Kama Hutengenezi Hiki Mahali Ulipo Hustahili Kulipwa Chochote.


Ndugu msomaji wa JIONGEZE UFAHAMU salamu. Karibu katika makala yangu ya leo. Napenda kutumia wasaa huu kuzungumza na wewe japo kwa ufupi kuhusu maisha. Katika maisha tumekuwa tukifanya mambo mengi sana, mengine yana faida lakini mengine mengi ni ya hasara sana kwetu hasa ukizingatia kwamba muda tulio nao hapa duniani ni mfupi sana na umehesabiwa na aliyetuumba, hivyo katika kila unachofanya ni vyema sana ukautumia muda wako vizuri kwani hutaweza kamwe kupata nyongeza ya japo saa moja kwa siku ili yafike 25.
Ndugu msomaji nikiandika hapa najua unasoma kwa sababu kuna kitu cha muhimu ambacho najua utakwenda kukipata. Unajua unapofanya kitu chochote katika dunia hii kuna malipo ambayo kwa kiasi kikubwa unayategemea ambayo yanaweza kuwa katika vitu au isiwe katika vitu (material and non-material things). Kwa wengi mategemeo haya yamekuwa yakiwasukuma kufanya kazi na kupata hicho wanachokitarajia. Kama ni mfanyakazi unategemea upate mshahara na marupurupu na kama ni mfanyabiashara unategemea kupata faida. Lakini hata kama wewe ni mwanafunzi nawe unahitaji kufaulu katika hatima ya masomo yako. Najua na naelewa vyema kuwa hakuna mtu atakayekupa hayo yote kama hakuna ulichokifanya.
Ndugu msomaji huwezi kulipwa kwa sababu wewe unafanya kazi saa nyingi kwa siku, huwezi kulipwa kwa sababu wewe una elimu kubwa wala huwezi kulipwa kwa sababu wewe ni mtanashati au mrembo sana. Utalipwa tu kama umefanya jambo lenye thamani. Kama hutatengeneza thamani yoyote kazini, shuleni, biasharani au popote pale ambapo wewe unapaswa kuwapo basi hustahili kulipwa chochote na wakati mwingine unastahili adhabu. Thamani utakayoitengeneza katika kile unachokifanya itatoa mchango katika nyanja za maisha ambazo wewe umezisimamia. Mchango wako katika sehemu ndio pia ambao utakupa furaha na kukuongezea uwezo wa kujiamini. Huwezi kujiamini kama hujatekeleza yale ambayo unapaswa wewe kuyafanya.
Ili uweze kutengeneza thamani katika kile ambacho unakifanya ni lazima kwanza uutumie vyema muda wako katika kufanya yale yenye thamani kubwa kwako kwanza kabla ya yale yenye thamani ndogo na pia kufanya jambo moja kwa wakati mmoja na sio kushika mambo elfu kwa wakati mmoja. Ukweli ni kwamba utafanya yote lakini hakuna hata moja ambalo utalifanya kwa ubora wake na hivyo kuondoa thamani yake. Kuwa yule mtu ambaye akikosekana sehemu kwa muda mfupi umuhimu wake unaweza kuonekana na thamani yake yaweze pia kuonekana. Kama ulipo hauna thamani ni muda wa wewe kujiongezea thamani au uondoke kwani hakuna utofauti wa wewe kuwepo ama kutokuwepo. Ninaposema fanya jambo moja kwa wakati mmoja (focus) namaanisha kuwa fanya kile unachokikusudia kukifanya tu na si vinginevyo. Mathalani upo kazini lakini unachokifanya ni kupiga soga, kutembelea mitandao ya kijamii na kutega tega kazi kiasi kwamba kufikia muda wa kuondoka unakuwa umetumia chini ya asilimia sabini katika kazi na kuwa na mzigo wa kuufanya unaporudi nyumbani. Kwa wale washabiki wa mpira wanajua thamani ya mchezaji haitokani na chenga anazopiga au kasi yake uwanjani bali idadi na uwezo wake wa kufunga magoli. Kumbuka katika mpira wa miguu chenye thamani ni magoli ambayo ndiyo huleta ushindi.
Labda nikupe mfano mdogo, wewe ni meneja masoko wa kampuni fulani na unaona mwenendo wa kampuni sio mzuri katika mauzo unaweza kubuni mbinu mpya na kuongeza mauzo. Katika hili umetengeneza thamani na wewe umeongeza thamani yako pia. Kwa maana hiyo unaweza kumfuata bosi wako na kumwambia akuongeze mshahara naye bila shaka atakubali kulingana na faida unazoleta.
Ni wakati wa wewe kukaa chini sasa na kutafakari kuhusu thamani yako sehemu uliyopo. Ongeza thamani yako na wewe pia utafaidika. Usikae kulalamika kuwa mshahara hauongezewi wakati bosi wako haoni unachokifanya. Usitegemee kufanya jambo lile lile kwa namna ile ile na utegemee kuongeza thamani bali badili namna unavyoenenda nawe utaona mafanikio.
Mwisho nirudie kwa kusema kuwa thamani yako mahali ulipo haitokani na kiasi gani muda unaokaa kazini, kiwango cha elimu ulicho nacho, uzuri, au uwezo wako bali kitu kimoja tu ambacho ni thamani unayotengeneza.
Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes
Unaweza kuwasiliana na nae kwa: simu: 0712 843030/0753 843030
                                                                     e-mail: nmyohanes@gmail.com
Pia unaweza kutembelea blog yake:  www.lifeadventurestz.blogspot.com kujifunza zaidi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s