mbegu ulionunua una stika yenye namba (Lotnumber).

2. Tumia mbegu chotara kwa uhakika wa mazao bora. Usikubali kuanza na mbegu zisizoeleweka. Mavuno bora huanza na mbegu bora

3. Kama kuna uwezekano wa kununua moja kwa moja kwa kampuni ni vyema zaidi kuliko kununua kwa wakala. Usinunue mbegu kwenye minada. Hii itapunguza uwezekano wa kuuziwa mbegu feki.

4. Hakikisha unanunua mbegu zinazohitajika sokoni na zinaendana na hali ya hewa na udongo wa mahali husika

5. Hakikisha unaponunua mbegu unachukua risiti. Hii itakusaidia endapo umeuziwa mbegu feki, na mamlaka husika zikathibitisha ni mbegu feki, utatakiwa kulipwa fidia

6. Hakikisha unafuata ushauri wa kitaalamu.

Asanteni

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

Makala imeangaliwa muundona lugha fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makalaza Kiswahili na Mjasiriamali Email: rumishaelnjau@gmail.comsimu 0713 683422.

KARIBU KWENYE SEMINA YA MAFANIKIO KUPITIA BIASHARA MWAKA 2015.

AMKA CONSULTANTS imekuandalia semina ya mafanikio kwenye biashara mwaka 2015. Katika semina hii utajifunz amambo yote muhimu yatakayokuwezesha kuanza, kukuza na kufikia mafanikio kwenye biashara yako. Semina itaanza tarehe 04/05/2015 na itaendeshwa kwa mwezi mzima kwa njia ya mtandao(yaani email). Mwisho wa kujiunga na semina hii ni tarehe 01/05/2015. Wahi sasa kujiunga ili upate maarifa yatakayokuwezesha kufanikiwa kwenye biashara. Kwa maelezo zaidi na jinsi ya kujiunga bonyeza maandishi haya.